KLM yarejesha safari za ndege Tanzania

NA DIRAMAKINI

SAA chache baada ya Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM) kutoa ufafanuzi na kuomba radhi juu ya kusitisha safari zake za ndege kuja Tanzania pamoja na kutoa taarifa ya uwepo wa machafuko nchini, hatimaye ndege yao imetua.
Usiku wa Januari 30,2023 ndege kubwa yenye abiria 330 imetua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) huku asilimia 95 ya abiria hao wakiwa ni watalii.

Awali kupitia barua ya Meneja wa Air France-KLM Tanzania, kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Prof.Makame Mbarawa KLM ilisema kuwa;

“Tunasikitika hatukueleza sababu iliyotufanya tuamue kusitisha safari za ndege zetu Dar es Salaam kwa sasa kwa usahihi. Matumizi ya kauli ‘machafuko ya kiraia’ hayakuwa sahihi, tunaomba radhi kwa kauli hiyo.
“Tishio maalum la ndani limetusukuma kufanya uamuzi huu. Hatuwezi kutoa maelezo zaidi kuhusu suala hili la usalama. Tulizingatia maoni yako na tumerekebisha ujumbe kwenye tovuti yetu.

“Tunashughulikia mchakato wa kuanzisha upya safari za ndege za Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar haraka iwezekanavyo. Hili linahitaji marekebisho ya kiutendaji ili kuwafanya wafanyakazi wetu kutua nje ya Dar es Salaam,"ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Ikumbukwe awali Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilieleza kusikitishwa na taarifa iliyotolewa na Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM) ya kuwepo kwa hali ya hatari nchini na kusitisha safari zake zilizopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam,Kilimanjaro na Zanzibar.

KLM kupitia taarifa waliyoitoa Januari 27,2023 katika tovuti yao walitahadharisha abiria wake na kueleza kusitisha safari katika viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Dar-es-Salaam (JNIA), Kilimanjaro (KIA) na Zanzibar.

Aidha, kupitia taarifa iliyotolewa Januari 28, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alikanusha taarifa hizo akisema hazina msingi wowote...Endelea;

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news