MMEPEWA JUKUMU KUHUBIRI HABARI NJEMA

NA ADELADIUS MAKWEGA

WAKRISTO wameambiwa kuwa kila mmoja amepewa jukumu la kuhubiri habari njema kwa watu wato, kila Mkristo anatakiwa kuacha shughuli zote na kumtangaza Kristo.

Hayo yamesemwa katika misa ya Jumapili ya tatu ya mwaka wa Liturujia ya Kanisa, Januari 22, 2023 katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.
Akihubiri mara baada ya kusomwa masomo mawili na Injili ya Dominika hiyo Padri Paul Mapalala amesema, “Kazi ya kumtangaza Kristo siyo kazi nyepesi, kwa maana ina mambo mengi, kuna wakati mtu anaweza kudhani anamtangaza Kristo, kumbe anajitangaza mwenyewe au anautangaza ubaya wa watu wengine.”

Kazi kubwa ni kutangaza wema wa Mungu kwa kila mmoja na kila mmoja anayo nafasi yake kwa kutukusanya sote pamoja kwa kulisikiliza neno la Mungu na kulipeleka kwa wengine.

“Wakristo tunapaswa kuwa tayari kumfia Kristo na siyo kuyafia mambo mengine, kama Yesu alivyowakusanya wanafunzi wake, wakaacha na waliyokuwa wakiyafanya na kuambatana naye.”

Mara baada ya mahubiri hayo waamini walisali Sala ya Kanuni ya Imani na baada ya sala hii yalisomwa maombi ya misa hiyo na mojawapo lilikuwa hili. “Uliwasamehe wote waliokujia wewe, utupe moyo wa sisi kuwasamehe pia wale wote wanaotukosea.”

Mwishoni mwa misa hiyo walitambulishwa watawa kadhaa wageni wa kike ambao wanatarajiwa kuanzisha miradi kadhaa ya kimaendelea katika Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma na mpaka misa hiyo ya kwanza inamalizika, mvua katika eneo la Chamwino Ikulu imeendelea kunyesha vizuri na wakulima bado wengine wakipanda kwa mara ya kwanza, wengine wakirudishie mbegu mashambani mwao maeneo zilipoota kidogo na wengine wakipalilia mashamba hayo palizi ya kwanza.

Post a Comment

0 Comments