Rais Dkt.Mwinyi:Tunaifungua Pemba kiuchumi

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti na Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar amesema, Serikali ya Awamu ya Nane imekusudia kuifungua Pemba kiuchumi.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia wana CCM na wananchi wa mikoa ya Pemba alipofika kutoa shukurani zake katika Uwanja wa Tibirinzi kwa kuchaguliwa kwake katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa 10, kushika nafasi hiyo ya juu katika CCM. (Picha na Ikulu).

Ameyasema hayo Desemba 17, 2022 wakati akihutubia wanachama wa CCM na wananchi wa mikoa ya Pemba alipofika kutoa shukurani zake katika Uwanja wa Tibirinzi baada ya hivi karibuni kupata ushindi wa kishindo katika nafasi ya juu ndani ya chama.

Kupitia uchaguzi wa chama ambao ulifanyika jijini Dodoma, Rais Dkt.Mwinyi alipata kura 1,912 kati ya kura zote 1,915 zilizopigwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 10 wa CCM.

"Tunaifungua Pemba. Hauwezi kuleta maendeleo kama nchi haijafunguka, nikisema nchi kufunguka maana yake nini, maana yake ni viwanja vya ndege, maana yake ni bandari, maana yake ni barabara. Kwa hivyo kwa uwanja wa ndege kama mlivyosikia, tayari fedha zimeshapatikana.
"Za kuufanya Uwanja wa Ndege Pemba kuwa Uwanja wa Kimataifa, tunatarajia kazi hiyo itaanza ili uwanja wetu huu uwe wa Kimataifa, ndege kutoka nje ya nchi zije moja kwa moja Pemba,"amesema.

Kwa upande wa bandari,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema,Bandari ya Mkoani imeshaanza kujengwa ikiwemo Bandari ya Shumba.

"Lakini na Bandari ya Wete, mipango ipo katika hatua nzuri ili tuweze kupata fedha tuijenge Bandari ya Wete, tuifungue Pemba kwa maana ya bandari,"amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi..
Kwa upande wa Barabara amesema kuwa,Barabara ya Chake- Wete tayari mkandarasi yupo kazini, lakini pia fedha zimeshapatikana kwa ajili ya barabara ya Chake- Mkoani.

"Sina shaka tukishafungua maeneo haya matatu. Ya viwanja vya ndege, ya bandari, ya barabara uchumi wa Pemba utakuwa mkubwa zaidi na yale tuliyoyakusudia yataweza kupatikana,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar.

Katika mkutano huo, wananchi kutoka mikoa ya Pemba wameonesha kuwa na imani kubwa na uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi kwa namna ambavyo anatekeleza ahadi mbalimbali alizozitoa kupitia kampeni zake wakati wa uchaguzi pamoja na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wananchi wamesema, wataendelea kuunga mkono jitihada zake hizo ili Zanzibar iweze kupata maendeleo yaliyokusudiwa kupitia Serikali ya Awamu ya Nane ambayo imejikita kuwahudumia wananchi wote Unguja na Pemba.

Hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi alisisitiza kuwa, kipaumbele kikubwa hivi sasa katika serikali anayoiongoza ni kufikia uchumi wa buluu.

Aliyasema hayo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na kuhudhuriwa na Waziri Ofisi ya Rais Fedha na Mipango,Dkt.Saada Mkuya Salum.

Rais Dkt.Mwinyi alisema, kwa sasa Serikali inafanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia rasilimali zilizopo za bahari.

Pia alisema, kwa sasa serikali inatarajia kutumia vema rasilimali hizo ili kufikia azma ya mageuzi hayo ya kiuchumi ambapo tayari sera ya uchumi wa buluu imeshatengenezwa.

Alisema, malengo hayo yanategemea sana uwepo wa miundombinu ya barabara,bandari,maji na nishati ya uhakika ya umeme hivyo maeneo hayo kwa sasa ndio kipaumbele katika serikali.

Naye Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania,Dkt.Patricia Laverley alisema, benki hiyo inatambua jitihada kubwa za mageuzi ya kiuchumi zinazofanya na Rais Dkt.Mwinyi kupitia mwelekeo wa uchumi wa buluu.

Alisema, kupitia mwelekeo huo wa uchumi wa buluu ambao kwa kiasi kikubwa una rasilimali za kutosha za baharini utawanufaisha Wanzanzibari katika eneo la uvuvi,kilimo cha zao la mwani na viwanda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news