HUDA USALAMA WAKO: Bodaboda, abiria, mjenzi jali kichwa chako kwanza

NA LWAGA MWAMBANDE

KOFIA ngumu kwa maana ya Huda ni moja wapo ya nyenzo muhimu ambayo huwa inavaliwa na wahandisi, waendesha pikipiki,abiria, wachimba migodi, askari waliopo vitani au wakaguzi wa miradi mbalimbali ya ujenzi.
Nyenzo hii ni muhimu zaidi katika mazingira yetu ya kila siku hususani kwa shughuli za ujenzi na usafiri wa pikipiki. Miongoni mwa faida zitokanazo na Huda ni kukilinda kichwa pindi ajali inapotokea.

Inaelezwa kuwa, mfano ukiwa katika pikipiki ikapata ajali, sehemu hatari zaidi kupata majeraha wakati huo ni kichwa, hivyo uvaaji wa Huda huwa unasaidia kujikinga dhidhi ya majeraha hayo kwa sababu zimetengenezwa kwa mfumo ambao unaweza kukilinda kichwa dhidhi ya hali hiyo.

Vivyo hivyo katika shughuli za ujenzi. Sambamba na kujikinga na madhara ya kimazingira kulingana na maeneo ambayo unatekeleza majukumu yako. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ukivaa Huda upo salama wakati unaendelea kutekeleza majukumu yako ya kila siku. Endelea;

1.Huda usalama wako,
Huda hiyo kinga yako,
Na tena Amani yako,
Hakiki wavaa huda.

2.Kwa kuchakarika kwako,
Na kuwajibika kwako,
Muhimu salama yako,
Kichwani uvae huda.

3.Waliosoma wenzako,
Wenye kazi kama yako,
Kwao hakuna vituko,
Lazima kuvaa huda.

4.Unao mradi wako,
Wa huo ujenzi wako,
Huo uhandisi wako,
Muhimu kuvaa huda.

5.Angalia boda yako,
Kwa hizo safari zako,
Nao abiria wako,
Hakiki mwavaa huda.

6.Hii ni elimu kwako,
Sambaza na kwa wenzako,
Huo usalama wako,
Inasaidia huda.

7.Itoe kapelo yako,
Au hilo pama lako,
Havina chochote kwako,
Unachohitaji huda.

8.Ni mashambulizi kwako,
Ni mapenzi yangu kwako,
Mabaya yasije kwako,
Hakiki unayo huda.

9.Kofia ngumu ni yako,
Magumu yakija kwako,
Ibakie kinga yako,
Uwe kaka au dada.

10.Ni baiskeli yako,
Na huo ujenzi wako,
Ajali ifike kwako,
Itakuokoa huda.

11.Ukigonge kichwa chako,
Ukiwa na mwendo wako,
Hakiguswi kichwa chako,
Badala yake ni huda.

12.Pengine ujenzi wako,
Lishuke tofali kwako,
La kubonda kichwa chako,
Hufi sababu ya huda.

13.Unayo leseni yako,
Nayo pikipiki yako,
Ukianza mwendo wako,
Lazima kuvaa huda.

14.Huda ni maisha yako,
Ya wategemezi wako,
Na tena ni ya mwenzako,
Siyo kitu cha ziada.

15.Huko kuhimizwa kwako,
Pia kukumbushwa kwako,
Jua ni upendo kwako,
Ulipo iwepo huda.

16.Ni wengi jamaa zako,
Wengine sasa hawako,
Walivifanya vituko,
Kichwani pasipo huda.

17.Kufika ajali huko,
Na kubondwa kichwa huko,
Na kinga haikuwako,
Kwa kutokuvaa huda.

18.Lakini pia wenzako,
Hao ushuhuda kwako,
Huda kichwani kuwako,
Maisha ni kawaida.

19.Hii ni elimu kwako,
Mjulishe na mwenzako,
Na utani usiweko,
Muhimu tumia huda.

20.Abiria pia kwako,
Wadandia boda yako,
Hakiki kichwani kwako,
Umejivalisha huda.

21.Mwadai uchafu uko,
Na majashojasho yako,
Hamtaki shombo huko,
Nunua za kwenu huda.

22.Kichafue kichwa chako,
Uokoe fuvu lako,
Na pia uhai wako,
Hakiki wavaa huda.

23.Huda ni mkanda wako,
Huda egemeo lako,
Ajali ikija kwako,
Kuumia kawaida.

24.Iwe bodaboda yako,
Au panda ya mwenzako,
Jali usalama wako,
Hakiki wavaa huda.

25.Wafanya ujenzi wako,
Wa hiyo ghorofa yako,
Au kazi kwa mwenzako,
Jikinge kichwa na huda.

26.Naona miguu yako,
Buti ngumu ni za kwako,
Vilevile kichwa chako,
Jikinge uvae huda.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news