Dodoma Jiji yapongezwa kwa kuwajali Wamachinga

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Philip Isdori Mpango ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa jitihada kubwa za kuhakikisha inatoa kipaumbele katika eneo la uwekezaji.

Hayo yamesemwa leo Januari 20, 2023 kupitia hotuba ya Makamu wa Rais iliyosomwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe.Angellah Kairuki (Mb) katika hafla ya kuufahamisha umma mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Mkoa wa Dodoma.

"Katika eneo la uwekezaji, niwapongeze kwa soko la machinga lililojengwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na Serikali Kuu. Hii inadhihirisha jinsi ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan inavyojali vijana hususani wajasiriamali wadogo wanaotafuta riziki yao kwa njia za halali.

"Hii pia inaonesha nia ya Serikali kutambua mchango wa wananchi katika uchumi wa Taifa lao. Ninaipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kukamilisha mradi huo kwa wakati na kuwahamishia wajasiriamali wadogo katika soko hilo bila usumbufu wowote,"amefafanua Mhe.Kairuki kwa niaba ya Makamu wa Rais.

Amesema, kuwaweka vijana wajasiriamali wadogo pamoja, kumefanya Jiji la Dodoma lianze kuonekana safi na lenye mazingira bora.

"Nizitake halmashauri zote nchini kutenga na kuyaendeleza maeneo maalumu kwa ajili ya wamachinga na wafanyabiashara wadogo wadogo.

"Na niwaombe wamachinga na wafanyabiashara ndogo ndogo kuitika wito wa Serikali unaowataka kuhamia katika maeneo yaliyoboreshwa bila usumbufu wowote. Ninaamini hata wao wanapenda kuwahudumia wateja wao katika mazingira bora zaidi,"amefafanua.

Pia amewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza mkoani Dodoma. Amesema, yapo maeneo yaliyotayarishwa kwa ajili ya uwekezaji kwenye viwanda vya aina zote, biashara ikiwemo shopping malls, supermarkets, maduka madogomadogo, viwanja vya michezo ikiwemo vya golf course,hoteli hususani hoteli za hadhi ya nyota tatu na maeneo maalum kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news