UENDESHE KWA HADHARI:Dereva wewe sikia, mbiombio ni hatari

NA LWAGA MWAMBANDE

DESEMBA 28, 2022 watu 57 wamenusurika kifo katika ajali iliyotokea Barabara Kuu ya Morogoro-Dar es-Salaam baada ya basi la abiria la Kampuni ya Al-Seady lililokuwa linatoka Kilosa kuelekea jijini Dar es Salaam kupinduka eneo la Kitungwa katika Manispaa ya Morogoro.

Ajali hii imetokea ikiwa imepita siku chache tangu kutokea ajali ya IT na lori la mafuta eneo la Iyovi huko Mikumi katika Barabara ya Morogoro-Iringa na kuua watu watano wakiwemo wanandoa wawili.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslimu alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi la Ally's Star lililokua linatokea Dar es salaam kuelekea Mwanza kutaka kuyapita magari yaliyopo mbele yake bila kuchukua tahadhari.

Ndipo dereva wa gari la Al Saedy alimkwepa kuepusha gari kugongana uso kwa uso, ndipo likapinduka, hata hivyo dereva aliyesababisha ajali hiyo anashikiliwa na jeshi la polisi.

Mshairi wa kisasa, Lwanga Mwmabande anasema kuwa, dereva bora anapaswa kujua kuendesha gari vizuri, kuzifahamu na kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuzifahamu alama zote za barabarani na maana yake.

Pia dereva bora anapaswa kuzijua ishara zote zinazotumika barabarani, michoro yote ya barabarani, kanuni za usalama barabarani na kuhakikisha anazitii na kuzifuata bila shuruti ili safari yake na aliowabeba iwe salama. Endelea;

1:Bora chagua kuishi, kuliko kupita gari,
Kuovateki uzushi, na kwa maisha hatari,
Safarini haukeshi, waweza fika vizuri,
Wewe dereva wa gari, uendeshe kwa hadhari.

2:Fikiria mwendo wako, kwa miguu si mzuri,
Tapoteza muda wako, ukiwa kwenye safari,
Lakini na gari lako, mambo huwa ni mazuri,
Wewe dereva wa gari, uendeshe kwa hadhari.

3:Hivyo vema chukulia, gari njia yako nzuri,
Mahali kupafikia, wala huwezi subiri,
Endesha ukitumia, mwendo ulio mzuri,
Wewe dereva wa gari, uendeshe kwa hadhari.

4:Alama barabarani, zatuepusha hatari,
Ni bora kuwa makini, usikimbie subiri,
Tayari uko njiani, tafika kwako vizuri,
Wewe dereva wa gari, uendeshe kwa hadhari.

5:Umeshika usukani, jiangalie vizuri,
Bila ulevi mwilini, kwani huo ni hatari,
Mbele tashindwa uoni, kwako iwe ni hatari,
Wewe dereva wa gari, uendeshe kwa hadhari.

6:Kingine kukielewa, tena elewa vizuri,
Barabara yatumiwa, na watu wengi wazuri,
Ambao wategemewa, huko mbele ya safari,
Wewe dereva wa gari, uendeshe kwa hadhari.

7:Kama wewe hujipendi, hiyo ni mbaya habari,
Na wengine hawapendi, uwaletee hatari,
Tumia wa kwako ufundi, kiendesha kwa hadhari,
Wewe dereva wa gari, uendeshe kwa hadhari.

8:Dereva wewe sikia, mbiombio ni hatari,
Vifo tunavisikia, vyaondoa utajiri,
Tunabaki tunalia, kwa kutoepuka shari,
Wewe dereva wa gari, uendeshe kwa hadhari.

9:Pole kwa wafiwa wote, kwa hizi nyingi hatari,
Pia majeruhi wote, mpone muwe vizuri,
Iingie kwetu sote, ovateki ni hatari,
Wewe dereva wa gari, uendeshe kwa hadhari.

10:Yalofika yawe basi, mengine tusisubiri,
Zatosha habari hasi, chanya ndizo twasubiri,
Maisha ni yetu sisi, tuziepuke hatari,
Wewe dereva wa gari, uendeshe kwa hadhari.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news