Benki Kuu yatadharisha udaganyifu wa fedha mitandaoni

NA DIRAMAKINI

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imebaini kuongezeka kwa udanganyifu wa fedha nchini unaohusisha mwananchi kupokea taarifa kwa maana ya hati au barua pepe inayodai kuwa ni uthibitisho wa malipo kupitia SWIFT au mifumo mingine ya uhamishaji fedha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 6, 2023 na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefafanua kuwa, mpokeaji anafahamishwa kuwa fedha zimeingizwa kwenye benki au akaunti katika taasisi ya fedha nchini Tanzania jambo ambalo halina ukweli.

"Wakati mwingine, mpokeaji fedha anaelekezwa kulipa kiasi fulani cha fedha kuwezesha kupata fedha hizo nyingi. Matukio mengi ya taarifa hizo yanahusisha kiasi kikubwa cha pesa kinachodaiwa kuletwa kwa ajili ya ufadhili wa mradi au matumizi binafsi.

"Hivyo, Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutaarifu umma kwamba taarifa hizo ni za kughushi na za kubuni. Wananchi mnashauriwa kuwa waangalifu na kuacha kujihusisha na miamala hiyo ambayo kwa kawaida inalenga kuwatapeli fedha,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo ya BoT.

Pia, BoT imewataka wananchi kuzingatia kanuni bora za kufanya miamala ya fedha ili kuepuka upotevu wa fedha ambazo ni kuhakikisha usalama wa taarifa za fedha wakati wa kutoa taarifa binafsi mtandaoni (tovuti, mitandao ya kijamii), kupitia barua pepe au kwenye simu.

"Wananchi hawapaswi kujibu barua pepe, barua au simu zinazoahidi kupokea fedha kutoka kwa watu au kampuni wasizozifahamu vizuri na kuwa waangalifu mnapofanya malipo ya mtandaoni kwa kufanya uhakiki wa mshirika wa kibiashara (mtu au kampuni) kabla ya kutoa maelezo au kufanya malipo.

"Aidha, wananchi waliokumbwa na matatizo hayo wanashauriwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama kwa hatua stahiki,"imefafanua Benki Kuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news