NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefika Ofisi za Ubalozi mdogo wa China uliopo Mazizini jijini Zanzibar na kutia saini kitabu cha maombolezo kutokana kifo cha aliyewahi kuwa Rais wa China, Jiang Zemin (96).
Katika salamu zake Dkt.Mwinyi amesema, amepokea kwa masikitiko na huzuni taarifa za kifo cha Rais wa zamani wa China Hayati Jiang Zemin, aliyefariki dunia Novemba 30, 2022 kutokana na sababu za ugonjwa wa saratani ya damu.
Amesema Komredi Jiang Zemin atakumbukwa kwa kuwa kiongozi bora na Mwanamapinduzi, aliyekuwa chachu ya ushirikiano kati ya China na Afrika.
Pia amesema, Hayati Zemin atabakia daima katika kumbukumbu kwa kuzingatia ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Taifa hilo na Zanzibar na Tanznaia kwa ujumla.