Wahimizwa kukuza elimu ya jinsia

NA DIRAMAKINI

WANAWAKE katika vyombo vya habari hawakupewa nafasi kubwa na hivyo uwakilishi wao bado umekuwa mdogo katika maudhui, nafasi za uongozi na hata wakati wa kupewa aina za habari za kufuatilia.

Picha na Getty Images.

Akizungumza hivi karibuni katika mafunzo ya siku moja kuhusu muongozo wa kufundishia wa masuala ya jinsia katika vyuo vya uandishi wa habari, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania, Kajubi Mukajanga, alisema kuwa kuna haja ya makusudi ya kuimarisha taswira ya wanawake katika vyombo vya habari na hivyo wakufunzi wa vyuo wanahitajika kupewa kipaumbele.

“Hakuna taifa linaloweza kuendelea ikiwa tutaiwacha nyuma jinsia moja, hivyo vyombo vya habari vinahitaji mipango imara ya kuimarisha sauti za wanawake na masuala ya jinsia yanazingatiwa katika vyombo vya habari,”alisisitiza katika mafunzo hayo yaliyofanyika kwa njia ya mtandao.

Alisema kuwa,Baraza la Habari limekuwa likiimarisha shughuli zake zote kwa kuangalia jinsia na mafunzo hayo ni mojawapo ya shughuli hizo za baraza hivyo kutoa wito maalum kwa wakufunzi kutumia vyema muongozo huo .

Alisema kuwa, moja wapo ya shughuli za baraza kwa sasa ni kuimarisha masuala ya usawa wa jinsia katika vyombo vya habari, hivyo kumekuwa na programu tofauti ikiwemo kutoa mafunzo ya wanawake katika vyombo vya habari na uongozi, mafunzo ya habari za uchunguzi pamoja na kuimarisha weledi na umahiri waandishi chipukizi wanawake kwa kupata mbinu za utendaji kwa kuwaambatanisha na waandishi wabobevu.

Akiwasilisha mada kuhusu muongozo wa kufundisha kuhusu Jinsia, Mtaalamu Elekezi wa Masuala ya Habari, Pili Mtambalike alisema kuwa, muongozo huo utakuwa ni dira elekezi katika kutoa elimu ya jinsia na vyombo vya habari ili wakufunzi waweze kuimarisha utendaji wa kazi zao.

Alisema kuwa, bado masuala ya jinsia na vyombo vya habari hayakuimarishwa katika vyuo na taasisi za habari hivyo ni dhahiri kuwa muongozo utakuwa na mawanda mapana ya mbinu na mikakati ya kufundisha vijana waliopo katika vyuo masuala ya Jinsia na vyombo vya habari.

“Tafiti mbali mbali zilizofanywa zimebainsha kuwa bado kuna pengo katika masuala ya jinsia na vyombo vya habari, kuanzia maudhui hadi katika uongozi hivyo kuna haja ya kubadili yaliyopo ili haki na usawa wa jinsia katika vyombo vya habari viweze kupatikana,”alifafanua.

Masuala ya jinsia kamwe yasiwe somo moja bali yapewe kipaumbele katika maeneo yote ya habari kuanzia katika habari, makala, vipindi ili kuimarisha jinsia katika vyombo vya habari.

“Muongozo ukitumika vizuri ni dhahiri kuwa utajenga waandishi imara ambao watakuwa ni watekelezaji wa haki na usawa wa jinsia katika vyombo vya habari,” aliongeza.

Vyuo vina nafasi nzuri ya kutoa waandishi ambao watakuwa mahiri katika masuala ya jinsia katika utendaji wao na pia kuwa ni chachu ya mabadiliko katika vyombo vya habari. “Waandishi hao wawe ni nguvu ya kuleta mabadiliko,”alifafanua.

Wakichangia katika mafunzo hayo ya siku moja ya wakufunzi wa vyuo vya habari hapa nchini walisema kuwa muongozo huo ni muhimu na ni hazina ambayo itapaswa kutumiwa kwa vitendo katika vyuo hivyo ili kuimarisha dhana ya usawa wa jinsia katika vyombo vya habari.

Dkt.Rehema Kilagwa kutoka chuo kikuu cha Kiislamu Morogoro alisema kuwa, waandishi wanafunzi nao wanapaswa kuwa imara ili kutekeleza kwa vitendo masuala ya haki na usawa katika kazi zao.

“Walimu tuna dhima ya kuwaongoza wanafunzi ili waweze kujua masuala ya haki na usawa wa jinisia lakini pia sisi tuwe mfano wa kuigwa katika kuimarisha masuala hayo,”alifafanua.

Athumani Gamba kutoka cha Uandishi Habari cha Dar es salaam alisema kuwa, bado suala la jinsia lipo zaidi kinadharia hivyo juhudi zinahitajika katika kuimarisha suala hilo kwa vitendo.

Aidha, sera ya jinsia na vyombo vya habari haina budi kusambazwa katika vyuo ili nayo iwe muongozo katika suala hilo.

Irene Chizenga kutoka The Arusha East African Training Institute (AEATI), alisema suala la kujiamini ni muhimu katika haki na usawa wa jinsia hivyo wakufunzi wanatakiwa kuimarisha kujiamini kwa wanafunzi ili wawe imara katika kuimarisha weledi na umahiri katika fani ya uandishi wa habari ambao utazingatia haki na usawa wa jinsia.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliwashirikisha wakufunzi 11 kutoka vyuo mbalimbali vya habari hapa nchini na ni mojawapo ya shughuli za kuimarisha haki na usawa wa jinsia katika vyombo vya habari chini ya mradi wa wanawake na vyombo vya habari unaofadhiliwa na shirika la VIKES chini ya ufadhili wa serikali ya Finland.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news