Kasulu wapatiwa elimu ya upimaji wa afya

NA RESPICE SWETU

KUWEPO kwa watumishi wanaokabiliwa na magonjwa yasiyoambukiza ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuzorota kwa utendaji wa kazi katika utumishi wa umma.
Hayo yamefahamika wakati wa mafunzo na upimaji wa afya kwa hiari uliofanyika kwa watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo.

Wakizungumza wakati wa kutoa mafunzo hayo, afisa lishe wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, James Ngalaba na mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Nyakitoto Mahamud Mitende wamesema kuwa, magonjwa yasiyoambukiza hupunguza nguvu kazi na kuchangia vifo kwa asilimia 80 kwa nchi za uchumi wa chini na uchumi wa kati ikiwemo Tanzania.

Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo, wataalamu hao wamewaasa watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kujikinga na magonjwa hayo, kwa kuwa yanaepukika.
"Magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na magonjwa ya moyo, figo, saratani kiarusi na kisukari, magonjwa haya kwa kiasi kikubwa yanaweza kuepukika,"wamesema.

Wataalamu hao waliokuwa wameongozana na matabibu wengine kutoka idara ya afya ya halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, wamezitaja baadhi ya sababu zinazochangia kuwepo kwa magonjwa hayo kuwa ni pamoja na urithi, athari za mazingira, unene uliokithiri na kutokufanya mazoezi.

Sababu nyingine kwa mujibu wa wataalamu hao ni mfumo mbaya wa maisha, mafuta mengi mwilini, kukaa muda mrefu na uwezekano mkubwa kwa mgonjwa wa kisukari kupatikana kwa kutokana na familia yenye historia ya kuwa wagonjwa wa ugonjwa huo.

Kwa upande wake mganga mkuu wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Dr. Robert Rwebangila amesema kuwa, magonjwa yasiyoambukiza hayasemwi kama magonjwa mengine wakati ndio yanayosumbua zaidi kwa sasa na kuongoza katika kuathiri uchumi wa taifa na wa familia.
Akitoa mfano amesema kutokana na kukuthiri kwa magonjwa hayo, familia huingia gharama kubwa za matibabu kuliko kugharamia wagonjwa wa magonjwa mengine.

"Magonjwa haya sasa yanatishia hata uwezo wa mfuko wa bima ya afya ya taifa kutokana na gharama kubwa zinazotokana na wagonjwa wanaotibiwa magonjwa hayo,"amesema.

Ili kukabiliana na hali hiyo, watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu wameshauriwa kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi na kupima afya mara kwa mara.

Upimaji wa afya na utoaji wa mafunzo hayo, umefanyika sambamba na bonanza la watumishi wa halmashauri hiyo lililohusisha michezo ya aina mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news