WAZIRI MKUU:ANZISHENI MAJUKWAA YA KIUCHUMI

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza viongozi na watumishi katika balozi waendelee kufanya tathmini ya fursa za kiuchumi ambazo Tanzania inaweza kupata kutokana na ushirikiano wa kidiplomasia kwenye nchi walizopo.
Amesema ni vema balozi hizo zikaanzisha majukwaa ya kiuchumi yatakayowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizo katika sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ardhi, madini, utalii, mawasiliano na biashara.

“Muwasihi wafanyabiashara na wawekezaji waje kuwekeza Tanzania na washirikiane na Watanzania kufungua makampuni, hii itatusaidia Watanzania kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuendesha biashara.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Desemba 30, 2022 wakati akizungumza na watumishi wa ubalozi wa Tanzania ulioko jijini Pretoria, Afrika Kusini.

Amesema watumishi wa balozi za Tanzania hawana budi kuandaa makubaliano baina ya Tanzania na nchi walizoko ambayo yataonesha nini kinatakiwa nchini humo na ambacho kinapatikana kwa wingi nyumbani Tanzania.

“Hapa kwenu, ubalozi unapaswa kutengeneza makubaliano maalum ya kibiashara miongoni mwa nchi hizi mbili na kubainisha aina ya bidhaa ambazo zinapatikana Tanzania kwa wingi na zinahitajika Afrika Kusini,” amesisitiza.

Aidha, Waziri Mkuu amesema ni vema pia ubalozi huo ukaendelea kuhamasisha watalii kutoka nchini humo kwa kubainisha vivituo vya utalii vilivyoko Tanzania ambavyo nchi hiyo haina huku akitolea mfano Mlima Kilimanjaro.

Awali, akitoa taarifa ya kiutendaji ya ubalozi huo, Kaimu Balozi Peter Shija alisema Tanzania inaweza kunufaika zaidi na fursa za biashara zilizopo nchini humo kwa kuuza mazao kama, mchele, maharage, korosho na mazao ya matunda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news