USIAMINI KILA UAMBIWALO

NA ADELADIUS MAKWEGA

KUNA wakati Baba wa mwanakwetu alihamishwa kutoka Shule ya Msingi Kimanzichana kwenda Shule ya Msingi Mkuranga zote zikiwa shule zilizokuwepo wakati huo katika Wilaya ya Kisarawe (Mkuranga) ndani ya Mkoa wa Pwani.

Mara baada ya mwalimu huyu kupewa barua ya uhamisho serikali ya Wilaya ya Kisarawe ilimpa haki zake na familia yake na kupewa lori la kubeba mizigo na familia hii kusafirishwa umbali unaokaribia kilomita 50.

Siku hiyo kabla ya safari vyombo hivyo vilipakiwa katika lori la serikali muda wa jioni na hadi saa moja ya usiku vyombo vilikuwa vimejaa na safari kuanza kuelekea Kijiji cha Mkuranga.

Kwa aina ya usafiri wa wakati huo hiyo ilikuwa safari ndefu japokuwa sasa si safari ndefu tena kutokana na ubora wa barabara na ubora wa vyombo vya usafiri.

Mama na wadogo wa mwanakwetu walikaa mbele kwa dereva wa lori hilo huku mwanakwetu ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu, baba yake mwanakwetu na mtumishi mmoja wa Wilaya ya Kisarawe walikaa nyuma ya lori hilo pamoja na vyombo.

Wakati huo Mbunge wa Kisarawe ni Profesa Kighoma Malima na walipofika Mkuranga baba wa mwanakwetu alipewa nyumba ya shule jirani na barabara ya Mkuranga-Kisiju nyumba hii hadi leo bado ipo ikiwa katika ubora ule ule miaka inayokaribia 50 sasa, mbele ya nyumba hii nyeupe mizigo ilishushwa na kuingizwa ndani na maisha katika Kijiji cha Mkuranga kuanza.

Baba wa mwanakwetu alikuwa mwenyeji wa ukanda huo kwani shule ya msingi alisoma Kilindoni Mafia kwa hiyo Mkuranga hakukuwa eneo geni sana akilini mwake.

Kijiji hicho kilikuwa na mwenyekiti wake aliyefahamika kama Shekhe Iddi Ally, mzee mmoja muungwana aliyependa maendeleo na mpenzi wa kuvalia misuli meupe, fulana nyeupe na kofia nyeupe, huku watoto wake akiwamo Habiba Idd Binti Ally akisoma na mwanakwetu .

Kijiji hiki kilikuwa na wenyeji wandengereko wengi, wazaramo kadhaa, wamatumbi kiasi na wamakonde chale na wamakonde maraba.

Hawa wamakonde maraba ni wamakonde shikamoo–marahaba, hawa walikuwa wakitazamwa kama wamakonde waswahili- wamakonde shikamoo marahaba, kwa lugha ya mazungumzo unaposema wamakonde+shikamoo+marahaba ni maneno mengi waswahili wakafupisha wamakonde maraba, ndiyo kusema neno shikamoo likadondoshwa chini na silabi ha.

Hawa Wamakonde wa aina mbili walikuwa wakitofautishwa na makabila mengine kwa mambo kadhaa.

Kwanza ni ule muonekana wao wa nje wa chale iliyokuwa michoro na kupendezesha sura zao na ndonya.

Michoro hiyo na ndonya katika sura zao ilikuwa nakshi nzuri sana ambayo ni mwanakwetu alivutiwa nayo mno kama ilivyokuwa alama II kwa wandengereko kwenye upande wa sura na sumuni katika paji la uso la Wagogo.

Kwa wale wamakonde maraba hawakuwa na utambulisho wowote katika sura zao wakifanana na kama waswahili wengine kama wazaramo, wandengereko na wamatumbi.Tofauti ya wazi ilikuwa wamakonde maraba wengi wao walikuwa ni Waisilamu huku wamakonde chale wengi wao walikuwa Wakristo hasahasa Wakatoliki wakitoka nao huko huko Msumbiji.

Kama ilivyokuwa ikifahamika na wengi hawa wamakonde walikuwa wakienda kufanya kazi katika mashamba ya mikonge kama manamba wengine walienda huko na kubakia huko na wengine kurudi na kuishia njiani na kuweka makazi yao maeneo mbalimbali huko Tanga, Pwani Dar es Salaam, Lindi hadi Mtwara. Mwanakwetu anamkumbuka mzee Mateo Nandumba ambaye alikuwa pia katekista mstaafu alikuwa akiishi Mkuranga mbele ya eneo la Magogo Matatu unapoelekea Dundani huku alikuwa akifunga safari hadi Msumbiji kusalimia nduguze.

Kumbuka mwanakwetu yupo Mkuraga darasa la tatu aliwakumbuka rafiki zake wawili aliosoma nao darasa la kwanza na pili Shule ye Msingi Kimanzichana Mohammed Kindundusi na Tatu Ally na Mgeni hakosi rafiki hapo mwanakwetu pia alipata rafiki mgeni binti wa Kimakonde aliyefahamika kama Veronika Mchiwawo ambaye alimwambia mwanakwetu namna ya kuishi hapo na akimtajia jina la Hamisi Issa kuwa ni mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa darasani.

“Nyumbani kwa akina Hamisi Issa katika kila mwaka wanapokuwa na mwanafunzi wa darasa la saba wanafaulu wao tu tangu shangazi zake, mama zake wadogo na dada zake kwao ni nyumba ya wasomi.”

Jambo hilo lilimtisha sana mwanakwetu, kuna siku ulifanyika mtihani wa Somo la Hisabati karatasi hizo zilikusanywa, mwanakwetu aliporudi nyumbani kwao nyumba ya mwalimu iliyokuwa na vitabu vingi alikitafuta kitabu kimoja kilichokuwa na majibu ya somo la hisabaiti darasa la tatu, Kiongozi cha Mwalimu.

Wakati huo katika shule za msingi kulikuwepo na aina tatu za vitabu kwanza Kitabu cha Kiada ambacho hicho kilitumika kufundishia wanafunzi wote nchi nzima.

Hivi ni kama vile vitabu vya Juma na Roza na Mr& Mrs Daudi, alafu kulikuwa na aina ya pili ya Kitabu cha Ziada hivi vilikuwa havifanani shule zote bali vilitumika kuwaongezea ujuzi wa mada husika wanafunzi na hata mwalimu.

Aina ya tatu kilikuwa ni Kitabu cha Kiongozi cha Mwalimu kilikuwa kitabu chenye majibu kutoka kitabu cha kiada na kinamuongoza mwalimu.

Mwanakwetu alipotazama katika Kiongozi cha Mwalimu alibaini kuwa katika maswali 20 aliyopewa darasani alipata maswali 16 na kukosa maswali manne na hata mwalimu aliposahihisha karatasi hizo majibu yalikuwa hayo hayo huku Hamisi Issa akipata maswali 15.

Hamisi Issa sasa ni mjuzi wa masuala ya mahesabu ya kifedha nchini Tanzania kutoka ile familia ya wasomi pale Mkuranga naye mwanakwetu ndiye anayekusimulia simulizi hii.

Ni kweli maneno ya Veronika Mchiwawo yalimtisha mwanakwetu mno wakati ule yamekuja kweli, lakini katika maisha jambo la msingi siyo kutishika na yale unayoambiwa au kushauriwa yapokee na kuyafanyia kazi kwa kuyapima vizuri sana moja baada ya lingine, unaweza kuambiwa kuwa kijiji hiki kina wachawi hauwezi kuishi kumbe pengine ungeweza kuishi na kupata mke hapo hapo,usiamini tu kila uambiwalo.

makwadeldaius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news