Mheshimiwa Sagini:Viongozi tuwashirikishe wananchi utekelezaji wa miradi

NA DIRAMAKINI

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Butiama mkoani Mara, Mheshimiwa Jumanne Sagini amewataka viongozi wa Kijiji cha Nyabange wilayani humo kushirikiana na wananchi wao kukamilisha ujenzi wa vyumba sita vya madarasa na matundu ya vyoo ili shule hiyo mpya iweze kupata usajili na kuanza kupokea wanafunzi.
Ambapo hatua hiyo itawasaidia wanafunzi kuondokana na tatizo la kutembea umbali mrefu kwenda kufuata huduma ya shule.

Akizungumza mara baada ya kukagua shughuli za ujenzi zinazoendelea shuleni hapo, Sagini amesema kuwa siri kubwa inayopelekea miradi kuweza kufanikiwa na kukamilika kwa wakati ni viongozi kuhakikisha wanawashirikisha wananchi na kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu hatua zinazofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo kwa kuwa na uelewa wa pamoja na wananchi kuweza kuwa na umiliki wa miradi.
“Kazi mnayoifanya ni kwa niaba ya Wananchi. Sisi tumekabidhiwa haki ya kusimamia hivyo inatupasa tutoe taarifa kwa wananchi waliotutuma. Ukiimarisha mawasiliano endelevu kati ya unaowaongoza na viongozi unajenga uaminifu. Huwezi kuwaita kesho wakakuangusha lazima watakuunga mkono. Ukiwakwepa wananchi na ukajimilikisha mradi wewe kiongozi ni tatizo kubwa,”amesema Mheshimiwa Sagini.
Sagini ameendelea kuwasihi wananchi kushiriki katika kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwani maendeleo hayana chama na badala yake kutumia nafasi hiyo kutafakari na kuwahurumia watoto ambao wanatembea zaidi ya kilomita nane mpaka 12 kufuata huduma ya shule jambo ambalo linapelekea idadi ya Wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne kuwa ndogo ukilinganisha na idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa.

Pia, ni sababu kubwa ya kutowafanya wanafunzi wengi kutomaliza masomo yao ya kidato cha nne na kufanya vizuri ikichangiwa na umbali wa shule.
Katika hatua nyingine, Sagini ametembelea katika Shule ya Msingi Mkiringo iliyopo wilayani humo na kujionea uharibifu uliofanywa kutokana na upepo mkali na mvua ambapo katika shule hiyo vyumba vitatu vya madarasa viliezuliwa paa.
Mheshimiwa Sagini ameutaka uongozi wa kijiji hicho kuchukua hatua za haraka kwa kufanya mkutano na wananchi na kuona ni kwa namna gani wanashiriki katika kufanya marekebisho hayo ili shule zinapofunguliwa wanafunzi wapate vyumba vya kusomea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news