Rais Samia anavyoivusha Sekta ya Habari kutoka madhila ya miaka kadhaa-2

NA GODFREY NNKO

“Kosa la kashfa halina uzito mkubwa kama linapogeuzwa kuwa jinai, na walipoliweka hilo ni kwamba wanataka kukomoa. Sasa hapo mwandishi anachukuliwa kama muhujumu uchumi, hii ni hatari sana,”amesema Maregesi, Endelea...
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye tangu aingie madarakani, Serikali yake imekuwa rafiki mwema na Sekta ya Habari nchini na tayari ametoa nafasi kwa ajili ya kufikia hatua za maboresho ya sheria ambazo zinadaiwa ni kandamizi katika sekta hiyo nchini.

ZINAZOHUSIANA

Rais Samia anavyoivusha Sekta ya Habari kutoka madhila ya miaka kadhaa 

Naye Regina Mkonde kutoka Mwanahalisi Digital amesema, kosa la kashfa kugeuzwa jinai kunamuweka mwandishi katika hatari zaidi na kumjaza hofu.

Ufafanuzi

Akieleza ufafanuzi wa vifungu hivyo, Wakili wa kujitegemea James Marenga amesema, hatua ya kosa la kashfa kugeuzwa jinai, inaongeza hofu na sintofahamu kwa wanahabari nchini.

“Vifungu vya 35, 36, 50(1)(a)(ii) vinafanya kosa la kashfa kuwa ni kosa la jinai badala ya kuwa ni kosa la madai. Tunapendekeza kuwa, mashauri yote yatakayotokana na kashfa yaendeshwe kama kesi za madai sio jinai,” ameeleza Wakili Marenga.

Amesema, madhumuni ni kuhakikisha vikwazo katika uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza vinaondolewa nchini ili kuifanya Sekta ya Habari kuwa imara na iweze kustawi.

Mwanasheria huyo amesema, kugeuza kashfa kuwa ya jinai kunaleta hofu na kufifisha haki ya kujieleza na kutoa maoni.

“Kifungu cha 37 kinasema kwamba, uchapishaji wa kashfa ni kosa la jinai isipokuwa kama jambo lililochapishwa ni la kweli na limechapishwa kwa manufaa ya umma, pia kama uchapishaji huo umetolewa kama upendeleo wa kutoshitakiwa (privileged) kwa kashfa na ulikuwa ni manufaa kwa umma,”amesema.

Amesema, kama uchapishaji huo umetolewa kama upendeleo wa kutoshitakiwa (privileged) kwa kashfa na ulikuwa ni manufaa kwa umma, kifungu hicho cha sheria hakijaweka vigezo vingine vinavyoonesha kuwa uchapishaji wa kashfa sio kosa la jinai.

Sheria rafiki

Wakili James Marenga amesema,sheria rafiki kwa vyombo vya habari ni miongoni mwa nguzo muhimu ambayo itawawezesha wadau wote wa habari wakiwemo waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kujiamini bila kukinzana na sheria kwa manufa ya Serikali na umma nchini.

Marenga alikuwa akiangazia vifungu mbalimbali vya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 vikiwemo vile ambavyo vinaonekana kuwa chanya kwa ustawi bora wa jamii na Taifa.

Sambamba na vifungu ambavyo wadau wanaona kuna haja ya Serikali kuvifanyia maboresho au kuvifuta kabisa kwa kuwa, vina changamoto ili kuiwezesha tasnia ya habari na wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Wakili Marenga amesema, kwa ujumla wake sheria hiyo imeweka baadhi ya maneno ambayo yanaweza kutumiwa vibaya na mahakama huku tafsiri ya maneno hayo ikiwa imefichwa.

Wakili Marenga ametaja baadhi ya maneno yenye mitego katika sheria hiyo kuwa ni pamoja na, ‘kwa namna nyingine’ ama ‘kusudio na kinyume cha sheria.’

“Neno kama ‘kwa namna nyingine ama kusudio na kinyume cha sheria,’ ni maneno hatari yanayotumika hasa kuharamisha jambo ambalo sio kosa kisheria. Maneno haya unaweza kuyaona kuwa ya kawaida, lakini ni hatari sana,” amesema Wakili Marenga.

Wakili Marenga amesema, kwenye sheria hiyo kuna adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia amesema, sheria hiyo kupitia Kifungu 7 (i)(g) imevuruga uhuru wa faragha ambapo taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.

“Sheria hii katika Kifungu cha 50(2)(b) kinaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila muhusika kuwepo.

“Hukumu ikitolewa, ndio unatafutwa na kufungwa bila kujua kesi yako ilipelekwa mahakamani lini, na kwa kosa gani. Ndio maana tunasema sheria hii inatakiwa kupitiwa upya,”amesema Wakili Marenga.

Wakili Marenga amesema, sheria hiyo inayohusu makosa yanayohusiana na mifumo ya kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) iliwasilishwa Machi, 2015 bungeni kwa hati ya dharura na ilipitisha na Bunge tarehe Mosi Aprili, 2015 na kuidhiniswa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 25, 2015.

"Ni sheria ambazo zilikwenda kwa mfumo wa hati ya dharura tunasema certificate of agency,"amesema.

Sheria imetibu

Amesema, sheria hiyo licha ya mapungufu iliyo nayo inatibu mambo mbalimbali kwa ustawi bora wa jamii hususani kwa upande wa maadili, hivyo wadau wanaamini ikifanyiwa maboresho au vifungu vyenye mikinzano kufutwa huenda ikwa miongoni mwa sheria bora nchini

Maeneo chanya;-

-Kusimamia utoaji na ukusanyaji wa maudhui katika mtandao,

-Kudhibiti picha za ngono (wakubwa/watoto),

-Utoaji wa taarifa za uongo,

-Ujumbe unaotumwa bila ridhaa,

-Matusi ya kibaguzi,

-Unyanyasaji kupitia mtandao kula njjama ya kutenda kosa,

- Ukiukwaji wa haki bunifu;

Wakili Marenga amesema kuwa, miongoni mwa vifungu muhimu kwa ustawi bora wa jamii na Taifa katika sheria hiyo ni 39-49 ambavyo vinazungumzia kuhusu usimamizi wa maudhui ya mitandao.

"Sheria imekuja kutibu baadhi ya hayo mambo, sheria hii jambo muhimu ambalo inafanya ni kusimamia ukusanyaji wa maudhui katika mtandao. Hii ni sehemu muhimu sana ya sheria,ndio sababu ina control maudhui kuhusu nini kirushwe na nini kisirushwe na mambo mengine yanayohusiana na Usalama wa Taifa.

"Kudhibiti na kupiga marufuku picha za ngono ambayo yamekuwa yakifanyika sana bila watu kujua kifungu cha 13-14 cha sheria hiyo ukisoma kinazungumzia hayo mambo na kuna watu ambao sheria hii tayari imewatafuna.

"Kwani sheria inasema hata kama ni wewe umerusha au umerushiwa sheria imeweka makatazo kwa sababu sheria imekuja na taratibu za wewe kuweka password (nywila) kwenye simu yako na kadhalika.

"Sheria haina excuses ya aina yoyote kwamba mimi sikuwa na taarifa au mtu mwingine nilimwachia simu yangu na hiyo simu yangu ndio ilionekana imerusha hivyo vitu, na hii inawagusa sana kinamama wamekuwa wakiaminiana kwenye haya masuala, lakini matokeo yake ni mabaya.

"Kudhibiti utoaji wa taarifa za uongo na hii ndio imekuwa vilevile sababu ya Serikali kuja na hii sheria moja kwa moja, kwa haraka. Ni kweli kwamba watu walipata taarifa za uongo, na taarifa za uongo zinatokana na nini? Yawezekana mtu anayezitoa sio professional, hajui kama anachotoa ni uongo au ni ukweli.

"Tukio kwa mfano limetokea mahali fulani ninyi waandishi wa habari mmefundishwa matukio haya kwa mfano ajali mtu anayetakiwa kusema ni msemaji wa Polisi wa eneo husika, lakini ilikuwa kwamba watu wakipata taarifa kama zile wanazirusha na kutoa taarifa ambazo haziaminiki na sio sahihi.

"Lakini matukio ya mauaji maeneo fulani fulani watu wengine walikuwa wakitoa taarifa na kuwataja hata watu wa matukio hayo yawezekana hata mtu aliyefanya hilo tukio sio yule unayemsema wewe na kesi ya mauaji ni kesi sensitive sana, lakini kama umesharusha kwenye mtandao mara moja watu wana tendecy ya kuamini taarifa ya awali.

"Halafu yule mtu anaweza kudhurika, kuna watu wanaamini watu wanaorusha kwenye mitandao ni waandishi wa habari na ndugu zangu waandishi wa habari wanaaminika ni kweli ukirusha content kama hiyo...ni kweli kabisa hii sheria inasaidia kudhibiti utoaji wa taarifa za uongo soma kifungu cha 14 na 16 vya sheria vinasaidia katika eneo hilo.

"Lakini vilevile sheria hii inasaidia kudhibiti jumbe zinazotumwa bila ridhaa ya mpokeaji siku hizi tunaona jumbe zinaingia...zingine zinaelekeza mambo fulani fulani...na wewe baadaye unazirusha.

"Sheria hii inasema kupokea ni jambo moja na kushea ni jambo jingine ukiipokea na kuishea unaingia kwenye hatia kama mtu aliyekutumia, meseji ambazo hazifai ni za kuangalia sana unaweza ukapuuzia, lakini tatizo linapokukumba ni kubwa na pia kudhibiti matusi ya kibaguzi,"amesema Wakili Maranga wakati akiainisha baadhi ya maeneo chanya katika sheria hiyo.

Mambo bado

Wakati huo huo, inabainishwa kuwa, uhuru wa vyombo vya habari unaozungumzwa sasa, bado haujawekewa misingi ya kisheria ili kuulinda.

Wakili James Marenga anasema, inadaiwa kuna sheria mbovu za habari ambazo hutumika tu pale mwandishi ama chombo cha habari kinapowindwa, hivyo jambo hili linaua tasnia ya habari nchini.

Amesema, kwa sasa vyombo vya habari nchini vinaandika na hata kukukosoa, lakini pale mwandishi ama chombo cha habari kinapowindwa, sheria zilizopo zinatumika.

“Kwa sasa vyombo vya habari vinaandika kwa uhuru, vinakosoa lakini kilichopo, kama mwandishi ama chombo cha habari kinawindwa, sheria hizi hizi zinatumika kuumiza chombo ama mwandishi.

“Mwandishi anaweza kufungwa kwa sheria zile zile ama chombo cha habari kinaweza kuondolewa sokoni kwa sheria hizo hizo, ndio maana tunasema uhuru wa habari lazima ulindwe kisheria,”amesema Wakili Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN).

Amesema, kuwepo kwa sheria hizi za habari, kwa kiwango kikubwa kumesababisha kushuka kwa habari za uchunguzi, na kwamba baadhi ya wanahabari wamepoteza vifaa vyao kutokana na polisi kuvitwaa kwa ajili ya upekuzi.

“Sheria hii imewapa mamlaka makubwa polisi, wanapoamua kukufuatilia na hata kuchukua vifaa vyako, wanaweza kufanya hivyo kwa sheria hii. Kwa nchi ya Ghana lazima polisi awe na kibali, lakini hapa kwetu hiyo haipo,” amesema.

Pia Wakili Marenga amesema, miongoni mwa mambo yanayokwaza tasnia ya habari ni pamoja na sheria kuelekeza usajili wa magazeti kila mwaka.

Amesema, kwa magazeti ingetosha kusajiliwa mara moja na sio kila mwaka kama inavyoelekezwa na sheria ya sasa.

“Unakuwa ni usumbufu na kupoteza pesa, yaani ukimaliza mwaka unaanza kukusanya documents (nakala) ambazo ulizipeleka awali unapeleka tena, tena unatakiwa kulipa. Hili jambo tunasema hapana, tunapaswa kusajili mara moja basi,”amesema.

Uimara

Angela Akilimali, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), amesema, uimara wa vyombo vya habari nchini utatokana na kuundwa kwa sheria rafiki na si zile zenye vitisho, kukandamiza na kunyanyapaa wanahabari.

Ameeleza kuwa, mchakato wa mabadiliko ya sheria za vyombo vya habari nchini, unalenga kujenga mazingira rafiki na bora kwa wanahabari katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Amesema, sheria zilizopo sasa zinakinzana na malengo ya ukuaji wa tasnia ya habari nchini hivyo kuwa chanzo cha kudumaza tasnia hiyo.

“Yapo mabadiliko mengi yaliyofanywa mwaka 2016 kwenye Sheria ya Habari yanayokinzana na kukua kwa tasnia hii, mfano huwezi kuunda Bodi ya Idhibati halafu serikali iisimamie bodi hiyo.

“Wanahabari kama taaluma nyingine, ina watu wenye weledi wa kutosha hivyo badala ya kuwa na vyombo vingi kama vilivyotajwa kwenye sheria hii (Bodi ya Idhibati, Mfuko wa Mafunzo na Baraza Huru la Vyombo vya Habari), tunaona tuwe na chombo kimoja tu ambacho ni Baraza Huru la Vyombo vya Habari ili kusimamia mambo yote ya wanahabari na tasnia kwa ujumla,”amesema Angela.

Amesema, kikwazo kingine kwenye tasnia ya habari ni sheria kulazimisha chombo cha habari hususani magazeti kuomba leseni kila mwaka na kwamba, jambo hilo limekuwa likisababisha usumbufu mkubwa.

“Hatuoni sababu kwa vyombo vya habari hususani magazeti kuwekewa utaratibu wa kukata leseni kila mwaka, kama ilivyokuwa awali kabla ya mabadiliko ya 2016 kwamba usajili ni mara moja, utaratibu huu unafaa kuendelea,” amesema Angela.

Amesema, tasnia ya habari inahitaji uwekezaji mkubwa na kwamba, kuweka mipaka ya uwekezaji kwa wageni kutoka nje kama inavyoelekeza sheria, kunaua tasnia hiyo.

“Kwenye hii sheria yapo mambo mengi magumu, lipo hili la kulazimisha mwekezaji kutoka nje awe na asilimia isiyozidi 49, lakini tunajiuliza mbona wawekezaji kwe nye mitandao ya simu wanawekeza kwa asilimia 100 tuna wao wana wateja zaidi ya milioni 10.

“Kwa nini kwenye tasnia ya habari wazuiwe, hii tunasema hapana. Tunasema hivyo kwa kuwa uwekezaji kwenye habari unahitaji mtaji hivyo kama ilivyo kwenye uwekezaji mwingine, kwenye habari akiwemo mwekezaji anayetaka kuwekeza kwa asilimia 100, aruhusiwe,”amesema.

Umoja

Wallace Maugo, Mhariri wa Gazeti la The Guardian amesema, wanahabari wanapaswa kuwa pamoja katika kuhakikisha sheria hizi zinazominya uhuru wa habari na wanahabari zinabadilishwa.

Amesema, mchakato wa mabadiliko haya umeanza wakati muafaka kwa kuwa, rais aliyepo madarakani (Rais Samia Suluhu Hassan) ni msikivu katika mambo mbalimbali.

“Tunapaswa kuwa pamoja wanahabari wote, lakini tuna bahati nzuri maana katika mchakato huu rais ni msikivu kabisa na anaonekana kuwa na dhamira ya kweli,” amesema Maugo.

Utayari

Wakati huo huo, Wakili James Marenga amesema, ni jambo la heri kwa Serikali iliyopo madarakani kuonesha utayari wa kupitia upya sheria za habari nchini.

Pia amesema, mabadiliko ya sheria huwa yanachukua muda mrefu, wakati wa sasa ni mzuri kwa kuwa, rais aliyepo madarakani Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameonesha dhamira hiyo.

“Mchakato wa marekebisho ya sheria iliyotungwa mwaka 2016, ulichukua miaka 10. Mchakato huo ulianza mwaka 2006, ni bahati utawala uliopo umeona kuna haja ya kupitia upya sheria hizi kama ambavyo wadau wamekuwa wakipiga kelele,”amesema Wakili Marenga.

“Tunaamini sheria hizi na zingine ambazo tumeorodhesha kwenye nakala yetu ya mapendekezo ya mabadiliko, wadau na serikali kwa pamoja tutapitia na kuona namna ya kunyoosha ili mapendekezo hayo yatapopelekwa bungeni, tuwe na msimamo unaofanana,”amesema.

Pia amesema kuwa, nia ya Serikali ni kuhakikisha mwafaka unapatikana katika Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Vyombo vya Habari na wadau wa habari wamekiri kuwepo kwa nia hiyo.

“Kwa hatua hii tunaona kuwa Serikali imeonesha nia katika kuhakikisha kuwa mabadiliko yua sheria ya habari yanafanyikiwa kazi na kupata mwafaka wa vipengele vya Sheria ya Habari vyenye ukakasi inaonekana wazi,” amesema Wakili Marenga.

Wadau wa habari wamekuwa wakilenga vifungu vinavyotisha waandishi na uhai wa tasnia ya habari nchini na kwamba, sio sheria yote ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 havifai.

“Kabla ya kuwapo kwa sheria hiyo, kulikuwa na sheria ya mwaka 1976 ambayo ilikuwa na changamoto kubwa sana ya udhibiti na uchapishaji.Sheria hiyo ilikuwa ikimpa mamlaka makubwa sana Waziri wa Habari kudhibiti uchapishaji wa magazeti,”amesema Marenga.

Amesema kwamba, mamlaka hayo kwa waziri, sheria mpya ilipotungwa (Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya 2016) ikayahamisha na kuyapeleka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambapo sasa anaweza kufunga magazeti, kunyima leseni wanahabari na hata kutoa hukumu kwa vyombo vya habari.

Dhamira njema

Naye Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Neville Meena akielezea kuhusiana na michakato mbalimbali inayoendelea ili maboresho ya sheria za habari nchini yaweze kutekelezeka kwa wakati anasema, awamu hii kuna dhamira njema.

“Awali Serikali haikuonesha dhamira ya kushughulikua maoni ya wadau wa habari nchini, lakini katika utawala huu wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan dhamira imeoneshwa tangu mwanzo, tunaamini tutafanikiwa,"anabainisha.

Meena amesema,Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016 iliacha mambo ya msingi katika kukuza tasnia ya habari na badala yake ikawa ni sheria ambazo ni ngumu kutekelezwa.

Amesema, kutokana na kuwepo kwa mazingira magumu ya habari na wanahabari nchini, tasnia ya habari iliyumba kwa kiwango kikubwa.

“Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016 ilipingwa na wadau wa habari siku moja baada ya kupitishwa ili kutumika. Si kwamba, hakukuwa na vitu muhimu kwa wanahabari, wadau waliona imebeba mitego na madhara mengi kwa wanahabari na vyombo vya habari,’’amesema Bw.Meena

Amesema kuwa, kuna lawama zinaelekezwa kwa vyombo vya habari kukosa weledi, moja ya changamoto inayovikabili ni kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati.

Madeni makubwa

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile amesema, miongoni mwa changamoto kubwa ambayo vyombo vya habari nchini inapitia licha ya sheria ambazo zipo katika hatua za maboresho ni pamoja na malimbikizo makubwa ya madeni ya vyombo vya habari.

Siku za karibuni,wamiliki wengi wa vyombo vya habari nchini yakiwemo magazeti waliamua kusitisha uzalishaji au kutoa huduma ya moja kwa moja kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha au malimbikizo ya madeni ambayo wanayadai kwa muda mrefu bila kulipwa.

Hatua ambayo ilichangia idadi kubwa ya wafanyakazi kupoteza ajira, kuacha madeni makubwa kwa waajiri wao ambayo hayajalipika hadi sasa, hivyo kuwafanya wadau hao wa habari kupoteza mwelekeo na wengine kukata tamaa ya maisha.

Balile amesema, licha ya juhudi kufanywa, bado taasisi za serikali zikiwemo halmashauri hazijalipa madeni yao kwa vyombo vya habari.

“Mpaka mwishoni mwa mwaka jana, madeni ambayo vyombo vya habari vinadai kwa serikali na taasisi zake ni shilingi bilioni saba.Ukijumuisha na deni la Gazeti la Daily News la Serikali (shilingi Bilioni 11), jumla ya deni ni shilingi bilioni 18 na zaidi.

“Halmashauri wana roho ngumu, hawajalipa mpaka leo licha ya kuandikiwa barua na TAMISEMI (Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambayo kwa sasa ipo chini ya Ofisi ya Rais). Tunaomba Mheshimiwa Waziri (Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mheshimiwa Nape Nnauye) liwekee mguu chini, utusaidie,”amesema Balile.

Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alisema Serikali itavilipa vyombo vya habari deni la zaidi ya shilingi bilioni sita baada ya kufanya uhakiki wa deni hilo ambalo ni moja ya mambo yaliyosababisha kufa kwa baadhi ya vyombo hivyo nchini.

Rais Samia alitoa ahadi hiyo Juni 28, 2021 jijini Dar es Salaam wakati akijibu swali la Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile aliyemuomba Mheshimiwa Rais kutimiza ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa ya kulipa deni hilo kabla ya Juni 30, 2021.

Alisema, Serikali itafanya uhakiki wa madeni hayo ya vyombo vya habari, kisha itaanza kulipa kidogo kidogo mpaka deni hilo liishe.

“Nitafanya kazi na Waziri Mkuu katika kuhakikisha kwamba tunalipa madeni haya kidogo kidogo, lakini lazima tuyafanyie uhakiki kisha tuweze kulipa, hatutaweza kulipa kwa mkupuo,”alisisitiza Mheshimiwa Rais.

Aidha, kuhusu katazo la Serikali kutangaza kwenye vyombo vya habari, Rais Samia alisema tangu ameingia ofisini, hajaona kama kulikuwa kuna katazo hilo hata hivyo katika utawala wake hakutakuwa na katazo hilo.

“Wakati wangu huu sitakataza matangazo kwenye vyombo binafsi, kwa hiyo ni jukumu letu kutafuta matangazo hayo,” alisema Rais Samia.

Meena anasema, vyombo vya habari vinashindwa kulipa mishahara kwa kuwa, watangazaji wengi hasa Serikali kwenye halmashauri,wanatoa matangazo lakini hawataki kulipa hivyo kuchangia kushuka kwa weledi kwenye vyombo vya habari.

“Vyombo vya habari vinalalamikiwa kukosa weledi, lakini tukumbuke kwamba wanaotoa matangazo na kushindwa kulipa, wanachangia kutengeneza tatizo.

“Wanaoongoza kutolipa ni wakurugenzi wa halmashauri, hili linachangia kuyumbisha vyombo vya habari na ndio maana tumependekeza baada ya miezi sita mtangazaji kushindwa kulipa, licha ya kukumbushwa basi afikishwe mahakamani,’’amesema.

“Suala la mapendekezo yote ya wadau wa habari kupita, hilo ni suala lingine. Cha msingi ni kwamba, miongoni mwa ahadi za Rais (Samia Suluhu Hassan), ikiwemo wizara kukutana na wadau wa habari na kupitia vifungu, imetekelezwa.

“Sisi kama wadau wa habari tunaamini tunakwenda kufanikiwa kwa kuwa, hata Waziri Nape (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) ana hisia chanya katika mchakato huo,’’amesema.

Tujiangazie pia

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile licha ya kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa kuonesha dhamira njema katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini, pia amewataka waandishi wa habari nchini kuandika matatizo yanayowahusu.

Balile aliyasema hayo Oktoba 20, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari yaliyoandaliwa na TEF yakiangazia uchechemuzi wa sheria za habari nchini ambayo yalifunguliwa na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania,Wiebe Jakob de Boer.

Balozi de Boer alibainishwa vyombo vya habari huru ndio msingi wa kuibua mijadala mizito na hutoa mwongozo katika utungaji wa sheria na mwelekeo chanya wa taifa.

Amesema, uhuru wa vyombo vya habari ndio moyo wa demokrasia ya nchi yoyote kwa kuwa, hutoa mwanga na mwelekeo wa taifa.

Balozi huyo amesema, mamlaka zikijenga tabia ya kusikiliza sauti za watu wote na kuchukua mawazo kwa kiwango kikubwa, itasaidia katika kufanya uamuzi wenye manufaa kwa wananchi na taifa.

‘‘Tunaamini kwamba, uwepo wa tabia ya kusikiliza sauti zote na kusikiliza mawazo ya kila mtu, inawezesha kufanya uamuzi wenye busara kwa manufaa ya taifa sambamba na kuinua maisha ya wananchi wote,’’ alisema Balozi Boer.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Deodatius Balile alimueleza Balozi Boer utayari wa serikali katika safari ya mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016.

Alisema, mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari unahusisha taasisi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jamii Forums.

Mbali na hayo Balile aliendelea kufafanua kuwa, "Waandishi wa Afrika katika mafunzo wanayopewa, wanapewa mafundisho kwenye vyuo na vyumba vya habari kwa ajili ya kutetea jamii, lakini katika mafundisho hayo hakuna ndani ya mtaala sehemu inayomwambia mwandishi wa habari na wewe ni sehemu ya jamii.

Maslahi muhimu

"Kwa hiyo, wakati mwingine wanakuwa wakijua kwamba wanafanya hiki kitu si kwa ajili ya kujitetea wao, maslahi yao, wanajua kwamba wao wanatetea jamii. Kwa hiyo hii imekuwa ni hivyo, muda wote na matatizo mengi yanakuwa kwenye vyumba vya habari, waandishi wa habari wanapata shida nyingi bila kujua na wao kumbe wanastahili kutetea haki zao.

"Ndio maana sisi kama Jukwaa la Wahariri Tanzania, tukasema huu mkondo tusipoanza kutetea haki zetu tutaendelea kuwa katika hali ngumu, mtaona kuna mashirika mengi hata yanayoteta hata zile haki za waandishi wa habari hayafanywi kazi za habari.

"Yaani unakuta shirika limeanzishwa huko mbali kabisa, halina hata ujuzi wa vyombo vya habari vinafanyaje kazi. Sisi ndio tunaovaa viatu, tunajua wapi kinabana zaidi, kwa hiyo kwa kujua matatizo yetu tukaanza kuyasemea, kuyatetea itaifanya Dunia itambue. Lakini pia tukiondoa ile kasumba hatuandiki habari zinazotuhusu.

"Kwa hiyo, umefika wakati sasa na sisi ni wanajamii na sisi tunahitaji kuishi na sisi tunahitaji kuishi na kuwa maisha bora ili tutetee haki zetu zipatikane tukiwa na hali nzuri tutasimama vyema kutetea haki za wengine kwa ufasaha.

...Vyombo vya habari vinafanya kazi ya kujenga uelewa katika jamii ili kuwafanya wananchi wafanye uamuzi kutokana na uelewa walionao.

"Watafanya uamuzi wakijua kwamba wanamtaka fulani si kwa sababu amewapa kanga au amewapa kofia ama kitenge wakati wa kampeni, lakini ameahidi kujenga miundombinu, kukuza mfumo wa elimu, kukuza uchumi. Jambo ambalo litasaidia si tu mtu mmoja mmoja bali kizazi na taifa kwa ujumla," amesema Balile.

Utashi wa kisiasa

Kwa upande wake mwenyekiti wa zamani wa TEF, Theophili Makunga amesema, suala la utashi wa kisiasa ni muhimu katika uandishi wa sheria kwa sababu linatoa mwelekeo wa sheria husika.

"Ikumbukwe kwamba tumetoka mbali kwenye sheria za waandishi wa habari, kwa muda mrefu nchi yetu ilikuwa inaongozwa na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, sheria ya magazeti ilikuwa na vipengele vingi sana vilivyokuwa vinambana mwandishi wa habari.

"Lakini kulingana na teknolojia iliyokuwepo wakati ule, baada ya Media Service Act, 2016 kufuta ile Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 vile vile kuna vipengele bado vinambana mwandishi wa habari.

"Lakini tunashukuru kwamba, Serikali imeliona hilo na imekubali kuongea na vyombo vya habari kurekebisha baadhi ya vipengele ambavyo tunafikiri vinawabana waandishi wa habari,"amesema Makunga.

Balile tena

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile anasema vyombo vya habari vinapaswa kujenga tabia ya kuanzisha mijadala yenye kuchochea ukuaji wa uchumi na sio mijadala isiyo na tija kwa nchi na wananchi wake.

Anasema, ni vema masuala ambayo yanahusu uboreshaji wa viwanda, miundombinu na kilimo ambayo yatabadilisha maisha ya Watanzania wote kutoka katika umasikini kupewa kipaumbele na nafasi zaidi kuliko zile za maisha binafsi ya watu na malumbano ambayo hayana tija.

“Kwa wenzetu katika nchi zinazoendelea wanajadili namna ya kukuza biashara na viwanda vyao kwa kuzalisha bidhaa bora pamoja na kutafuta masoko, sisi hapa tuna viwanda, uzalishaji wa gesi, lakini hauoni mijadala mingi kwenye eneo hilo, wanahabari tubadilike,”anasema Balile.

Pia amesema, wataendelea kuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya sheria zinazogusa tasnia ya habari kwa kushirikiana na wadau wengine nchini.

“Tunajipanga kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kutatua matatizo yetu na yanayotukabili jamii, hatuwezi kutaka marekebisho ya sheria pasi na kushirikiana na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” amesema.

Kuboresha maisha

Mhariri Mkuu wa Gazeti la Guardian,Walace Maugo ametumia nafasi hiyo kuwataka waandishi wa habari nchini kupigania haki za Watanzania na kuboresha maisha yao kupitia taaluma yao na kazi wanazozifanya kila siku.

“Kama tunavyofahamu kwamba sisi ndiyo tunaotengeneza mijadala kwenye jamii, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha maisha bora yanapatikana na watu wanafurahia maisha katika nchi yao, tusijione wanyonge kuna hatua kubwa zimechukuliwa kutokana na kazi tunazozifanya,” amesema Maugo.

Naye Neville Meena anasema, waandishi wa habari wana wigo mpana wa kufikisha taarifa zao na kuifanya jamii ichukue hatua au ishinikize hatua zichukuliwe kulingana na kile walichokisoma, kukisikia au kukiona.

Ameyasema hayo wakati akizungumzia umuhimu wa wanahabari kuchochea maendeleo, uzalishaji mali na mabadiliko ya sheria kwenye warsha ya kuwajengea uwezo wahariri kuandika na kupitia habari za uchechemuzi wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari.

“Leo hii mitandao ya kijamii na katuni zimekuwa zikitumika kufikisha ujumbe kwa jamii na kuleta mabadiliko makubwa, cha msingi ni lazima sheria ziweke misingi imara ya Watanzania kuwa na uhuru wa kujieleza, kupata habari na kusambaza,” amesema Meena.

Mhariri wa Gazeti la MwanaHalisi, Jabir Idrisa amesema, jamii inapaswa iendelee kupigia kelele kwa kushirikiana na vyombo vya habari juu ya marekebisho ya sheria zinazokwaza uhuru wa habari.

Kwa upande wake, Tumaini Mbibo amesema, watu wanaweza kudhani sheria ni mbaya, lakini kumbe hawazijui hivyo jambo la msingi ni kuwawezesha wazijue ili wasizivunje na kuingilia haki za watu wengine.

“Hatuwezi kudai mabadiliko ya sheria kama hatuzijui, tufanye uzengezi wa mabadiliko ya sheria tunazozilalamikia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili tupate matokeo chanya,”amesema Mbibo.

Pia amesema, ni muhimu kwa waandishi wa habari kujua kiini cha matatizo yanayolikabili Taifa na njia za kutumia ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo husika.

Amesema, haki za binadamu zinakwenda sambamba na demokrasia, hivyo uwepo wa sheria zinazominya tasnia ya habari zinakwamisha maendeleo huku akishauri ni vema ikafanyika mipango ya kufanya ushawishi wa mabadiliko.

Wakati huo huo, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim amesema kuwa, mwandishi wa habari akijua haki zake, sheria zinazoongoza tasnia ya habari ataweza kukutana na makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo wabunge na kuwashawishi juu ya sheria zinaminya uhuru wa habari na haki za binadamu.

“Bado waandishi hatujawa na uelewa mpana wa sheria zinazotuhusu, tufanye jitihada kuzijua. Tuwashawishi wenzetu juu ya sheria zinazokwaza ukuaji wa tasnia ya habari na maendeleo ya Taifa,” amesema.

Kwa upande wake, Sylvester Hanga amesema, waandishi wa habari wanataka sheria za masuala ya habari ziwe rafiki ili zichochee demokrasia, haki za binadamu na maendeleo kwa Taifa.

Joyce Shebe amesema, anaamini wahariri wakijua namna ya kushawishi watunga sheria, sera na mipango ya Taifa watakuwa kwenye nafasi njema ya kuchochea maendeleo ya mtu mmoja na Taifa.

Kuhusu bodi

Wakati huo huo, wadau wa habari wameeleza kwamba, uundwaji wa Bodi ya Ithibati ya Habari huru, utaweka mazingira ya usawa kati ya serikali na vyombo vya habari nchini.

ITAENDELEA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news