Jengo la Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo litakuwa na vionjo vitatu-Yakub

NA ADELADIUS MAKWEGA

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini ndugu Said Yakub siku ya Januari 3, 2023 amesema kuwa kwa sasa ujenzi wa jengo la wizara hiyo umefikia asilimia 57 na asilimia 43 zilizosalia zitamalizika kabla ya mwisho wa Oktoba, 2023 ambapo wanatarajiwa kukabidhiwa rasmi na Mkandarasi Mjenzi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Akizungumza kando ya jengo hilo kubwa huku sauti yake ikisindikizwa na milio ya nyundo na misumari alipokwenda kufanya ukaguzi maalumu akiambata na Wakurugenzi wa sekta zote tatu za Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Naibu Katibu Mkuu Yakub alisema kuwa,

“Mpaka sasa Mkandarasi Mjenzi NHC ametumia miezi 14 na amebakiza miezi 10 kumalizia kazi kadhaa ambazo ni kuweka sakafu, kung’arisha kuta, kuweka mabomba ya maji, kuweka umeme, vifaa vya zima moto na usafi. Nina imani NHC watamaliza mapema na kwa ubora mkubwa.”

Akiendelea kukagua jengo hilo hatua kwa hatua Ndugu Yakub amesema kuwa jengo la wizara hii lina vionjo kadhaa vya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambavyo vitapatikana hapo tu na wadau wa sekta hizo na Watanzania wote wajiandae kuona hilo.

“Jengo letu ni kubwa na litaweza kuwapokea watumishi zaidi ya 300 ambapo kutakuwa na ofisi kadhaa na kumbi za kufanyia mikutano.”
Awali Naibu Katibu Mkuu Yakub alipokea tuzo mbalimbali ambazo wizara yake imepata katika utendaji wake wa kazi kwa mwaka 2022 huku akisema kuwa kwa mwaka 2023 wizara hii inatarajia kuwa kinara katika utendaji kazi na tuzo zote zitakazoshindaniwa itashinda tu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news