Waziri Mkuu:Tutunze rasilimali za misitu

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania watunze rasilimali za misitu kwa kuwa zinafaida kubwa kwa Dunia, Taifa na mwananchi mmoja mmoja.

Amesema kuwa katika vipindi tofauti Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza juu ya umuhimu wa kuhifadhi misitu nchini, hivyo kila mmoja ahakikishe anazingatia suala hilo.
Ameyasema hayo leo Desemba 12, 2022 alipozungumza na wananchi wa Kijiji cha Kagunga Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi baada ya kukabidhi hundi mbili zenye thamani ya shilingi bilioni 4.27. Fedha hizo zilizotolewa na taasisi ya CARBON TANZANIA kwa wananchi wa vijiji vinane na Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika zimetokana na mauzo ya hewa ya ukaa awamu ya sita.

“Fedha hizi mmezipata kutokana na tabia yenu nzuri ya utunzaji wa misitu, endeleeni kuitunza misitu hii ili tupate mvua za kutosha. Pia, tumieni mvua hizi zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao mbalimbali.”

Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini waendelee kuweka mikakati ya kuwaelimisha wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira. “Kila mtumishi wa umma kwenye eneo lake ahakikishe moja ya agenda iwe uhifadhi wa mazingira.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka halmashauri zote zenye miradi ya hewa ukaa zifuatilie mikataba inayosainiwa baina ya makampuni na vijiji kwa ajili ya mauzo ya hewa hiyo. “Mikataba hii ni lazima tuijue, wanasheria wetu lazima muifuatilie.”

Waziri Mkuu amewataka wana-Vijiji watumie fedha wanazozipata kutokana na mauzo ya hewa ya ukaa kwa maslahi ya wananchi wote. “Wakurugenzi fuatilieni kama mipango ya wanavijiji ina maslahi kwa wananchi wote, jengeni miundombinu ya umma, posho isichukue nafasi kubwa.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news