Rais Dkt.Mwinyi akoleza kasi ya kufuatilia vipaumbele, mikakati ya Serikali yake

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema ili Taifa liweze kupata mafanikio, kunahitajika uwepo wa vipaumbele na shabaha zinazoweza kupimika, sambamba na mipango ilio makini na ufuatiliaji. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe, Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipokuwa akitoa hutuba yake katika hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya Afisi ya Rais ya Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini “Presidential Delivery Bureau”(PDB) katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo.(Picha na Ikulu).

Dkt. Mwinyi amesema hayo leo Desemba 2, 2022 katika Uzinduzi wa Taasisi ya Ofisi ya Rais ya Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (PDB), hafla iliofanyika katika Viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar.

Amesema, mafanikio yanahitaji kuwepo kwa vipaumbele, mipango makini ya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuweza kutatua matatizo yanayojitokeza na kuepuka ucheleweshaji.

Pia amesema, jukumu kubwa la PDB ni kuhakikisha kunakuwepo utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa kwa wakati unaofaa.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, kwa kuanzia utekelezaji wa vipaumbele hivyo utahusisha sekta nne za miundombinu, Utalii, Maendeleo ya Kijamii pamoja na Uchumi wa Buluu.

Ameeleza kuwa, PDB ni kitengo maalum kilichopo chini ya ofisi yake, kinachoundwa na timu ya wataalamu walioajiriwa kwa utaratibu wa ushindani na uwazi.

Amesema taasisi hiyo itaondoa vikwazo, kubaini uhaba wa rasilimali na masuala mengine yanayoweza kuchelewesha maendeleo, ili kufanikisha lengo la utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi.

Amewataka viongozi na watendaji Serikali kubadilisha na kuharakisha njia za kufanyia kazi kwa kuondokana utendaji na mazoea. Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na waalikwa mbalimbali wakiwa katika hafla ya Uzinduzi wa Taasisi ya Afisi ya Rais ya Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (Presidential Delivery Bureau-(PDB) iliyozinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe, Dkt. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo.

Aidha, amesema ili kufikia mafanikio, Taifa linapaswa kujifunza kutoka kwa wengine na kukubali usaidizi kutoka kwa wahisani na marafiki, kama vile Taasisi ya Tony Blair (TBI) na UNDP, huku mkazo ukiwekwa katika kuwajengea uwezo watendaji.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar kushirikiana na taasisi hiyo, huku kila mmoja akiwajibika kwa nafasi yake.

Naye Waziri wa Nchi (OR) Ikulu, Jamal Kassimu Ali alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyektii wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuona haja na umuhimu wa kuanzisha taasisi hiyo na kubainisha imani aliyonayo kuwa itamsaidia kukamilisha dhamira yake katika kipindi cha Uongozi wake.

Aidha, alitoa pongezi kwaTaasisi za Tony Blair, Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na timu nzima ya Watendaji wa PDB kwa kufanikisha uanzishaji wa taasisi hiyo.

Mapema, Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Christine Musisi aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kazi kubwa ya kuhakikisha inakuwa karibu na wananchi kwa kuweka mazingira mazuri na sekta zote na kufanyakazi kwa ufanisi.

Amesema ili kufanikisha dhamira ya kutoa huduma bora kwa wananchi ni lazima kuwepo vipaumbele na akatumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kuanzisha taasisi hiyo. Baadhi ya Watendaji wa Taasisi ya Ofisi ya Rais ya Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (Presidential Delivery Bureau (PDB)) wakiwa katika hafla ya Uzinduzi wa taasisi hiyo iliyozinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe, Dkt. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar leo. 

Ameeleza kuwa, PDB itakuwa daraja la kuunganisha mahitaji ya Serikali, sekta binafsi pamoja na wananchi katika utekelezaji wa malengo ya Taifa na yale ya Kimataifa. Sambamba na hayo alisema UNDP itaendelea kushirikiana na Serikali katika utatuzi wa changamoto mbali mbali.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa na Kimataifa, wakiwemo Mawaziri, Mabalozi, Washirka wa Maendeleo, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa Dini.

Post a Comment

0 Comments