Waliomzika mtoto akiwa hai kama kafara wapandishwa kizimbani

NA DIRAMAKINI

ZAWADI Msagaja mwenye umri wa miaka 20 mkazi wa Kijiji cha Mahaha wilayani Magu Mkoa wa Mwanza na wenzake wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa kike kwa kumzika akiwa hai ili wapate mali.

Wengine waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza na kusomewa shitaka la mauaji ya mtoto huyo Desemba 27, 2022 ni dada yake Zawadi aitwaye Elizabeth Kaswa na mumewe, Mussa Mazuri ambaye ni mganga wa kienyeji.

Akiwasomea shitaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Fortunatus Kubaja, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mwanahawa Changale aliieleza Mahakama kuwa, washtakiwa hao walitenda kosa hilo Novemba 13, mwaka huu.

Aliendelea kusema, washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji namba 7/2022 walitenda kosa hilo katika Mtaa wa Kisundi Kata ya Bugogwa wilayani Ilemela mkoani humo kwa kumzika mtoto huyo akiwa hai ili wapate mali kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu marejeo namba 16 ya mwaka 2022.

"Washtakiwa wote mchana wa siku hiyo mlishirikiana kumpatia mtoto wa Zawadi dawa za kienyeji akalewa kisha mkamfukia akiwa hai na kumsababishia kifo kwa malengo ya kujipatia mali kinyume na sheria," alieleza Changale.

Hata hivyo, washtakiwa baada ya kusomewa shitaka hilo hawakutakiwa kujibu chochołe kwani mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo.

Aidha, baada ya washtakiwa kusomewa shitaka linalowakabili, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kubaja aliahirisha kesi hiyo hadi Jumatano itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa.

”Washtakiwa hamtakiwi kujibu chochote kwa sababu Mahakama hii haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi yenu. Wote mtaendelea kukaa rumande, kwani shitaka linalowakabili halina dhamana,”alisema Kubaja

Novemba 29, mwaka huu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kupitia kwa Kamanda wa Polisi Mkoa, SACP Wilbroad Mutafungwa alitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya kukamatwa kwa washtakiwa hao kwa makosa ya kula njama na kumzika mtoto wa Zawadi Msagaja (jina linahifadhiwa) kama kafara ili wajipatie utajiri jambo ambalo ni kinyume na sheria na kukiuka haki za binadamu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news