Maagizo ya Rais Dkt.Samia yaongeza mvuto Daraja la Tanzanite

NA DIRAMAKINI

IKIWA imebaki siku moja kabla ya kufunguliwa kwa Daraja la Tanzanite linalokatiza kandokando ya Bahari ya Hindi jijini Dar e Salaam, hatimaye nembo ya madini hayo ya kipekee duniani imeonekana.

Tanzanite ni madini yenye mchanganyiko wa rangi ya bluu na zambarau. Madini haya ni ya kipekee kwa Tanzania, kwani hayana chanzo chochote duniani isipokuwa kile cha Mererani mkoani Manyara.

Awali Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam ilitangaza kulifunga Daraja la Tanzanite kwa siku nane kwa ajili ya maboresho ya kuwekwa nembo ya Tanzanite.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa Jumamosi ya Desemba 31,2022 na TANROADS mabayo ilieleza kuwa, daraja hilo litafungwa kuanzia Jumatatu Januari 2, 2023 saa 12 asubuhi na kufunguliwa Januari 9, saa 12 asubuhi.

“Katika muda wote wa maboresho hayo, daraja hili halitatumika kwa sababu za kiusalama, hivyo TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam inawashauri watumiaji wa daraja kutumia barabara ya Kaunda na Ali Hassan Mwinyi,”ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Maboresho ya daraja hilo ambalo awali lilikuwa na nembo ya Mwenge wa Uhuru yalikuja kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan alilolitoa Machi 2022 wakati akizindua daraja hilo na kuamuagiza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kubadilisha alama hiyo na kuweka alama ya madini ya Tanzanite kuendana na jina la daraja hilo.

“Niseme kidogo waziri ushauri nilioupata kutoka kwa wananchi, daraja hili tunaliita la Tanzanite, lakini alama tuliyoiweka ni alama ya Mwenge. Pamoja na kutambua Mwenge ni tunu yetu adhimu wananchi wangependa sana kuona alama ya Tanzanite pale ilipo alama ya Mwenge ili liendane na jina la daraja hili,"alisema Rais Dkt.Samia.

Hadi kukamilika kwa daraja hilo gharama za ujenzi ni takribani shilingi bilioni 243 ambazo zinatokana na Serikali na ufadhili wa Serikali ya Korea Kusini.

Aidha, Daraja la Tanzanite lilijengwa na kampuni ya ujenzi ya GS E&Cambapo lilianza kujengwa mwaka 2018 na kuzinduliwa mwaka 2022.

Urefu wa daraja hilo ni kilomita 1.03, ikijumuisha njia nne za magari na njia mbili za watembea kwa miguu, pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 5.2 na linaunganisha Hospitali ya Aga Khan na barabara za Obama, Kenyatta na Toures jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news