Waziri Simbachawene:Niwaombeni wazazi muache watoto wasome

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene amempongeza Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iramba kwa kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba huku akiwataka wazazi kuwacha watoto wasome kwani Serikali inatoa elimu bure.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu,Mhe. George Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Iramba.

Kauli hiyo ameitoa katika ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Kata ya Rudi iliyopo Jimbo la Kibakwe Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambapo alifanya mkutano wa hadhara na kutembelea mradi wa maji.

“Ameweza kufaulisha wanafunzi 32 kati ya wanafunzi 40 baada ya kuwaahidi kwenda Bungeni mjini Dodoma, wanafunzi hao wamefaulu kwa wastani wa daraja B na Daraja C.

"Watoto wana akili sana ila wazazi wao wanawaambia wasifaulu kwa sababu hawana fedha ya kuwasomesha, hivyo mvuruge mvuruge majibu ili msifaulu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene akizungumza katika mkutano wa hadhara Kijiji cha Iramba.

“Nchi hii inataka watu wasomi, mwezi wa kwanza nitawapeleka bungeni Mjini Dodoma, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetangaza elimu bure ya msingi na sekondari hakuna ada.

"Dunia ya leo inahitaji watu wenye maarifa, tunasoma kwa ajili ya kuondoa ujinga niwaombeni wazazi muache watoto wasome,"amesema Waaziri Simbachawene.

Naye Mwalimu Yasinta Chipanjile wa Shule ya Msingi Iramba amesema, amepata changamoto katika kipindi cha miaka miwili kutokana na kushindwa kucheza na akili za wazazi.

“Tunakwenda vizuri mitihani ya kata, mitihani ya ujirani mwema, lakini kwenye mitihani ya kitaifa watoto hawafanyi vizuri kutokana na kikao cha kifamilia kinachofanyika wiki moja au siku mbili kabla ili kuwazuia watoto wasifaulu,"amesema Mwalimu Yasinta.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu (Mb) Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Iramba.

Amefafanua alichukua sauti ya Waziri iliyotoa ari ya wanafunzi kufaulu kuanzia watoto 30 ili waweze kutembelea bunge, na kutembea na kauli hiyo mpaka wakati wa mtihani yao ya kitaifa.

“Katika ufaulu huo wavulana walikuwa 12 na wasichana 20 ufaulu ambao haujawahi kutokea tangu shule ya msingi Iramba ianzishwe, kutokana na shinikizo la wazazi kwa watoto kutengeneza matokeo ya E,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news