Serikali yazindua Mpango wa Ufadhili wa Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi kwa Vijana kutoka Makundi Maalumu na Wanaoishi Katika Mazingira Magumu

NA MWANDISH WETU

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Lela Mohamed Mussa tarehe 14 Desemba 2022 amezindua Mpango wa Ufadhili wa Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi kwa Vijana kutoka Makundi Maalumu na Wanaoishi Katika Mazingira Magumu (Bursary Scheme for Vulnerable Groups) katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST).
Mpango huu wa Ufadhili unasimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) chini ya Programu ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi kwa ajili ya ajira zenye Tija (Education and Skills for Productive Jobs-ESPJ) unaoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. SDF inafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia na jumla ya vijana 600 watanufaika kutoka Zanzibar.
Mhe. Lela amesema, lengo la ufadhili wa mafunzo ya ujuzi unaotolewa ni kuwezesha vijana wa kitanzania wanaotoka katika makundi maalum na kaya maskini kupata ujuzi na stadi za kazi zitakazowawezesha aidha kuajiriwa au kujiajiri wao wenyewe hivyo kuchangia jitihada za Serikali za kuwawezesha wananchi wake wa makundi yote ki-uchumi na kijamii.

Aidha Mhe. Lela amesema anaona fahari kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa Mpango huo wa mafunzo ya ujuzi kwa ajili ya vijana 600 ambao watapata fursa ya kupatiwa mafunzo ya ujuzi katika fani za ushonaji, umeme wa majumbani, udereva, useremala, ufundi bomba, ujenzi, ufundi magari, uchomeleaji, ususi na urembo, upishi, kompyuta, utengenezaji majokofu na kilimo bustani.
Amesisitiza kwamba, mafunzo hayo yanaenda sanjali na programu ndogo ya Mafunzo ya Amali ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kama ilivyoanishwa kwenye Bajeti ya Wizara hiyo ya mwaka 2022/ 2023 ya kutoa elimu itakayowawezesha vijana kujiajiri ili kujikwamua na umasikini.
TEA imepewa jukumu la kusimamia na kutekeleza Mpango huu na Wizara mama ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kuwafikia vijana kutoka makundi maalumu na wanaoishi katika mazingira magumu walio katika kaya zilizosajiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuhakikisha wanafaidika na mpango huu kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujikwamua ki-uchumi.

Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Prof. Maurice Mbago ni mmoja kati ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi ambapo amesema, TEA ilipewa jukumu la kuratibu utekelezaji wa Mfuko wa SDF mwaka 2017 na awamu ya kwanza ya utekelezaji ilifanyika mwaka wa fedha wa 2017/2018 huku awamu ya pili ambayo inaendelea yenyewe ilizinduliwa rasmi mwaka 2020.
Prof. Mbago ameweka bayana kuwa, TEA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imekamilisha taarifa ya ufuatiliaji wa wanufaika (Tracer Study) kwa lengo la kupima matokeo ya mafunzo ya kuendeleza ujuzi kwa wanufaika waliopata nafasi kushiriki mafunzo hayo. 
 
Ufuatiliaji huo uliohusisha wanufaika 3,871 kati ya wanufaika zaidi ya elfu 35,000, umeonyesha kuwa asilimia 81 ya wanufaika hao wameajiriwa au wamejiajiri ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu walipopata mafunzo ya ujuzi.
Naye Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania Bi. Bahati Geuzye amefafanua kwamba, Mpango huu unatoa ufadhili wa mafunzo ya ujuzi katika sekta sita za kipaumbele ambazo ni: Kilimo na Kilimo - biashara, Utalii na huduma za Ukarimu, Uchukuzi, Ujenzi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Nishati. 

Mpaka sasa vijana wa kitanzania takribani 35,000 wamenufaika na mafunzo ya ujuzi tangu yalipoanza kutekelezwa mwaka 2018 ambapo kiasi cha Sh. Bil 13. 8 zimeishatumika ikiwa ni fedha zilizoelekezwa moja kwa moja kwa Taasisi 143 za Mafunzo ili kuwezesha mafunzo.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. 

TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unasaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa. Pia TEA inaratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news