Serikali yasema uchumi umeendelea kuimarika

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Philip Isdori Mpango amesema, uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika licha ya changamoto iliyoikumba Dunia ya UVIKO-19 na vita kati ya Urusi na Ukraine.

Hayo yamesemwa leo Januari 20, 2023 kupitia hotuba ya Makamu wa Rais iliyosomwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe.Angellah Kairuki (Mb) katika hafla ya kuufahamisha umma mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Mkoa wa Dodoma.

"Nina furaha kujumuika nanyi leo hapa Dodoma katika Ukumbi huu wa TAG kushirikiana na nanyi kuufahamisha Umma wa Watanzania na dunia kwa ujumla mambo makubwa ambayo kwa neema za Mwenyezi Mungu na juhudi za watanzania hususan wana-Dodoma zimetuwezesha kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

"Jambo la kwanza, sisi sote ni mashahidi kuwa uchumi wa nchi yetu umeendelea kumaimarika. Tanzania ni nchi ya mfano duniani katika usimamizi wa uchumi ambapo, licha ya majanga ikiwemo changamoto za UVIKO 19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine,"amesema Mhe.Kairuki kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt.Mpango.

Amefafanua kuwa, tathimini ya Benki ya Dunia inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania uko imara. Kulingana na taarifa za Benki Kuu, katika robo ya kwanza ya mwaka 2022 uchumi umekua kwa asilimia 4.8 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.8 katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia 2021.

"Hata hivyo, kutokana na mipango kabambe iliyowekwa na Serikali, tunatarajia uchumi utakua zaidi hadi kufikia
wastani wa asilimia 5.0.

"Nichukue fursa hii kumpongeza sana Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa na mikakati thabiti inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita iliyopelekea uchumi wa nchi yetu kukua kwa viwango hivi.

"Takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Dodoma umeendelea kukua katika uchangiaji wa Pato la Taifa ambapo unachangia asilimia 3.1 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 2.9 ya miaka mitano iliyopita,"amefafanua.

Pia amebainisha kuwa, bado Dodoma ina uwezo wa kuchangia zaidi katika Pato la Taifa kutokana na na fursa ya kuwa na idadi kubwa ya watu.

Matokeo ya Sensa ya Mwaka 2022 yanaonesha kuwa, Mkoa wa Dodoma una jumla ya watu 3,085,625. "Nihimize wananchi wa Dodoma kufanya kazi kwa bidi na kutulia fursa za uwekezaji zinazojitokeza baada ya Serikali kuhamishia shughuli zake hapa Makao Makuu, ili kukuza uchumi wa Dodoma na mchango wake katika Pato la Taifa,"amesisitiza Makamu wa Rais.

Mapato

Wakati huo huo, Waziri Kairuki kwa niaba ya Makamu wa Rais amesema, ni jambo la heri kusikia kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na halmashauri za Mkoa wa Dodoma zinaendelea kukua katika kuongeza mapato na zinafikia malengo na nyingine kupita malengo yaliyowekwa.

"Hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya mkoa pamoja na nchi kwa ujumla. Juhudi hizi za TRA na halmashauri zetu nchi nzima ndio zitakazowezesha nchi yetu kukusanya shilingi trilioni 23.653 ya mapato ya kodi na shilingi trilioni 1.012 mapato ya ndani ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2022/23 (Kitabu cha bajeti, 2022/23).

"Fedha hizi ndio nguzo ya bajeti ya Serikali na zinatumika kupeleka huduma muhimu kwa wananchi. Watanzania wakiendelea kulipa kodi na tozo mbalimbali kwa uaminifu, kwa furaha, kwa kujituma na kwa bidii itawezesha nchi yetu kufikia hatua ya kujitegemea kimapato,"ameongeza.

Kilimo

Pia amesema, amefarijika kusikia kuwa,kuna hatua nzuri na kubwa iliyofikiwa katika Sekta ya Kilimo hususani kwenye mazao ya alizeti, mtama na zabibu.

Sekta ya Kilimo ni sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania kwa kuwa ni chanzo kikuu cha chakula, ajira, fedha za kigeni na malighafi zinazotumika viwandani.

"Tanzania imejaliwa kuwa na hali ya hewa na kanda za kijiografia tofauti zinazowezesha wakulima na wafugaji kuzalisha mazao ya kilimo, mifugo na kufuga samaki,"amesema.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi mwaka 2020,mchango wa Sekta ya Kilimo katika Pato la Taifa (GDP) ni asilimia 26.9. "Na kwa kweli kaya za Watanzania wengi (asilimia 65.3) kiuchumi, zinajihusisha na shughuli za kilimo,"amesema.

Mheshimiwa Kairuki amesema, Serikali kupitia Sera na programu mbalimbali imekusudia kuleta maendeleo makubwa ya kilimo ikiwa ni pamoja na kufanya kilimo kuwa eneo la uwekezaji linalovutia vijana na wasomi.

"Nitumie mkutano huu kuwahimiza vijana wetu wa Kitanzania kuchangamkia fursa za kilimo zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo mfano program ya Building Better Tomorrow (BBT).

"Ni muhimu kuhakikisha tuna tumia pembejeo kama vile mbegu bora na mbolea ili kufanya kilimo kiwe na tija. Watanzania wote tutumie kipindi hiki cha mvua kuhakikisha kila ardhi inayofaa kwa kilimo imelimwa, kupandwa na kutunzwa kitaalam ili tujihakikishie usalama wa chakula na kuinua hali ya lishe nchini.

"Nimefurahi kuona kuwa Mkoa wa Dodoma umetekeleza agizo la Mhe.Makamu wa Rais la kutenga maeneo ya kilimo mijini ili kwezesha kilimo cha mjini (urban farming). Na hapa niendelee kusisitiza, Mikoa yote ihakikishe mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya mjini inajumuisha kilimo,"amefafanua Mhe.Kairuki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news