Rais Dkt.Samia aomboleza kifo cha Pele, atoa pole kwa Rais Bolsonaro

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kwa Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Brazil, Mheshimiwa Jair Messias Bolsonaro kufuatia msiba wa mfalme wa soka duniani, Edson Arantes do Nascimento (Pelé).

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa salamu hizo za pole leo Desemba 30, 2022 ikiwa ni siku moja baada ya kifo cha mwanasoka huyo kutokea wakati akiendelea na matibabu nchini humo.

"Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwanasoka wa Karne kutoka Brazil, Edson Arantes do Nascimento “Pelé”. Mchango wake katika soka Duniani utakumbukwa daima. Pole kwa Rais wa Brazil,Jair Messias Bolsonaro, familia na mashabiki wote wa soka. Mungu amuweke mahali pema peponi, Amina,"ameeleza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Desemba 29,2022 gwiji wa soka duniani, Edison Arantes do Nascimento (Pele) ambaye ni raia wa Brazil alifariki akiwa na umri wa miaka 82 katika Hospitali ya Israeli ya Albert Einstein huko São Paulo, Brazil.

Pele ndiye anayechukuliwa kuwa mchezaji bora zaidi wa soka ambaye ujuzi wake uwanjani ulisaidia kuutangaza kama mchezo mzuri, amefariki kufuatia mapambano ya mwaka mzima dhidi ya saratani ya utumbo.

Binti yake, Kely Nascimento alithibitisha kifo hicho kwenye Instagram yake,"Kila kitu tulichonacho ni kwa sababu yako. Tunakupenda sana. Pumzika kwa amani," Kely Nascimento aliandika.

Nyota huyo ambaye alizaliwa Oktoba 23, 1940 anahesabiwa na wengi wakiwemo wachambuzi mahiri wa soka duniani na mashabiki, kuwa mchezaji bora zaidi wa wakati wote.

Wakati wa uhai wake, kabla ya kustaafu soka, alicheza kama mshambuliaji wa kati. Aliisaidia Brazil kutwaa Kombe la Dunia 1958, 1962 na baadaye tena mwaka 1970.

Gwiji huyo aliweka rekodi mwaka 1958 ya kuwa mchezaji mdogo kuliko wote duniani kucheza katika fainali ya Kombe la Dunia alipocheza akiwa na umri wa miaka 17. Alivuma sana katika miaka ya 1970 duniani kote.

Mwaka 1999 alichaguliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuwa mchezaji bora wa karne. Kwa mujibu wa FIFA, Pele alikuwa mfungaji bora wa muda wote kwa kufunga magoli 1281 kati ya mechi 1363.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news