TWASHEREHEKEA UHURU-4:Naye Jakaya Mrisho Kikwete,Kwingi kwingi hufikii, bila usafiri wetu

NA LWAGA MWAMBANDE

KWA uchache,Rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2013 alichaguliwa kuwa Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi katika Maendeleo Barani Afrika.

Dkt.Kikwete ambaye ni mwanasiasa mahiri na mwanadiplomasia mbobezi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 alipohitimisha muhula wake.

Heshima hiyo kwa Rais Dkt.Kikwete ilitolewa na jarida maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine Group na tuzo ya heshima ikatolewa kwake Aprili 9, 2014, katika sherehe iliyofanyika jijini Washington, D.C nchini Marekani.

Tuzo hiyo kubwa ya heshima hutolewa kwa viongozi wa Afrika ambao hutoa mchango mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii kila mwaka kwa watu wao na ilitolewa kwa Rais Dkt.Kikwete kwa mwelekeo wake usiokuwa wa kawaida na wenye mafanikio makubwa kwa masuala ya utawala bora.

“Kuhusu maoni ya wasomaji wetu juu ya kiongozi yupi wa Afrika ambaye ni hodari zaidi kwa maendeleo ya kiuchumi na maendeleo, matokeo ya majibu ya swali hilo yamedhihirisha bila shaka yoyote kuhusu nafasi ya Rais Kikwete katika uongozi wa nchi yake. Na ushahidi uko kila mahali,ameweza kusimamia uchumi ambao umekuwa kwa wastani wa asilimia saba kwa miaka yote ya uongozi wake.” Jarida hilo lilibainisha.

Kuna mengi ambayo, Dkt.Kikwete aliyafanya ndani ya uongozi wake, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa,Mwenyenzi Mungu, amemkirimia Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete karama ya kipekee katika uongozi, hivyo tunaposherehekea miaka 61 ya Uhuru wetu leo, tuna mengi ya kujivunia kupitia uongozi wake, endelea;

1:Japo ni rais wetu, pia ni rafiki yetu,
Kwa kweli huyu mwenzetu, jinsi anakuja kwetu,
Japo itifaki zetu, zafanya asiwe wetu,
Twashereheka Uhuru, naye Jakaya Kikwete.

2:Huyu Rais wa Nne, Tanzania nchi yetu,
Wala si kama wengine, ana cha pekee kitu,
Acha Baraka avune, toka miongoni mwetu,
Twashereheka Uhuru, naye Jakaya Kikwete.

3:Kama Mkapa lianza, kwa miundombinu yetu,
Kikwete lifululiza, kwa maendeleo yetu,
Kujenga aliongeza, yote kwa faida yetu,
Twashereheka Uhuru, naye Jakaya Kikwete.

4:Acha nitaje vichache, vile alifanya kwetu,
Nisivyotaja viache, pia hivyo ni vya kwetu,
Kumuenzi tusiache, huyu kiongozi wetu,
Twashereheka Uhuru, naye Jakaya Kikwete.

5:Chuo Kikuu Dodoma, hilo jambo kubwa kwetu,
Kajenga kimesimama, wapo wanafunzi wetu,
Kikubwa acha kusema, kwenye hili bara letu,
Twashereheka Uhuru, naye Jakaya Kikwete.

6:Unataka kutalii, kwa Dodoma Jiji letu,
UDOM utatalii, huo utajiri wetu,
Kwingi kwingi hufikii, bila usafiri wetu,
Twashereheka Uhuru, naye Jakaya Kikwete.

7:Chuo kilivyojengeka, kweli ni fahari yetu,
Hata kozi kusomeka, vema sana kwa wenzetu,
Hosteli watosheka, nyingine hazina watu,
Twashereheka Uhuru, naye Jakaya Kikwete.

8:Hospitali ya moyo, nalo jambo kubwa kwetu,
Jinsi magonjwa ya moyo, yanavyotowesha watu,
Wala haina uchoyo, yapokea wote watu,
Twashereheka Uhuru, naye Jakaya Kikwete.

9:Gharama za tiba hapa, zimekaa zetu zetu,
Bila ya kuwepo hapa, tungepoteza wenzetu,
Wale waweza kulipa, wangeenda kwa wenzetu,
Twashereheka Uhuru, naye Jakaya Kikwete.

10:Sawa na waliopita, umoja ni tunu yetu,
Kulinda hakujivuta, huyu kiongozi wetu,
Hata watu walipata, kufanya yao kiutu,
Twashereheka Uhuru, naye Jakaya Kikwete.

11:Kwa sasa yuko Msoga, huyu kiongozi wetu,
Twasikia zake swaga, kikutana na wenzetu,
Ombi azidi kunoga, maisha yakiwa kwatu,
Twashereheka Uhuru, naye Jakaya Kikwete.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news