SILAHA YA BWANA MICHAEL:Wakubwa kichwa kikaanza kuuma ghafla

NA ADELADIUS MAKWEGA

SIMULIZI juu ya matumizi ya kengele ni ndefu sana, angalau leo mwanakwetu akwambie, katika hesabu za miaka ikiaminika kuwa tangu karne ya nne hadi ya kwanza kabla na baada ya Kristo Kuzaliwa kuliibuka maendeleo makubwa ya utengenezaji wa silaha kwa kutumia madini ya shaba pia yalitumika kutengenezea kengele.

Wengine wanadai kuwa hata miaka mingi nyuma ya hiyo huko Karkasi, Uchina na Mashariki ya Mbali madini haya yalitengezewa kengele pia.

Matumizi ya kengele kama kiashiria cha jambo fulani yalianza kabla hata ya Ukristo. Ukristo ulipoanza kuenea kati ya karne 1-3 Baada ya Kristo mwenyewe hakukuwa na mjadala juu ya kutumia kengele kama kiashiria lakini Ukristo huo ulikuwa unapigwa vita kwa hiyo kutumia kengele ilikuwa ni kuhatarisha uhai wao.

Sasa hawa Wakristo wa kale walifanyaje ? Wakristo wa kale walikuwa wakitumia viongozi wao wadogo wadogo kuitana na mbinu ya kuitana kimya kimya kuelekea kusali.

Kumbuka wakati huo mtawala wa dunia ni Dola ya Rumi mwaka 313 Constatino Mkuu alitoa kibali na kuufanya Ukristo kutambulika na mkutano huo wa kulifanya hilo ulifanyika katika Mji wa Milano ambao upo hadi leo hii.

Constatino Mkuu akawambia wale Wakristo wa Kwanza jamani ee tumieni dude kama tarumbeta kujulishana muda wa ibada zenu.Wakristo wa Kwanza hawakupinga hilo kwa kuwa sasa wametambuliwa na hawaabudu kwa mficho tena.

Huyu mtawala muungwani aliyeutambua Ukristo akafariki dunia mwaka 337 hapo hapo na matumizi ya tarumbeta kuitana kusali yakaanza kupungua nguvu na matumizi ya vitu vya kugonga kama mbao, chuma na mabati kwa kutumia nyundo yakaanza kusambaa kujulishana wakati wa kusali. Matumizi hayo yakapitiliza hatua kadhaa hadi sasa kengele inatumika hata kutambusha hali ya huzuni(misiba na hatari), furaha na hata sherehe.

Kumbuka katika utamaduni wa Kiafrika kazi hiyo ya kengele ilifanywa vizuri mno kwa kutumia ngoma na midundo ya ngoma hizo ilimaanisha hali ya hatari, furaha au huzuni.

Tambua kuwa milio ya kengele katika ulimwengu wetu wa sasa katika baadhi ya vijiji inatumika kujulisha umma juu ya mikusanyiko ya dharura nako mashuleni kengele inafahamika na wengi kuwa inatumika kujulishana kuanza kwa vipindi na mikusanyiko mingine ya wanafunzi.

Mwanakwetu akiwa mdogo yeye na wadogo zake watatu waliwahi kuoma Shule ya Msingi Mnazi Mmoja: Mwanakwetu, Modestus, Michael na Samwel wakitoka nyumbani kwao Mbagala, mara zote mkubwa ndiye alikuwa anakabidhiwa fedha za nauli na matumizi shuleni. Mkubwa dawa lakini mwanakwetu kumbuka pia mkubwa anaweza kuwa sumu.

Siku moja kengele ya mapumziko ya saa nne shuleni ikakongwa ndugu wa mwanakwetu wanamfuata ndugu yao kupata mgao wa fedha zao ya matumizi kununua ice cream, mihogo, juice na fedha zao ya nauli.

Mwanakwetu alipewa shilingi 30 ya mgao huo; nauli kutoka Mbagala hadi Temeke mwanafunzi mmoja ni shilingi moja, kutoka Temeke mpaka Mnazi Mmoja shilingi moja. pesa ya ice cream pakiti ndogo ilikuwa shilingi, juice ya limau /ndimu yenye barafu bilauri moja ilikuwa shilingi tano, kipande cha muhogo shilingi moja. Kuinywa juice ilikuwa ngumu maana gharama ilikuwa kubwa kwao.

Kila mmoja alipata mgao wa fedha ya vipande viwili vya mihogo na ice cream moja jumla ilikuwa shilingi 12 na nauli ya kwenda na kurudi wanafunzi wanne ilikuwa shilingi 16 hao jumla kuu ikawa shilingi 28, huku nakisi ya 30 na 28 ni mbili.

Kila mmoja ana chake kiganjani Michael aliyekuwa miongoni wa wadogo aliulizia zile shilingi mbili zilizobaki na wakati huo anasoma hesabu za ankara mahesabu ya pesa yamemuingia.

Mwanakwetu kabla hajajibu Michael akaibuka na kilio, wakubwa kichwa kikaanza kuuma ghafla hapo wanaogopa maneno ya wanafunzi wengine kwa kuonekana na madhurumati wa pesa kwa nduguze.

Kilio kimeanza na kilio hicho kama zile kengele kinajulisha umma kuwa hapa pana dhuluma, hapa pana huzuni.

Wanafunzi waliokuwa wanawafahamu wakasogea, walipofika pale waliuliza kulikoni ? Bwana Michael tumempa pesa yake anataka tumpe yote, anaweza akapoteza nauli alafu akaja kutusumbua wakati wa kurudi nyumbani na sisi tunakaa mbali, tunaishi Mbagala.

“Bwana mdogo acha kulia, hiyo pesa ya dharura, utalala madarasani ! Ahh na nyinyi mnakaa mbali sana, aa amieni mjini mwanakwetu, mambo ya vidole viwili, si unaiona miba katika magorofa na sasa kuna picha mpya yaTarzani.”Haya yalikuwa maneno ya mwanafunzi Jonson Kwilasi aliyekuwa anasoma Modestus aliyefika kutatua mgogoro huo.

Hapo sasa mkubwa inabidi ule muhogo mmoja na ice cream moja ili kuweka pesa ya tahadhari, bwana mdogo akipoteza nauli ya UDA unampa na wakati huo zile shilingi mbili akapewa Bwana Michael na kilio kikakata muda huo huo, kesi ikaisha na wakasoma na kurudi nyumbani salama salimini, hakuna aliyepoteza pesa.

Mwanakwetu kwa utaratibu huo wa maisha mkubwa alikuwa anapata kidogo kwa kuwa mdogo alipata haki yake na alikuwa na silaha ya kudai zaidi. Silaha hiyo ndiyo kile kilio cha huzuni ambapo kilijaza watu na lawama juu.

Kilio cha huzuni sawa na kengele na pia sawa na zile ngoma katika utamaduni wa Mwafrika ilikuwa silaha kubwa na ndugu Michael na kilikuwa kinamzalia matunda ya kupata maradufu ya wenzake.

Katika ulimwengu wa sasa ni kweli mkubwa anaweza kupata kidogo na mdogo kupata zaidi kwa kutumia ile silaha Mheshimiwa Michael?.Mwanakwetu hana jawabu.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news