Aliyekwea juu ya nguzo ya umeme mkubwa alijigamba yeye ni Mayele na hawamuwezi

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Kijiji cha Mwibagi, Kata ya Kyanyari wilayani Butiama Mkoa wa Mara, Nashon Thomas amesema kuwa, kijana aliyepanda kwenye nguzo za umeme wa msongo wa Kilovati 123 kwenye njia ya Mwanza-Musoma, alikuwa anajitapa kuwa yeye ni Fiston Kalala Mayele hawamuwezi.
Mayele kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni miongoni mwa washambuliaji hatari zaidi wa Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam ambaye ameiwezesha klabu hiyo kuendelea kufanya vizuri katika siku za karibuni.

Aidha, kijana huyo tayari anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mara kwa kosa la kupanda juu ya nguzo ya umeme, huku lengo lake likiwa bado halijajulikana.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele alisema kuwa kijana huyo alipanda kwenye nguzo ya umeme iliyopo katika Kijiji cha Mwibagi kando ya Barbara ya Musoma- Mwanza ambapo haikujulikana alikuwa na lengo gani.

Alisema kuwa, baada ya tukio hilo watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Mara walifika katika eneo hilo na kumshusha mtu huyo kisha kumkabidhi kwa polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Ikumbukwe kuwa, matukio ya namna hiyo yamekuwa yakijirudia ambapo moja ya tukio ambalo lilizua gumzo miaka kadhaa iliyopita ni lile la mkazi wa Kijiji cha Butulwa Kata ya Old Shinyanga, aliyetambuliwa kwa jina la Bw. Shija Machiya (30) kupanda kwenye moja ya nguzo za umeme wa njia kubwa inayopitisha umeme kwenda kwenye mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, ulioko Kahama, mkoani Shinyanga.
Hatua ya Bw. Machiya kupanda katika nguzo hiyo inayosafirisha umeme wa msongo wa KV 220 katika eneo la kiwanda cha nyama ilisababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo ambao waliacha shughuli zao kwa muda wakihofia maisha yake.

Kwa mujibu wa maelezo ya mama mzazi wa Bw. Machiya, Bi. Mondesta Madirisha, alisema awali mtoto wake alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kuchanganyikiwa akili kutokana na kile walichohisi kuwa ni malaria kali, ambapo waliamua kumpatia dawa za kienyeji na hali yake ilionesha kuwa ya kuridhisha.
Hata hivyo, Bi. Madirisha alisema, baadaye hali ilibadilika ghafla na alianza kupiga kelele na kutoroka nyumbani kwao na kuanza kukimbia ovyo barabarani hali ilisababisha baadhi ya wanakijiji kuanza kumfuatilia.

“Wakati natokea shamba, ghafla nilikutana naye akikimbia mbio, nilimsemesha na kumuomba asimame, lakini aligoma kabisa na kukimbilia eneo ambalo kulikuwa na watu wakilima, niliwaomba msaada ili waweze kumkamata, lakini aliwazidi mbio na hapo hapo aliamua kupanda katika nguzo ya umeme na kwenda juu kabisa,” alisema Bi. Madirisha miaka kadhaa iliyopita kijijini hapo.
Alisema baada ya kuona hali hiyo waliamua kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali ya kitongoji na kijiji ambao walichukua hatua za kuuarifu uongozi wa Shirika la Umeme (TANESCO) waliofika eneo la tukio na kuwasiliana na polisi pamoja kikosi cha zimamoto.

Katika tukio hilo, waandishi wa habari walishuhudia harakati za kuteremshwa kwa kijana huyo juu ya nguzo hiyo ambapo mbinu zilitumika ili kumteremsha bila kuleta madhara yoyote huku akirajibu kuwachenga kwa kupanda juu zaidi ya nguzo na kuvua nguo zote mwilini na kubaki uchi wa mnyama.

Mmoja wa maafisa wa TANESCO wakati huo alisema, kitendo cha Bw. Machiya kupanda katika nguzo hiyo kingeweza kuhatarisha uhai wake kutokana na njia hiyo kupitisha umeme mkubwa wa msongo wa KV. 220.
“Baada ya kupata taarifa na kufika eneo la tukio tulilazimika kuzima umeme haraka katika njia hiyo, ambapo juhudi za kumteremsha kijana huyo zilifanyika kwa ushirikiano wa kikosi cha zima moto na uokoaji manispaa ya Shinyanga, jeshi la polisi na wananchi na kufanikiwa kumteremsha bila ya madhara,”alieleza Afisa huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news