Salamu za Jumapili: NJE YA BIDII ZETU

NA LWAGA MWAMBANDE

WENGI wetu tumekuwa tukipitia changamoto mbalimbali katika maisha yetu ya kila siku iwe kiuchumi, kiafya, kifamilia na wakati mwingine mipango tuliyonayo kushindwa kufikia mwisho.

Haya yanatukabili ikiwa bado tunafanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha kila mpango unatimia kadri ya malengo tuliyojiwekea, inapofikia yote kukawia kutimia, kukata tamaa, kulaumu na kuanza kunyoosheana vidole imekuwa sehemu ya njia moja wapo ya kuona ndiyo hatua nyepesi ya kujifariji, bila kutambua kuwa, tunayaweza yote katika yeye atutiaye nguvu. Rejea, Biblia Takatifu kitabu cha Wafilipi 4:13.

Credit: Getty Images/iStockphoto.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, licha ya mapambando yote unapaswa..."Mkabidhi Mwenyezi Mungu maisha yako;mtumainie yeye naye atafanya kitu." Rejea, Biblia Takatifu kitabu cha Zaburi 37: 5. Endelea;


1.Nje ya bidii zetu, nje ya juhudi zetu,
Ndiyo kweli kuna vitu, vyazidi uwezo wetu,
Kufanya si kazi yetu, tusichoshe nguvu zetu,
Yaliyotushinda sisi, yeye ni ushindi wetu.

2.Kwenye jitihada zetu, kwa maendeleo yetu,
Tutumie nguvu zetu, pia maarifa yetu,
Na tusibweteke katu, ila vile juu yetu,
Yaliyotushinda sisi, Bwana ni ushindi wetu.

3.Sisi tuna Mungu wetu, anajali mambo yetu,
Anaona kazi zetu, hata kujituma kwetu,
Aona kushinda kwetu, na pia kushindwa kwetu,
Yaliyotushinda sisi, Bwana ni ushindi wetu.

4.Hatuna uwezo katu, kwa mambo yote ya kwetu,
Mengine uwezo wetu, tunacho kikomo chetu,
Huo si upweke wetu, tuna kimbilio letu,
Yaliyotushinda sisi, Bwana ni ushindi wetu.

5.Umejitahidi mtu, kuutoa ukurutu,
Sisemi ugonjwa wetu, ila changamoto zetu,
Huo ni ukomo wetu, tuna egemeo letu,
Yaliyotushinda sisi, Bwana ni ushindi wetu.

6.Tunazo fadhaa zetu, ziletazo shida kwetu,
Si kuchakarika kwetu, tupate jawabu kwetu,
Sababu uwezo wetu, huo una mwisho wetu,
Yaliyotushinda sisi, Bwana ni ushindi wetu.

7.Milima i mbele yetu, si Kilimanjaro wetu,
Zile changamoto zetu, kupanda ni ngumu kwetu,
Tumwendee Mungu wetu, ndiye ufumbuzi wetu,
Yaliyotushinda sisi, Bwana ni ushindi wetu.

8.Karuhusu Mungu wetu, kwamba zile shida zetu,
Ambazo kwa nguvu zetu, hakuna uwezo kwetu,
Tukabidhi njia zetu, awe tumaini letu,
Yaliyotushinda sisi, Bwana ni ushindi wetu.

9.Usilielie katu, huko peke yako mtu,
Tuko naye Mungu wetu, anajali mambo yetu,
Hataki kushindwa kwetu, yeye ni majibu letu,
Yaliyotushinda sisi, Bwana ni ushindi wetu.
(Zaburi 37:5, Mithali 16:3/)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news