Yanga SC wanakula raha huku Polisi Tanzania wakiugulia maumivu mkiani, Simba SC kimya huku Azam FC kicheko

NA DIRAMAKINI

MASHABIKI wa Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam wameendelea kuwa na raha zaidi baada ya klabu yao hiyo kuendelea kudhirisha soka wanalijua na wanachotaka ni mataji tu.

Ni kutokana na ukweli kwamba vigogo hao wa Jangwani ambao wamecheza mechi 15 wamekamilisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kwa kutwaa alama 38 ambazo zinawafanya kuendelea kung'ara kileleni.

Yanga SC inawaongoza wenzake 16 chini huku watani wao ambao walipata nafasi ya kukaa nafasi hiyo kwa saa chache, Simba SC wakiendelea kubakia nafasi ya tatu kwa alama 24 za michezo 15.

Mabingwa hao watetezi, Desemba 7, 2022 wamekamilisha mzunguko huo kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji, Namungo FC.

Wenyeji hao wa Kusini walitembezewa kichapo hicho katika Uwanja wa Majaliwa uliopo mjini Ruangwa mkoani Lindi.

Mchezaji Bora wa msimu uliopita, Yanick Litombo Bangala dakika ya 40 na winga Tuisila Kisinda dakika ya 82 ndiyo walifunga hesabu ya ushindi huo.

Ukifuatiwa ule wa awali ambao Yanga SC iliwapiga Tanzania Prisons bao 1-0 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC wakiwaondoa Simba SC iliyokalia usukani kwa huo kwa saa kadhaa, mara baada ya kupata ushindi mnono kwenye mechi ya dhidi ya Coastal Union kwenye mchezo uliochezwa Desemba 3, 2022 huko Mkwakwani jijini Tanga.

Mchezo huo kati ya Yanga SC na Tanzania ulipigwa Desemba 4, 2022 majira ya saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam ambapo Tanzania Prisons licha ya kuwa ugenini walifanikiwa kuwadhibiti wenyeji hao kwa dakika 88.

Aidha, baadaye dakika ya 89,ulinzi ulivurugwa baada ya Feisal Salum (Fei Toto) kupachika bao pekee lililowapeleka Prisons nje wakiwa vichwa chini.

Bao hilo la Feitoto lilipatikana kutokana na usumbufu alioingia nao Benard Morrison dakika za mwisho ambaye alionekana kuwatia presha zaidi walinzi wa Tanzania Prisons hatimaye kukubali yaishe.

Cedric Kaze, kocha msaidizi wa klabu hiyo alisema kuwa mchezo huo ilikuwa mgumu kutokana na ubora wa Tanzania Prisons katika kulinda na kufanya mashambulizi makali ya kushtukiza jambo ambalo liliwapa ugumu wachezaji wake na kuwafanya wataabike kwa dakika zote 88 bila bao.

Kwa upande wake,kocha wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo alisema mchezo huo ulikuwa na peresha kubwa kwao na kwamba mpango walioingia nao kwanza ni kuwaheshimu Yanga kutokana na ubora wa kikosi chao.

Sambamba na kuwa na wachezaji wenye viwango vizuri kwa moja moja. Aliongeza kuwa, wachezaji wake walifanya jitahada kubwa kuhakikisha wanatoka na alama yeyote, lakini mpango huo ulivurugwa na timu hiyo ya Jangwani.

Odhiambo aliwapongeza Yanga SC kwa kuipambania timu yao kwa udi na uvumba na kuhakikisha wanapata matokeo hata kwenye wakati mgumu kama ilivyokuwa kwenye mchezo huo.

Wakati huo huo, katika Ligi Kuu ya NBC yenye timu 16, nafasi ya pili inashikiliwa na Azam FC ya jijini Dar es Salaam ambao baada ya michezo 15 wamekusanya alama 35.

Nafasi ya tatu ikishikiliwa na Simba SC ya jijini Dar es Salaam ambayo baada ya michezo 15 wamekusanya alama 34. Singida Big Stars kutoka mkoani Singida inashika nafasi ya nne baada ya kutumia michezo yake 15 kujikusanyia alama 27.

Aidha, nafasi ya tano inashikiliwa na Geita Gold FC kutoka mkoani Geita ambayo baada ya michezo 15 imejikusanyia alama 22.

Mchezo uliopigwa Desemba 4, 2022 majira ya saa 10:00 kwenye dimba la Geita, kati ya wenyeji na Mtibwa Sugar ulimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu kwa kufungana bao 2-2.

Katika mchezo huo timu zote zilikuwa na shauku ya kushinda, zikipambana kutafuta kumaliza duru ya kwanza kwa kuvuna alama tatu.

Lakini mpaka dakika zinatamatika hakuna aliyeweza kuibuka na alama zote tatu, baadala yake wawili hao waliambulia alama moja moja.

Mtibwa Sugar ndiyo waliotangulia kuandika bao la kuongoza katika dakika ya 10 ya mchezo kupitia kwa Juma Nyangi huku Geita Gold wakijibu mapigo kunako dakika ya 35 ya mchezo kupitia kwa Saidi Ntibazonkiza aliyekwamisha kimiani mkwaju wa penati na kuzifanya timu hizo kwenda kwenye mapumziko ubao ukisoma 1-1.

Kipindi cha pili Geita Gold waliuanza mchezo kwa kasi zaidi na kufanikiwa kuandika bao la pili kunako dakika ya 49 kupitia kwa Juma Liuzio, bao hilo likisawazishwa na Mtibwa Sugar jioni kunako dakika ya 90+ ambapo mchezaji wa Geita Gold, George Wawa.

Kocha Mkuu wa Geita Gold,Fred Felix Minziro alisema kuwa, timu yake imepambana vilivyo, lakini mwishoni walifanya makosa ambayo yaliwanufaisha Mtibwa Sugar huku kocha Mkuu wa Mtibwa Salum Mayanga naye akisema matokeo hayo kwake yana nafuu kuliko kupoteza alama zote.

Mayanga aliongeza kuwa, ligi ya mwaka huu ni ngumu kwa kuwa kila timu inasaka kufanya vizuri, hivyo haikuwa rahisi kupata alama hiyo moja.

Aidha, katika mchezo huo kiungo mshambuliaji, Saidi Ntibazonkiza hakuweza kumaliza dakika 90 baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwa kumchezea faulo mchezaji wa Mtibwa Sugar.

Wakati huo huo, nafasi ya sita inashikiliwa na Mtibwa Sugar FC ambayo baada ya michezo 15 ilijikusanyia alama 22, Kagera Sugar FC nafasi ya saba ambayo baada ya michezo 15 imejikusanyia alama 21.

Pia nafasi ya nane inashikiliwa na Mbeya City FC kutoka mkoani Mbeya ambayo baada ya michezo 15 imejikusanyia alama 20, huku nafasi ya tisa ikishikiliwa na Namungo FC kutoka mkoani Lindi ambayo baada ya michezo 15 imejikusanyia alama 18.

Nafasi ya 10 inashikiliwa na KMC FC kutoka jijini Dar es Salaam ambayo baada ya michezo 15 imejikusanyia alama 16, nafasi ya 11 inashikiliwa na Tanzania Prisons FC ambayo baada ya michezo 15 imejikusanyia alama 15.

Katika hatua nyingine, nafasi ya 12 inashikiliwa na Coastal Union FC ambayo baada ya michezo 15 imejikusanyia alama 15, nafasi ya 13 inashikiliwa na Dodoma Jiji FC kutoka jijini Dodoma ambayo baada ya michezo 15 imejikusanyia alama 15.

Ihefu FC kutoka Mbarali mkoani Mbeya inashika nafasi ya 14 ambayo baada ya michezo 15 imejikusanyia alama 11, nafasi ya 15 inashikiliwa na Ruvu Shooting FC ambayo baada ya michezo 15 imejikusanyia alama 11 huku wanaoburuza mkia nafasi ya 16 wakiwa ni Polisi Tanzania FC ambayo baada ya michezo 15 imeambulia alama tisa tu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news