YALIYOSISIMUA 2022:Ujenzi wa barabara,madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe na matofali ya kuchoma

NA MWANDISHI WETU

MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amesema ujenzi wa barabara na madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe na matofali ya kuchoma unaokoa gharama kwa asilimia 50.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dodoma, Mhandisi Seff alisema teknolojia hiyo inapunguza gharama kwa sababu inatumia malighafi ambazo zinapatikana katika maeneo husika.

“Tumejenga madaraja ya mawe zaidi ya 73 Kigoma kwa shilingi bilioni 1.4, lakini pia ujenzi unaendelea katika Mkoa wa Mwanza, Iringa na Singida ambapo bei ni nafuu na ukizingatia mawe yanapatikana katika maeneo mengi nchini,”alisema Mhandisi Seff.

Aliongeza kuwa, mkakati wa TARURA ni kuanza kufundisha mafundi katika kujenga madaraja hayo ili nao waweze kufundisha wengine.

Kwa upande wake Mratibu wa madaraja ya mawe, Mhandisi Pharles Ngeleja alisema mipango iliyopo ni kuhakikisha wanawezesha mafunzo kwa wahandisi ili waweze kufahamu kwasababu wao ndio wasimamizi wa miradi.

"Bado kuna changamoto kwa baadhi ya wananchi juu ya teknolojia hii lakini elimu inaendelea kutolewa na tunaamini itafika muda ambao wananchi wataielewa vizuri maana teknolojia hii ni ya gharama nafuu na huleta matokeo chanya kwani ukiangalia miundombinu mingi ya zamani ilitumia teknolojia hii," alisema.

Alisema, madaraja yanayojengwa kwa kutumia teknolojia ya matofali na mawe ni imara na yana uwezo wa kukaa zaidi ya miaka 200.

"Ukiangalia nchi za wenzetu wana madaraja ambayo walijenga kwa kutumia chokaa lakini hadi leo yapo na yanafanya kazi hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi waipokee teknolojia hii,"alisema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliipongeza TARURA kwa kutumia teknolojia hiyo ambayo itasaidia kuokoa fedha za serikali.

Mkazi wa Makulu, Godwini Chisili alisema amevutiwa zaidi na ujenzi wa barabara na madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe na matofali kwasababu ni malighafi ambazo zinapatikana katika mikoa mingi nchini na kutokana na kupatikana kwa malighafi hizo kutasaidia serikali kupunguza gharama za ujenzi.

“Sasa tumepiga hatua tunachoomba ujenzi wa barabara na madaraja hayo uzingatie ubora na hatutegemei kuona daraja linajengwa ndani ya wiki tatu linakatika,"alisema.

Aidha, ameishauri Serikali kuona umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa wazawa wakati wa utekelezaji wa miradi hii ili kuwezesha teknolojia kusambaa kwa urahisi na kutumika katika maeneo mengi yenye mawe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news