Kwa nini Waziri Dkt.Mabula anawanyooshea kidole watu hawa? Huku akiwaonya tena Dar

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amesema, wizara yake haiwezi kukubaliana na tabia za baadhi ya kampuni zinazorasimisha makazi kuchukua fedha za wananchi bila kutimiza wajibu wao.

"Miradi mingi ya urasimishaji imekwisha toka mwaka 2019, lakini mpaka leo wananchi wanapiga kelele ni jukumu la wakurugenzi pamoja na timu zenu kuhakikisha hili linakwenda mbele, hatuwezi kuvumilia baadhi ya makampuni kuchukua fedha za wananchi na kutofanya kazi bila kuchukuliwa hatua;

Mheshimiwa Dkt.Mabula ameyasema hayo Januari 6, 2023 jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kujadiliana kuhusu Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam.

Sambamba na ukwamuaji wa zoezi la urasimishaji ambalo linakwenda kwa kusuasua ili kutoka na maazimio ya uwajibikaji wa kila mmoja wao katika kutekeleza matakwa ya kisheria kwa sababu kumekuwa na hali ya kutegeana.

"Mnataka (kampuni) mpaka Mkuu wa Wilaya awakamate awaweke ndani? Kwa nini hutimizi wajibu wako, unasubiria mkuu wa wilaya afanye. Sasa hivi tunahamisha matatizo tunapeleka kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya hatuendi hivyo na hatuwezi kufanya kazi kwa mfumo huo.

"Lakini pia kutokuwepo kwa kumbukumbu sahihi za taarifa za urasimishaji na makusanyo ya pesa za wananchi katika mamlaka za upangaji kwa hiyo unaweza kukuta wananchi fedha walizotoa ni tofauti na fedha inayosomeka manispaa au halmashauri,"amefafanua Waziri Dkt.Mabula.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Dkt.Mabula alifafanua kuwa, wakati mwingine inashangaza kuona kampuni za upangaji na upimaji kuchukua kazi nyingi kuliko utendaji. "Mtu mmoja hawezi kufanya kazi zote nyingi, sehemu nyingi unakuta yuko na kazi nyingi.

"Baadhi ya makampuni kuchukua fedha taslimu kinyume na taratibu za uhamishaji wa fedha, maelezo ni kwamba hizi fedha zifunguliwe akaunti na haziwezi kutoka mpaka kujiridhisha na kazi inefanyika na hii inawaumiza sana wananchi.

"Lingine kulikuwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za upangaji na upimaji wa baadhi ya makampuni kufanya upimaji kwenye maeneo yaliyokwishapimwa na maeneo hatarishi hasa katika mabonde, vyanzo vya maji na kwenye hifadhi za miundombinu.

"Tayari kuna maeneo yalikuwa yamepimwa kama mashamba, lakini kwa sababu ya kukosekana coordination baina ya ofisi na yule mpima haikuwepo yule jamaa anaendelea kupima, jamaa anapima juu ya shamba."

Mashamba

"Naomba niseme kwa wale wenye mashamba pori mjini, kuna watu wana hati za mashamba, hatuzuii kwa sababu ni hati aliyokuwa nayo je? Kwenye lile shamba kuna chochote kinachofanyika? Je sheria ambazo zinaguide mashamba mjini amekidhi?.

"Kwa sababu anatakiwa awe na shamba lisilozidi hekari tatu, lakini shamba lenyewe sio kulima mahindi, unalima mazao yale ya chini ambayo usalama unakuwa mzuri zaidi. Sio unatulimia mahindi katikati ya mji, halafu jioni inakuwa vichaka vya vibaka.

"Kwa hiyo lazima nayo yazingatiwe, hatusemi mashamba mjini hayatakiwi, lakini kuna ukomo wa mashamba. Sasa kuna wale wengine ambao mashamba yao ni mapori, hayana kitu kabisa na wengine yamevamiwa kabisa.

"Sasa yale tulisema kisheria lazima tuone namna ya kuzungumza nao tuweze kubadilisha matumizi kwenye maeneo yale na ikiwezekana ndio hao ambao mashamba yao yamevamiwa, ndio tunafanya zoezi la kurasimisha yale ambayo Mkuu wa Mkoa anahangaika nao na wengine wanakiburi hawataki kutekeleza yale makubaliano."

Wavamizi

"Wewe ni mvanizi eneo ni la kiwanda, mwenye nalo alishindwa kujenga kiwanda, wewe umejenga pale amekushitaki ameshinda ana hukumu ya mahakama unatakiwa uondoke, lakini Serikali inayoongozwa na kiongozi makini, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inasema zungumzeni nao hawa muone.

"Lakini tumefika sehemu, tumezungumza nao, unayo document ya mahakama, hebu tuzungumze basi huyu mtu alishajenga hapa ukimbomolea hapa sio vizuri sana. Sasa unaambiwa ulipie tu pesa kidogo, labda square mita shilingi 8,000.

"Unasema hapana, maneno yanakuwa mengi Mkuu wa Mkoa akishasema umevamia eneo la mtu zingatia yale unayoelekezwa na Serikali huwezi kuzingatia yatakayokupata huna pa kukimbilia.

"Kwa hiyo tunawataka hao nao walitambue hilo na wajue Serikali inawapenda, inataka waishi kwa amani na ndio maana inapenda kufanya maridhiano na wale ambao walitakiwa wawaondoke.

"Naomba sana mkuu wa mkoa (Amos Makala) baraka zote za Serikali unazo na wewe pia ni Serikali, kwanza nishukuru sana kwa sababu tuna Mheshimiwa Rais ambaye ana hekima sana na busara, anakwambia hata kama mwananchi kavunja sheria, usifanye utatuzi wa jambo lile kwa taharuki, zungunza naye kwanza mweleze kosa lake ni nini na hata unapochukua maamuzi kama Serikali atakuelewa.

"Kuliko kwenda kwa nguvu pale na kelele nyingi, kina mama watabeba vitoto watalia...lakini maelekezo ni kwamba zungumza naye aelewe."

Kwa wanasiasa

"Nanyi wanasiasa zungumzeni nao, muwaambie ukweli, lakini hiyo haihalalishi kwamba watu waendelee kuvunja sheria, amri ya Mahakama ikishatoka kwenda kuvunja, lakini kwa busara ya kiongozi mkuu tuliyenaye Mkuu wa Mkoa, mkuu wa wilaya atazungunza naye aseme naye hicho kiwanja mbona sio kiwanja hebu tufanye namna nyingine kwa njia nzuri zaidi,"alifafanua kwa kina Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Halmashauri

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amezitaka halmashauri na manispaa kuhakikisha wanatoa kipaumbele kikubwa katika sekta ya ardhi ili iweze kuleta matokeo mazuri hususani katika upande wa mipango miji.

"Hauwezi ukatenga shilingi milioni 10 au 20 kwa mwaka ukategemea utafanya kazi na wala hatuwezi kutegemea fedha kidogo ambazo Mheshimiwa Rais anazitoa, sasa unakwenda kwenye halmashauri sekta ya uendelezaji unakuta shilingi milioni 10, hiyo ni OC ya watumishi wako.

"Na hata wanayopewa kwa ajili ya kuendeleza wanatumia kinyume. Kuna halmashauri zimepewa mikopo na wanauza viwanja. Lazima tuzingatie Sheria namba 8, jukumu hilo ni la wakurugenzi sio wizara. Wizara ni wasimamizi wa sera,tukiyatambua hayo tutafika mbali.

"Na sasa tutawekeana taratibu tujue mmeuza viwanja vingapi, mmefanya kazi gani kwa sababu Serikali tunafanya kazi as a team, kwa hiyo kuwa na TAMISEMI na Ardhi haiondoi dhamana ya mimi (Waziri Dkt.Mabula) kusimamia sekta yangu, kumekuwepo na baadhi ya Wakurugenzi wakiona Waziri mwingine wanasema huyo sio wa upande wangu.

"Bahati nzuri Adhi na TAMISEMI ni kama pete na kidole katika upangaji, sasa tukijua hilo ndio tutafanya kazi kama team.

"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa naomba sasa usimamie mpango huu ili fedha za serikali zilizotumika ziwe na tija. Na moja ya changamoto ni kukosekana kwa uratibu mzuri wa mojawapo wa sekta mbalinbali, aidha naelekeza iundwe timu ya wajumbe wako watokane na taasisi ambazo zinawajibika kutekeleza mradi mbalimbali iliyoainishwa kwenye Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam kwa sababu wadau lazima watokane na sekta mbalinbali."

"Nitoe rai kupitia Jiji la Dar es Salaam na kwa halmashauri zote zihakikishe zinaandaa mipango ya kina na hasa zile ambazo zina mpango kabambe na kutoa vibali vya ujenzi kulingana na mpango.

Ujenzi holela

"Wito wangu kwa wananchi ni kutofanya ujenzi wowote bila kuwa na vibali. Kuna staili moja mbaya wanawafuata wale mabibi waliochoka choka wanaomba vibali wakarabati zile nyumba badala ya kuchukua kibali ili ajenge kulingana na master plan, kwa sababu tayari imeshaidhinishwa anapewa kibali cha innovation...anazungushia mabati anaongea na mwenye nyumba anamwambia, mimi nitakuwekea maduka 10, fremu ambazo mnaziita tano za kwangu na tano za kwako, ukiangalia kwenye master plan lile ni eneo zuri la kuboresha mji wetu, labda ghorofa tatu. Nyumba inajengwa siku tatu imeisha."

"Nimshukuru sana Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza baada ya kuona wataalam wake wamemuingiza chaka alikwenda akavunja. Hatutaki kuvunja nyumba za watu, tunataka watu wazingatie sheria na taratibu, hapa kuna master plan lazima zifuatwe. Uendelezaji wa namna hiyo haufai, kamati za miji ziwajibike.

"Haiwezekani mtu anataka atoe kwenye makazi ajenge sijui baa, au nyumba ya biashara vitu kama hivyo tusiviruhusu hata kidogo...pia hatufanyi kazi kwa kuwasiliana, unakuta mtu anatoa kibali bila kufanya mawasiliano lazima kelele za viongozi zisikikie kukemea haya ili tiwe na lugha moja.

"Ni muhimu sasa kamati zisimamie na ushiriki wa sekta binafsi uwepo kwa ajili ya kuimarisha na mpaka hapa tulipo tulipata makampuni 166 yanajumuisha kampuni za upimaji ambazo hizi zitafanya kazi za upimaji na upangaji maeneo mbalimbali,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Kuoneshwa bikoni

"Na siku zote ninasema kuoneshwa bikoni moja, mbili au tatu ndio mwisho wa kiwanja chako sio, bado haisaidii kwa sababu kisheria bado inakuwa si mmiliki halali, lakini ukiwa na nyaraka itakusaidia.

"Sasa hivi viwanja ambavyo vipo kwenye upimaji wa awali ni vizuri kwa kila hamashauri na manispaa nchini ikavitambua na kuweza kukamilisha upimaji wake na kuweza kuwamilikisha wahusika.

"Kwa upande wa umilikishaji kupitia urasimishaji jumla ya ankara 475,915 sawa na asilimia 20 zilitolewa kwa wananchi kwa ajili ya kupata hati miliki.

"Lakini ni jumla ya hati miliki 17,7330 sawa na asilimia nane ndio zimeandaliwa, sasa hapo lazima tuangalie viwanja vilivyokamilika, vilivyomilikishwa vilivyotolewa ankara ni chungu nzima, lakini ni asilimia nane tu, kwanza kasi ni ndogo halafu udogo wake ule ule umilikishaji ndio uko chini zaidi, hapa lazima tujiulize kwa sababu wizara ilitoka kwenye shilingi 230,000 mpaka 300,000.

"Kwenye upimaji ikashusha hadi shilingi 130,000.Na ukiangalia kwenye umilikishaji kisheria yaani unaweza ukakata pesa wakati mwingine haizidi shilingi 100,000 hutegemeana na ukubwa wa eneo, matumizi na location.

"Ukija kuangalia, wenye maeneo makubwa ndio unaweza ukakuta ziko kubwa, lakini wenye maeneo madogo unaweza ukakuta gharama iko chini, lakini kwa sababu hawapati elimu sahihi, hawapati maelezo sahihi wanashindwa kufanya maamuzi ya kuchangamkia kumilikishwa.

Fedha

"Hadi kufikia Novemba 22, 2022 wizara imebaini kuwa jumla ya shilingi bilioni 70.2 zimekusanywa kutoka kwa wananchi kwa ajili ya kugharamia miradi ya urasimishaji katika halmashauri mbalimbali nchini na kiasi cha shilingi bilioni 68.9 kimetumika kufanya malipo kwa wakandarasi mbalimbali nchini, wengine wamelipwa na kazi wamekamilisha na tayari pesa imeshalipwa. Sasa ni jukumu letu kuhakikisha kwamba hayo yanazingatiwa.

"Kwa Dar es Salaam hapa Katibu (Katibu Mkuu Dkt.Allan Kijazi) amesema fedha shilingi bilioni 24.6 zimekusanywa, lakini katika hizo fedha katika zoezi la utekelezaji ambalo ni sawa na asilimia 35 ya kiasi hicho kilichokusanywa shilingi bilioni 24.6 zimetumika kulipa wakandarasi, lakini sio wote wamemaliza kazi zao, lakini tayari fedha wameshapewa.

"Katika hili Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa (Amos Makalla) wakurugenzi hawawezi kukwepa katika hili, yale makampuni yaliachwa wazungumze na kamati za mitaa, kamati za mitaa waliongea nazo wakaingia makubaliano. Halmashauri zinasema hawa waliletwa na wizara, naomba niseme hakuna kampuni iliyopelekwa na wizara kwenda kufanya kazi kule, wizara ilitoa orodha ya makampuni ambayo yamesajiliwa na yanatambulika.

"Unaingia na nani, unafanya kazi na nani ni wewe kufanya uchaguzi juu ya yale makampuni, halafu hukutakiwa wewe kama halmashauri umwachie mwananchi wa kawaida ambaye haelewi masuala ya mikataba, ukomo wa ile kampuni katika utendaji, unamuacha anasaini. Anachukua hela hizi shilingi bilioni 24 zimekwenda kwa sababu tuliwaachia kamati, kwa nini tuwaachie kamati na ninyi ndio mamlaka za upangaji.

"Mwananchi sijui wa mtaa wa wapi...Kivule anajua nini kuhusu masuala ya mikataba? Anamjuaje huyu mwenye kampuni ya upimaji au upangaji, tulitakiwa kama halmashauri tuijue hiyo mikataba wanavyokubaliana tuwasaidie wananchi wetu kutambua nini kinataka kufanyika katika maeneo yao ili wanapoingia makubaliano yanakuwa yanasimamiwa na halmashauri husika.

"Mwananchi atakusaidia kutambua watu wake ni nani, anamiliki wapi na nani anaishia wapi, wewe ukamsaidia mwenye kampuni kuhamasisha wananchi zoezi hili Serikali inalitambua, zoezi lile mwananchi anawajibika kulipia kwa sababu amekaa pale bila ridhaa ya mipango miji, lakini ni kosa la Mipango Miji kutopima viwanja mapema wakakuta viwanja vimepimwa."

Hatuwezi kubomoa

"Ana hela yake amepata anataka ajenge kiwanja chake akae anatafuta kiwanja kilichopimwa hakipo, kuliko apoteze ile pesa anaamua kujijengea, Serikali ikasena hatuwezi kuwabomolea kwa sababu ni kosa sio la kwao kosa ni la Serikali.
"Lakini kwa sababu kosa ni la Serikali kutopanga maeneo, basi tuwapange vizuri waweze kupata huduma za jamii huko walipo kama ni umeme, maji, na kadhalika lakini na wao lazima wakubali walijenga bila kibali hapa barabara ipite utamega kidogo na ndio ilikuwa shirikishi kwa namna hiyo.

"Sasa tunapoendelea na hiyo kwa sababu urasimishaji unakoma mwaka 2023 kuanzia 2013 ilikuwa miaka 10 tu. Kama wasimamizi wa upangaji maeneo hatutakiwi kuruhusu sasa ujenzi unaoendelea kwenye eneo ambalo lina master plan tunawarasimishia hawa ambao walituwahi, lakini asije mwingine akafikiri zoezi hili linaendelea linakoma mwaka huu.

Hakuna kujenga

"Kwa hiyo msiruhusu tena watu kujenga bila utaratibu na hili unaona mtu amejenga bila kibali, sheria ichukue mkondo wake na kama ni kubomolewa, ibomolewe hatutaki kuingia kwenye changamoto nyingine hivi kweli halmashauri mnakosa kuweka vijana walau sita au saba na vijana wengi kwa sasa hawana kazi, hata ukisema unampa posho ya shilingi 20,000 akufanyie kazi kila siku atafanya, kila kakichipuka kajumba tu ameshatoa taarifa kwa hiyo utamuwahi yule mtu kabla hajafika mbali.

"Unamuwahi kabla anasafisha kiwanja aanze kujenga, unamuuliza tu tuoneshe kibali chako cha ujenzi hana kibali unamwambia acha. Kama ataendelea na kiburi, leteni taarifa na mtamuokoa gharama zake badala ya kujenga nyumba ikamilike mtamsimamisha, akiwa hatua ya msingi kwa hiyo, hilo ni jukumu lenu kwa kila halmashauri.

"Hapatakuwa na zoezi la urasimishaji kwa wale ambao watakuwa wameachwa na hii programu na walitangulia kujenga wataingia kwenye programu zetu za kawaida za kupanga, kupima na kumilikisha, lakini hatutaki tena watu waendelee kufanya hivyo na hili ni jukumu lenu mtusaidie,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Post a Comment

0 Comments