Ronaldo amchefua Kocha Santos katika Kombe la Dunia

NA DIRAMAKINI

KOCHA wa Ureno, Fernando Santos amesema, hakufurahishwa na tabia ya Cristiano Ronaldo baada ya fowadi huyo kujibu kwa hasira alipotolewa wakati wa mchezo wa mwisho wa kundi katika Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) nchini Qatar.

Kocha wa Ureno, Fernando Santos na Ruben Dias wakati wa mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Kituo Kikuu cha Habari kilichopo Doha, Qatar, tarehe 5 Desemba 2022. (Picha na Gareth Bumstead/Reuters).

Santos, ambaye alisema suala hilo sasa limefungwa, anaiandaa timu yake kumenyana na Uswisi katika hatua ya 16 bora leo Desemba 6, 2022. Timu hizo zitaumana baadaye leo katika dimba la Lusail Iconic (Lusail Stadium) lililopo Lusail mjini Doha, Qatar.

Awali Ronaldo alisema, alitukanwa na mchezaji wa Korea Kusini alipotolewa katika kipindi cha pili cha kichapo cha mabao 2-1 kwa timu hiyo ya Asia siku ya Ijumaa.

Lakini, vyombo vya habari vya Ureno vimeonesha picha zinazoonesha kuwa, Ronaldo alitumia lugha chafu kujibu uamuzi wa Santos.

Alipoulizwa jinsi alivyoitikia picha hizo, Santos aliuambia mkutano wa wanahabari Desemba 5,2022 mjini Doha nchini Qatar kuwa: "Sikupenda kabisa. Sikuipenda hata kidogo."

Lakini alisema suala hilo lilishapigiwa mstari. "Halafu mambo haya yanatatulika, na huwa yanatatuliwa ndani," alisema. "Yameisha. Ni mwisho wa hadithi kuhusu suala hilo na sasa tunafikiria juu ya mchezo wa kesho (leo) na kila mmoja amejikita katika maandalizi ya mechi."

Nafasi ya kuanza kwa Ronaldo kwenye timu bado ni gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa Ureno, lakini Santos alisema hakuwa makini na mjadala au kura za mtandaoni kuhusu suala hilo.

"Sisomi aina hii ya taarifa," alisema. "Sio ukosefu wa heshima, ni kwamba tuna siku tatu za kufanya mazoezi kwa ajili ya mchezo na siangalii habari za aina nyingine. Tunaangazia mechi ijayo."

Santos alisema alitarajia mchuano wa karibu dhidi ya Uswisi. Ureno iliishinda Uswisi mabao 4-0 katika Ligi ya Mataifa ya UEFA mwezi Juni kabla ya kufungwa 1-0 katika mechi ya marudiano.

"Haitakuwa mara ya kwanza dhidi ya Waswisi, tunajua itakuwa mechi ngumu," aliongeza. “Ni timu iliyojipanga vyema na ina wachezaji wa hali ya juu na wanajua uchezaji wao vizuri sana. Wamesawazishwa vyema na wanazingatia kila wakati na ndivyo tunatarajia katika mechi hii, tutakabiliana na upande wenye nidhamu katika soka."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news