Rais Dkt.Mwinyi awataka wataalam wa afya nchini kutoa huduma bora za afya

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, wauguzi na wakunga katika hospitali za Zanzibar wanatakiwa kutoa huduma nzuri na bora ili kwenda sambamba na juhudi zinazofanywa na Serikali kuboresha sekta ya afya.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Desemba 20, 2022 wakati wa sherehe ya kumpongeza kwa kufikisha miaka miwili tangu aingie madarakani.

Ni sherehe zilizoandaliwa na wauguzi pamoja na wakunga wa hospitali za Zanzibar zilizofanyika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi jijini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Dkt.Rajab Mohammed Bilal,wakati akitembelea banda la maonesho la Kitengo cha Macho la Wizara ya Afya Zanzibar katika viwanja vya Chuo Cha Utalii Maruhubi Wilaya ya Mjini Unguja, wakati wa sherehe za kumpongeza kwa kutimiza miaka miwili ya uongozi wake zilizoandaliwa na Wauguzi Zanzibar katika ukumbi wa Chuo hicho,kulia kwa Rais ni Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Ahmed Nassor Mazrui na kushoto kwa Rais ni Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Hassan K.Hafidh.(Picha na Ikulu).

Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa, jitihada zinapaswa kuongezwa kusomesha wanataaluma zaidi kuhakikisha huduma bora zaidi zinapatikana katika hospitali nchini pamoja na zile mpya zinazoendelea kumaliziwa kujengwa.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi, alisema pia ili kuboresha huduma za afya nchini kuna umuhimu wa kutoa fursa kwa baadhi ya huduma zitolewe na hospitali binafsi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Tuzo Maalum ya Kutimiza Miaka Miwili ya Uongozi wake,iliyotolewa na Wauguzi Zanzibar akikabidhiwa na Muunguzi Bi. Maryam Rashid Suleiman, wakati wa sherehe za kumpongeza zilizofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi Unguja.

Wakati huo huo amesema,baada ya hospitali zinazojengwa kukamilika zisiwe na uzuri wa majengo yanayopendeza bali huduma zitakazotolewa ziwe bora zaidi ili kuendana na majengo yenyewe.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameridhia kuanzishwe Kurugenzi ya Afya katika Wizara ya Afya ili kurahisisha utoaji wa huduma za afya nchini.

Hata hivyo, kuhusu ombi la wauguzi la posho maalum,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameahidi kuzitatua changamoto hizo mara baada ya ukaguzi wa hesabu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news