Serikali inaendelea kuwajali watu wenye ulemavu nchini-Waziri Prof.Ndalichako

NA MWANDISHI WAF

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya watu wenye ulemavu nchini katika nyanja zote ikiwemo afya, elimu, uwezeshwaji wa kiuchumi, huduma za marekebisho, michezo na utamaduni pamoja na shughuli za kisiasa na uongozi.
Hayo ameyasema na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (Mb) kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Watu wenye Ulemavu Duniani ambapo Kitaifa yamefanyika jijini Arusha.

"Serikali imeendelea kuwajali walemavu kwa kujenga vituo vya afya, zahanati pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba na kinga ili kuwapa namna bora ya kuishi,"amesema Prof. Ndalichako.
Pia, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu kwa watoto wenye ulemavu kuanzia ngazi ya awali hadi Chuo Kikuu, ambapo kwa mwaka huu 2022 jumla ya watoto wenye ulemavu 2,883 wameandikishwa katika elimu ya awali wakiwemo wavulana 1,470 na wasichana 1,413.

Prof. Ndalichako ameendelea kubainisha kuwa, wanafunzi 1,157 wakiwemo wasichana 562 na wavulana 595.
Vilevile, kupitia mpango wa MEMKWA wanafunzi wenye ulemavu 122 wamesajiliwa ambapo wasichana ni 67 na wavulana 59.

Hivyo Prof. Ndalichako ametoa rai kwa watu wenye ulemavu pamoja na wadau wanaojishughulisha na masuala ya elimu wakiwemo watendaji wa Serikali kuhakikisha Watoto wote wenye Ulemavu wanaandikishwa ili kupata elimu itakayowasaidia wao na vizazi vyao.
Kwa upande wake Mtaalamu kutoka Wizara ya Afya Kitengo cha Tiba, Bw.Msafiri Kabulwa akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt.Tumaini Nagu amesema hapa nchini inakadiriwa kuwa asilimia 9.3 ya watu wenye umri kuanzia miaka saba na kuendelea wana aina fulani ya ulemavu ambao unaweza kuwazuia kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

"Katika taarifa hiyo mikoa iliyokuwa na kiwango kikubwa cha watu wenye ulemavu ilikuwa Mara asilimia 15.0, Tanga asilimia 14.6 na Ruvuma asilimia 13.5. Mkoa wa Manyara ulikuwa na idadi ndogo ya watu wenye ulemavu kwa asilimia 4.3,"amesema Bw.Kabulwa.

Aidha, amebainisha kuwa aina ya ulemavu ulioathiri watu wengi ilikuwa uoni kwa asilimia 1.9, ujongevu asilimia 1.2 na usikivu asilimia 1.0, Idadi hii inaweza kubadilika kutegemeana na taarifa iliyotolewa ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti, 2022.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lisilo la Kiserikali (Sightsavers), Bw.Godwin Kabalika amesema, shirika hilo linashirikiana kwa karibu na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wizara ya Afya kwa kuhakikisha wanatetea haki za watu wenye ulemavu.
"Kwa Tanzania tunafanya kazi ndani ya mikoa mitano ambayo ni Singida, Morogoro, Manyara, Ruvuma pamoja na Lindi kwa kushirikiana na Serikali katika eneo la vifaa, miundombinu, na utoaji wa elimu,"amesema Bw.Kabalika.
Pia, Bw. Kabalika amesema miongoni mwa kazi zao wanazofanya ni pamoja na kuwajengea uwezo waajiri pamoja na walemavu ili waweze kupata ajira katika soko la ajira na hata ujasiriamali.
Kilele hicho cha Maadhimisho ya watu wenye ulemavu hufanyika kila mwaka Desemba 3 ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ni "Suluhisho Mabadiliko kwaajili ya Maendeleo Jumuishi: Nafasi ya Ubunifu katika Kuchagiza Duniani Inayofikika na Yenye Usawa."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news