SIMANYILE AYU MDALA

NA ADELADIUS MAKWEGA

DESEMBA 13, 2022 mwanakwetu alipita kwa majirani zake watatu ambao ni wafugaji kupeleka malipo ya pesa zao za mbolea ambazo mwanakwetu alichukua kwa ajili ya bustani yake.

Kwanza kwa Muhawa Manoza mwanakwetu alichukua mbolea ya shilingi 5000. Pili kwa Mdala Asha mke wa Adam mtoto wa Mdala Anna mwanakwetu alichukua mbolea ya shilingi 10,000.

Mwisho kwa Mdala Anna mwanakwetu alichukua mbolea ya shilingi 10,000.Jumla kuu mwanakwetu alilipa shilingi 25,000.

Hapa kwa Mdala Anna anashamba kubwa jirani ya nyumba yake ambapo kwa miaka mitatu mfululizo mwanakwetu ameshuhudia kwa macho yake mama huyu analima mahindi na kuvuna magunia kadhaa, huku chakula hicho kikimfaa yeye na wajukuu zake wengi.

Kwa miaka yote anayolima yaani 2019, 2020 na 2021 ambayo mwanakwetu ameshuhudia kwa macho yake bibi huyu aliitumia vizuri samadi kutoka katika zizi lake.

Mwanakwetu kwa kuwa anaelewana na Mdala Anna alimuuliza bibi huyu mbona hajapanda hadi muda huu? Mdala Anna alijibu kuwa hali ya hewa ya mwaka huu bado hajaielewa kabisa. Kidogo hali ya hewa ya miaka ya nyuma ilieleweka.

“Miaka ya nyuma mara nyingi wakati tunapokwenda kanisani pale tu tunapoanza kuimba-Tazama bikira amechukua mimba na yeye atamzaa mwana, hapa nyumbani kwetu tunakuwa tumetoka kupanda mahindi na pale inapofika wakati tunaimba-Mtoto amezaliwa kwa ajili yetu na tumepewa mtoto mwanaume, hapo mahindi yameshakuwa makubwa na yana majani manne hadi sita na palizi ya kwanza tunafanya lakini hali hii ya sasa haieleweki.”

Mwanakwetu alipomuuliza mdala huyu kama amenunua mbegu bora za kupanda majibu yake alisema hajafanya hivyo kwani ilitolewa ahadi ya wao kupatiwa mbegu za bure na kama mbegu hizo zisipotolewa basi ameshajiandaa kupanda mbegu za asili.

Mdala Anna ni miongoni mwa wakulima wengi nchini Tanzania wanaotegemea kilimo chao kwa neema ya mvua za mwaka huku matumzi ya mbegu za asili likiwa ndiyo tegemeo lao.

Kwa hakika Mdala Anna atapanda mbegu zake asili maana ahmadi kibindoni! Kwa maana ni ngumu kutegemea majaliwa yaliyo mbali na wewe. Je mkulima kama huyu anatarajia kuvuna mahindi ya kutosha? Mwanakweu hayo ni majaliwa.

Matumaini hayo ya kuvuna mahindi mwakani hayapo kabisa kwa Mdala Anna akipata picha ya upungufu wa chakula akisema,

“Msukuma akalonga siilavya chukulya cha bwete, simanyile ayu mdala-Msukuma alisema hatoi chakula cha bure sifahamu huyu mama.”

Hata kama kitatolewa chakula cha bure je tutaweza kuwapa wote? Sasa ni wakati sahihi wa kusambaza mbegu bora muda mfupi kwa wakulima wetu kwa ile mikoa ambayo mvua hazijaanza kunyesha.

makwadeladius @gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news