Yaliyojiri Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani 2022

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameagiza kuwepo juhudi za pamoja, ushirikiano na mikakati madhubuti ili kutekeleza mpango wa kutokomeza maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU), unyanyapaa na UKIMWI.
Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo hayo Desemba Mosi,2022 mjini Lindi alipozungumza na wananchi kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo kitaifa kwa mwaka huu wa 2022 yalifanyika mkoani Lindi.
Rais Dkt.Samia alisema, ili kufanikiwa kufikia lengo la mpango mkakati wa miaka mitano wa kudhibiti maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI, unyanyapaa na UKIMWI kunahitajika juhudi za pamoja na ushirikiano. 

Huku akibainisha kwamba mafanikio yaliyopatikana yatakuwa endelevu iwapo kutakuwa na ushirikiano baina ya serikali, wahisani, wadau, asasi mbalimbali na wananchi.
Alisema, ili kufikia lengo ni lazima kuwepo mikakati madhubuti ya kuzuia maambukizi mapya. Hasa kwa kundi la vijana ikizingatiwa kwamba kundi hilo ambalo ni nguvu kazi muhimu ya uchumi na maendeleo ya taifa linakabiliwa na hatari ya kupata maambukizi mapya.

Alisema, licha ya mafanikio yaliyopatikana katika maeneo hayo matatu ambayo ni kupungua kiwango cha maambukizi, UKIMWI na unyanyapaa itakuwa Kazi ngumu kufikia lengo iwapo kutakuwa na ongezeko la maambukizi mapya.
Kwa kuzingatia ukweli huo Rais Dkt.Samia aliiagiza Wizara ya Afya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS kuweka mikakati madhubuti na endelevu katika kutoa elimu na kampeni. 

Mambo ambayo inabidi yafike maeneo na makundi yote. Huku akiweka wazi kampeni ijikite katika upimaji, utumiaji dawa, usimamizi na matibabu.
Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alisema mafanikio yaliyopatikana yametokana na ushirikiano mkubwa baina ya serikali, wahisani, wadau,asasi mbalimbali na wananchi. 

Kwa hiyo ushirikiano na juhudi za pamoja zinahitajika. Huku akizitaka sekta zote pamoja na wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano hayo. Kwani mchango wa kila mmoja unahitajika, na siyo kazi na jukumu la Wizara ya Afya pekee.
Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pia alisisitiza suala la usawa. Alisema bila usawa itakuwa ni vigumu kufikia lengo. Hasa katika upimaji, utumiaji dawa, uangalizi na matibabu. 

Ingawa alitahadharisha kwamba maradhi kama UKIMWI ambao upo duniani kote ni kazi ngumu kuwa na usawa kwa haraka, ni kazi inayohitaji muda wa kutosha.
Rais alibainisha kwamba mafanikio yaliyofikiwa yalitumia fedha ambazo zilitolewa na wahisani, wadau na serikali. 

Hata hivyo, alisema japokuwa wahisani wanaonesha dhamira ya kuendelea kusaidia fedha na huduma nyingine kutokana kuridhishwa na juhudi zinazofanyika, lakini sisi wenyewe kama nchi tunatakiwa kupata fedha kutoka kwenye vyanzo vyetu vya mapato ya ndani badala ya kutegemea wahisani pekee yao.
Aidha, mkuu huyo wa nchi alisema licha ya mafanikio hayo lakini yapo maeneo ambayo hayafanywa vizuri na kwa kiwango cha kuridhisha. Miongoni kwa maeneo hayo alilitaja eneo la unyanyapaa kwa wanaoishi na VVU. Huku pia akilitaja eneo la usawa.

Alisema kukosekana usawa katika upimaji, utumiaji dawa, uangalizi na matibabu kunaweza kusababisha kuathiri na kukwamisha juhudi kubwa zinazofanyika. Kwahiyo inaweza kuwa kazi ngumu kufikia lengo ambalo kwa mujibu wa tamko la Umoja wa Mataifa kutokomeza UKIMWI, maambukizi na unyanyapaa ifikapo mwaka 2030 lazima litimie.
"Maradhi haya hayaheshimu mipaka, yapo Dunia nzima. Kwa hiyo kupata usawa katika upimaji, matunzo na matibabu ni kazi kubwa. Kazi hiyo inategemea sisi wenyewe,"alisema Dkt.Samia.
Alisema, licha ya tamko la Umoja wa Mataifa la kutokomeza UKIMWI.Kunahitajika mkakati madhubuti na endelevu kwetu wenyewe kama nchi. Kwa kuzingatia ukweli huo kuna mpango wa tatu ili kufikia lengo la sifuri tatu ambalo ni kutokomeza maambukizi, UKIMWI na Unyanyapaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news