Sterling arejea Uingereza baada ya majambazi kuvamia nyumbani

NA DIRAMAKINI

MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Uingereza, Raheem Sterling amerejea nyumbani baada ya majambazi waliokuwa wamejihami kuvamia nyumba ya familia yake huko Oxshott, Surrey nchini Uingereza.
Sterling (pichani kulia) akiwa na mke wake Paige Milian (katikati) na watoto wake watatu. (Picha na Dailymail).

Sterling aliondoka nchini Qatar ambapo timu yake ya Taifa inashiriki michuano ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022 ili kusaidia familia yake baada ya tukio hilo.

Dakika chache kabla ya kuanza kwa mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Senegal, Desemba 4, 2022 ilitangazwa kuwa Sterling, mmoja wa wachezaji wa kutumainiwa wa Kocha Gareth Southgate, hatacheza.

Southgate alithibitisha tukio hilo, akisema: "Wakati mwingine soka sio jambo muhimu zaidi na familia inapaswa kutangulizwa mbele."

Alisema, hana uhakika iwapo atarejea kwenye michuano hiyo. “Kwa kweli sifahamu, ni hali ambayo anahitaji muda wa kukabiliana nayo, sitaki kumpa presha, tunataka kumpa nafasi hiyo na tutaona siku chache zijazo itakuaje."

Ripoti zilionesha kuwa, baada ya wizi wa kutumia silaha kwenye jumba la Sterling, timu za polisi zilifanya doria kuzunguka nyumba hiyo hadi Jumapili jioni.

Aidha, katika mtanage kati ya Uingereza na Senegal, walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-0. Ni kupitia mabao ya naodha Harry Kane ambaye alifunga bao lake la kwanza dakika ya tatu ya kipindi cha pili.

Ushindi huo ulipatikana Desemba 4, 2022 katika dimba la Al Bayt lililopo Doha, Qatar hivyo kutinga robo fainali ya michuano hiyo mikubwa duniani. Pia ushindi huo, ni hatua ya maandalizi kwa mechi dhidi ya Ufaransa katika robo fainali.

Kane alifunga kwa mara ya 52 kwa nchi yake kuingia ndani ya rekodi moja ya Wayne Rooney. Pia alimpita Gary Lineker kama mfungaji bora wa nchi yake katika mashindano makubwa akiwa na mabao 11.

Jordan Henderson ndiye alianza dakika ya 38 na Bukayo Saka akahitimisha tabasamu la Senegal dakika ya 57 katika dimba la Al Bayt huku Jude Bellingham akicheza nafasi muhimu kufanikisha ushindi huo.

Uingereza, ambayo ilitinga nusu fainali katika Kombe la Dunia lililopita nchini Urusi mwaka 2018, itamenyana na mabingwa watetezi Ufaransa kwenye Uwanja wa Al Bayt siku ya Jumamosi hii.

Wakati wanandoa na watoto wa wachezaji wengi wakiwa Qatar kutokana na mchuano huo, mke wa Sterling Paige Milian alikuwa nyumbani wakati wa wizi huo siku ya Jumamosi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news