Serikali yasisitiza nguvu ya uzalendo kwa Taifa

NA MWANDISHI WETU

WASOMI na vijana wamekumbushwa umuhimu wa kuwa wazalendo, kujenga,kuiendeleza na kuilinda nchi na watu wake kwa ajili ya maslahi ya maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika sherehe ya Mahafali ya 40 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare kilichopo Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Katibu Mkuu Mteule Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Kaspar Mmuya amesema, mustakabali wa maendeleo ya Taifa lolote duniani unategemea mchango wa taasisi za mafunzo katika kuandaa wataalam wenye weledi ambao ndio chachu ya kuleta mageuzi ya kifikra na maendeleo jumuishi na endelevu kwa jamii.
"Wizara inatambua mchango mkubwa unaotolewa na chuo hiki katika kuandaa wataalam wa fani ya maendeleo ya jamii ambao ndiyo injini ya kutafuta suluhisho la changamoto za maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kiteknolojia, kiutamaduni, kisiasa na kimazingira kwa kutumia rasilimali zinazoizunguka jamii, hivyo mafunzo yanayotolewa hapa sharti yaakisi mipango ya nchi na vipaumbele vya jamii ili kuleta matokeo chanya ya maendeleo,"amesema Katibu Mkuu huyo.
Pia Bw.Mmuya amekipongeza chuo hicho kwa kuanzisha programu ya uanagenzi ambayo imesisitizwa katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 ambapo hadi kufikia sasa baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya uanagenzi wamepata ajira katika taasisi na makampuni mbalimbali nchini.
Aidha, Mmuya ametoa rai kwa chuo kuhakikisha kinafanya utafiti kwa lengo la kuishauri serikali kuhusu changamoto zinazohitaji mabadiliko ya kisera,kimkakati au kisheria.
"Kwa upande mwingine tafiti zinaweza kuwa na msaada mkubwa katika kubuni na kuboresha zana na mbinu shirikishi za kuhamasisha jamii kUshiriki katika kubuni, kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kutathimini shughuli au miradi ya maendeleo, hivyo jitahidini sana kutekeleza jukumu hilo kwa kiwango kikubwa,"ameeleza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news