Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo muhimu kwa viongozi wa umma

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewataka viongozi wa umma kukamilisha taratibu za uhaulishaji wa mali zao ili kurahisisha uwekaji wa kumbukumbu sahihi za taarifa na mali zao katika Daftari la Usajili wa Taarifa za Mali za Madeni za Viongozi wa Umma.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, maadhimisho hayo yameyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini Unguja leo.(Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Desemba 16, 2022 katika maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema, katika kutekeleza jukumu la msingi la uhakiki wa taarifa za mali za madeni ya viongozi wa umma kwa kipindi cha mwaka 2021,2022 jumla ya viongozi 224 wamehakikiwa taarifa zao za mali na madeni.
Pia Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, idadi hiyo ni sawa na asilimia 112 ya shabaha ya viongozi 200 waliopangwa kuhakikiwa.

Amebainisha kuwa, Serikali inafarijika kuona idadi ya viongozi wanaohakikiwa inaongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, licha ya Tume ya Maadili kutekeleza kazi hiyo bado kuna tatizo la kukosekana kwa nyaraka za umiliki wa mali zilizoorodheshwa kwenye fomu za tamko la mali na madeni.
Wakati huo huo, amesema katika kazi hiyo inayotekelezwa na Tume ya Maadili imebainika kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya viongozi wameorodhesha mali ambazo hawajakamilisha taratibu za uhaulishaji wa mali hizo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amezitaka taasisi zinazohusika na uhaulishaji kutekeleza majukumu yao ili kuepusha migogoro na kuondosha urasimu usio wa lazima katika kushughulikia suala hilo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa zawadi maalumu ya CD ya Utenzi na Nyimbo za kupiga vita Rushwa na Uhujumu wa Uchumi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar,Mhe.Haroun Ali Suleiman, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, yaliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini Unguja.

Amesema, katika kipindi cha mwaka 2021/2022 tayari tume imepokea Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Viongozi 2,496 ikiwa ni sawa na asilimia 99.8 ya shabaha iliyopangwa.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, kati ya fomu hizo, fomu zilizowasilishwa ndani ya muda ni 2,485 na zilizowasilishwa nje ya muda ni fomu 11.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Tuzo Maalumu ya kuthamini mchango wake katika Kupiga Vita Vitendo vya Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar na Waziri Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe.Haroun Ali Suleiman, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu zilizofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mazizini Unguja.

Amesema, kuchelewa kurejesha fomu kwa wakati bila sababu za msingi ni kosa la kimaadili, hivyo viongozi ambao sababu zao zilionekana kuwa si za msingi, tume iwasilishe kwenye mamlaka zao za uteuzi kwa hatua za kinidhamu.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, viongozi wanapaswa kuhakikisha wanazingatia matakwa hayo ya kisheria kwa kujaza fomu hizo kwa wakati na kuzirejesha kwa wakati ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.

Mbali na hayo,Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi ametunukiwa Tuzo Maalumu ya kuthamini mchango wake katika Kupiga Vita Vitendo vya Rushwa na Uhujumu wa Uchumi ZanzibarTuzo hiyo imetolewa na Waziri Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe.Haroun Ali Suleiman, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu zilizofanyika katika ukumbi huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news