Mbowe asema hajalambishwa asali, awapa saluti askari polisi Mwanza

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mheshimiwa Freeman Mbowe amesema, hajalamba asali kama baadhi ya watu wanavyodai huku akisema amepoteza fedha nyingi kukipigania chama hicho na hawezi kuwasiliti wanachama kisa fedha au mali.

Mheshimiwa Mbowe ameyasema hayo leo Januari 21, 2021 akiwa katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza kwenye mkutano wa kwanza wa hadhara wa chama hicho tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Samia aliporuhusu mikutano ya vyama vya siasa kuendelea nchini

“Yaani mnaanza kusema eti Mbowe kalamba asali, hivi mnajua Mbowe nimepoteza bilioni ngapi kwa kuwa mwana CHADEMA? Mnakubali kutunza propaganda za kitoto kwamba eti Mbowe kalamba asali hataki Katiba Mpya, hataki tume huru so what?.

"Upande wa pili ninaweza kuelewa vilevile hisia za viongozi na wanachama wa CHADEMA kwa maumivu ambayo tumeyapitia kwa muda mrefu,”amesema Mheshimiwa Mbowe mbelea ya umati mkubwa wa wanachama wa chama hicho.

Mheshimiwa Mbowe ameendelea kufafanua kuwa, “Kwahiyo wakitoka wanachama wa CHADEMA wakahofu maamuzi ya Mwenyekiti binafsi nawaunga mkono, naelewa kwa sababu tumeumizwa sana.

"Ni asilimi mbili tu ya wanachama wa CHADEMA wanaiamini CCM, lakini mimi niliwaamini kwa kiwango fulani niliokuwa nazungumza nao,”ameongeza.

Pia Mbowe amesema, walipoanza mazungumzo walikubaliana misingi ikiwemo usiri,wanachama wa CHADEMA wakiwemo viongozi wenzake wakuu wakawa wanamnyooshea kidole.

"Wakasema Mbowe anafanya usiri hatuambii, yupo Ikulu kila siku, hii Mi-CCM sio ya kuiamini, kalamba asali, yaani kama kuna kitu kimewahi kuniumiza ni kuwepo kwa mtu anayeweza kuamini kwamba eti mimi naweza kulamba asali nikawasaliti watu ambao nimeteseka kwa miaka 30 kuwalinda.
“Nilisimama miaka 30 iliyopita kuitafuta haki, nitasimama hapo kwa gharama yoyote, hakuna idadi ya fedha au mali itakayonifanya Mbowe niwasaliti Watanzania, nimepoteza mabilioni ya fedha, anavyotokea mtu anamuhukumu Mbowe eti amelamba asali, asali ipi?, nimezaliwa kwenye familia yenye uwezo, nimekua na kusimama kwenye familia yenye uwezo, lakini nimesema nitasimama na haki kwenye maisha yangu,"amefafanua Mbowe.

Pongezi polisi

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mbowe amewapongeza maafisa wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa kusimamia usalama tangu kuanza kwa maandalizi hadi kufanyika kwa mkutano wa CHADEMA bila kuwakwaza viongozi na wanachama wa chama hicho.

“Naomba wana Mwanza kwa kauli moja muungane nami kulishukuru Jeshi la Polisi kwa namna ambavyo kuanzia tumeanza hii mikutano ya hadhara na maandalizi yake wamesimama na sisi kuhakikisha usalama upo, hawajatukwaza kwa hatua yoyote, wapigieni makofi polisi.

“Na polisi ndugu zangu, nyinyi ndugu zetu tambueni makofi haya ni makofi ya kulilia Taifa, haina maana kwamba CHADEMA leo tumekubaliana kwamba sisi ni wateja wa Serikali, lakini pale wenzetu wa upande wa pili wanapofanya jambo jema naomba wana CHADEMA kote nchi nzima tuwapongeze, hawa ni ndugu zetu,”ameongeza Mbowe.

Aidha, amefafanua kuwa,licha ya kufanyika kwa maridhiano bado CHADEMA itaendelea kuwa chama kikuu cha upinzani nchini hadi hapo kitakapofanikiwa kuwa chama tawala.

“Hatujaingia kwenye maridhiano kwa kukiua chama kimoja. Chama hiki (CHADEMA), mimi ninaweza kusema nilikuwa miongoni mwa waliokiasisi chama chetu nikiwa kijana mdogo wa miaka 29, kwa hiyo hiki chama ninakifahamu kuliko wengi wanavyoweza kufikiria.

"Maisha yangu kwa miaka 30 nimetumia fedha, rasilimali na nguvu zangu kukijenga chama hikii nikijua taasisi hii ina malengo mazuri kwa nchi yangu na sio malengo mazuri kwa familia yangu. Tumepitia milima na madimbwi mengi, leo nikisema tuna miaka 30 nazungumza kwa imani na ujasiri, tumepigana kuijenga CHADEMA,leo hakuna chama cha kushindana na CHADEMA,”amebainisha Mbowe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news