Mradi wa NHC Morocco Square waivutia KingJada Hotels, wasaini mkataba wa upangishwaji na uwekezaji

NA GODFREY NNKO

UONGOZI wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na KingJada Hotels and Apartment Ltd wamesaini mkataba wa kihistoria kwa ajili ya upangishwaji na uwekezaji wa ubia kwa ajili ya huduma ya hoteli katika Mradi wa NHC Morocco Square jijini Dar es Salaam.

Awali kwa mujibu wa Meneja Mradi wa NHC Morocco Square,Samuel Metili amebainisha kuwa, mradi huo una ukubwa wa mita za mraba 110,000 kwa ghorofa zote ambazo zinajumuisha ofisi,makazi, biashara na hoteli.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Nehemia Mchechu amesema kuwa, mkataba huo wa Januari 27, 2023 baina ya shirika na mwekezaji huyo una tija kubwa na fursa nyingi za ajira ikiwemo kutunisha pato la Taifa.

"Tunamshukuru Mungu sana kwa hatua hii muhimu ya leo, kitu cha kwanza jengo linaonekana na tunasema una physical property, physical ownership na upande wa pili unazungumzia business on that property kwa maana ya biashara katika eneo hilo.

"Hapa unazungumzia physical property, biashara na revenue kwa hiyo leo inatupa ukamilifu kwa uwekezaji kwamba ukifanya uwekezaji na ukakosa watu wa kuja kupanga au watu wa kununua hujafanya uwekezaji, unaweza kuwa umefanya kazi ya kujenga, lakini sio uwekezaji.

"Pili tulichokuwa tunakifikiria kinaweza kuleta utimilifu kwa sababu ni jambo moja kufikiria, na ni jambo lingine kuanza kutekeleza yale mawazo, vivyo hivyo ni jambo lingine kabisa yale mawazo kutimia katika maono ya mwanzo.

"Wanapokuja watu wakaweka hela zao, wakapanga na tukaingia makubaliano wakaweka uwekezaji wao linakuwa ni jambo la kushukuru sana. Lakini niseme hii safari ya ujenzi wa Morocco Square tulivyopanga tutakuwa na majengo mengi tunayojenga, lakini aina ya ujenzi wa Morocco huu ni wa kwanza ambao tulianza nao.
"Labda kwa kuchelewa kukamilika kwa mradi wa Morocco imefanya tuchelewe kuanza majenzi mengine ya namna hii, lakini tulianza kwa kujiuliza mara mbili, wote tunatembea nchi za nje ukienda huko unaenda hotelini, unaenda shopping, unaenda kwenye ofisi huna sababu ya kukaa mbali, unakaa kwenye apartments ambazo ziko karibu, baadaye unaenda kupata chakula hapo hapo. Ni kwa nini hatuwezi kuiga hizo na ndiyo kisa cha kusema tufanye hivyo."

Awali, mradi wa Morocco Square ulisimama kwa miaka kadhaa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ile ya kifedha na mabadiliko ya baadhi ya maboresho kwenye maeneo ya majengo.

Kwa nini Morocco Square

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Nehemia Mchechu amesema kuwa, Morocco walichagua kutekeleza mradi huo kutokana na eneo hilo kukaa kimkakati katika biashara.

Pia amesema eneo hilo ambalo lipo katika Mkoa wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Kinondoni jijini Dar es Salaam ni kitovu cha jiji hilo la kibiashara nchini.

"Na tulichagua Morocco kwa makusudi kabisa, kwamba tuanzie hapa kwa sababu ukiniuliza mimi ninaiona Morocco ni senta ya Dar es Salaam kutoka Morocco ni kilomita hazizidi tano kwenda Masaki na Oysterbay hazizidi kilomita tano mpaka sita kwenda Mjini Kati.

"Vivyo hivyo, kilomita nne mpaka Magomeni, kilomita tano au 4.5 hadi Mwenge ndio Dar es Salaam hiyo, na ni kama kilomita 7 kwenda Mlimani City kama unatokea Mbezi ni kilomita 7, kwa hiyo naiona ndio senta, lakini pia tulikuwa tunaangalia maunganiko ya miundombinu hata mtu wa Kimara anaweza kuja kwa usafiri ulio rahisi zaidi, anakuja BRT anashukia hapo,"amefafanua Mchechu.

BRT ni nini?

Huu ni mfumo wa usafiri wa haraka wa mabasi ulioanza kufanya kazi miaka kadhaa jijini Dar es Salaam ambao umeonekana kuleta nafuu kubwa zaidi katika sekta ya usafirishaji jijini humo.

Mfumo huo unasimamiwa na Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ambayo ni taasisi ya serikali iliyoundwa kwa mujibu wa tangazo la serikali No. 120 la Mei 25,2007 chini ya sheria No. 30 ya Wakala za Serikali ya mwaka 1997 na marekebisho yake.

Mchechu tena

"Na tutakuwa na mazungumzo na wenzetu wa TANROADS (Wakala wa Barabara nchini) na tunajua wana mradi wao mkubwa wa kufanya fly over katika lile eneo na michoro inaendelea na ndani ya michoro yao wanakuja ku-intergrate movement ya kuja Morocco ili watu wasipite chini.
"Lakini tulikuwa tumekubaliana nao ni kwamba kabla ya huo mradi wao mkubwa haujafanyika hebu tufanye pamoja tupate suluhisho na tunakubaliana na nafikiri watu wetu wa technical kwa upande wa NHC na TANROADS nafikiri baadaye tutakuwa na mazungumzo ili tuone mtu akifika kule kwenye BRT anawezaje kuvuka kwa urahisi kuja kushoto kwa sababu ni sehemu ambayo itakuwa inatembelewa na watu wengi kwa sababu ya complex layer,"amefafanua Mchechu.

Pia amebainisha kuwa, KingJada Hotels wamefanya chaguo sahihi kuwekeza huduma zao katika mradi huo kwani, licha ya ubora wake na kufikika kwa urahisi pia kuna matarajio makubwa ya kupata wateja wa kutosha kutoka ndani na nje ya nchi.

"Hapa kuna nyumba za makazi 100, ambao ni watu wengi, makazi haya tuliyalenga kwa watu wa kati na juu kwa sababu tunafikiri aidha wapangaji au watumiaji wengi watakuwa wenye kuhitaji huduma za maofisi, kwa hiyo hata mkiona bei wakati mwingine mnasema Mchechu bei hizi ni Tanzania gani? Ni vizuri nikasema kwamba tulilenga makazi haya kwa watu wa vipato vya kati kwenda juu.

"Ndio maana hapa kuna apartment inauzwa shilingi milioni 900, sasa nani ataweza shilingi milioni 900 by the way zilishakwisha, kwa hiyo kuna kundi tulikuwa tumelilenga na hilo kundi lipo na siyo hewa na tayari limeshanunua apartment zake kwa hiyo ndio ilikuwa lengo.

"Lakini tunalenga kabisa wawekezaji ambao wanataka hiyo convenience na sisi tunasema wakienda kwenye nchi nyingine wanapata hiyo convenience ukiacha makazi kuna shoppings ambazo tumeambiwa ni square mita zaidi ya 17,000. Ambayo ni ya maghorofa matatu na niseme pia tunamshukuru Mungu mawazo tunayaweka na mawazo hayo yanakuwa kweli.

"Kwa hiyo wapangaji wameshajaa, target yetu sasa hivi kwa sababu imefika sehemu watu tumewaambia wapunguze maeneo ambayo walikuwa wameyakodi ili wawepo wapangaji wengine na wamekubali.

"Unapofika sehemu unamwambia mtu apunguze space wewe unatakiwa upambane kuongeza space na ma-ontractors wameshamaliza shughuli yote, nafikiri kutakuwa na phase two ndogo ya kufanya expansion for little space na tutai-expand tukielekea upande wa chini kwa sababu hapo mbele kuna viwanja vyetu ambavyo sasa tutavibomoa na ku-expand hiyo little space.

"Mungu akituwezesha jinsi anavyotuwezesha inawezekana chain hii mpaka ile njia ya Migombani Street ikawa ni proper little space ya Morocco inakuwa ni extension ya Morocco ambayo ina maduka ya kutosha ambapo tukienda tunapata mahitaji yetu.

"Ndio transformation ambayo tunataka kuiona ukiacha little space, kuna ofisi sasa katika ofisi mojawapo hapa itakuwa ni Dar es Salaam Exchange Tower, ukienda nchi nyingine zote kama South Africa wanayo, sasa kwetu hapa tunajiuliza where is our exchange tower, hatukuwahi kuwa na facilitates zinazoendana na uchumi wetu kama ambavyo leo tunatakiwa tufanye juhudi tuwe na facilitates zitakazoendana na uchumi wa kesho wa Tanzania.

"Uchumi wa kesho wa Tanzania ni energy, gesi, mining na vitu kama hivyo, kwa hiyo lazima tuimarishe katika hizi ofisi mbili, lazima kutakuwa na exchange tower.

"Kwa hiyo tuna wanunuzi na wapangaji, kwenye eneo la ofisi huko bado ofisi ziko na kama kuna mtu anahitaji kununua maeneo yapo na kuna blocks nyingine ipo kwa ajili ya watu kuja kupanga."

Kuhusu hatua hii

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Nehemia Mchechu amesema kuwa, "La pili ni hili ambalo limetukusanya leo ambalo ni sehemu ya hoteli, kwa sababu hiyo ndio inaenda kukamilisha seti yetu ya matumizi ya malazi, makazi,ofisi na matumizi ya maduka makubwa ya kisasa.

"Na matumizi ya hoteli, sasa jambo hili lilikuwa ni muhimu sana kwani, linahitaji mwekezaji mmoja ambaye atawekeza. Sasa kuwekeza hoteli inatakiwa ufanyie na furnitures equipments na kila kitu equipments za jikoni.

"Sisi NHC tuna-deal na real estate ndio maana hatumuiti KingJada Hotels mpangaji, tunamuita mwekezaji kwa sababu huyo mwekezaji ndiye atakayekwenda kufanya hayo mambo maana jengo kuwa ni hoteli ni jambo moja na hoteli ni jambo jingine na nina imani kabisa vijana watashirikiana na hoteli itaanza kwa kasi sana.
"Kwa hiyo, King Jada ninawaona mkipanuka Tanzania nzima iwapo mtatoa huduma nzuri, ninasema KingJada wanaanza sehemu nzuri kinachohitajika ni mwingiliano mkubwa wa watu, na tunategemea idadi kubwa ya mwingiliano wa watu katika mradi huu

"Tunakadiria kwa siku mradi huu utahudumia watu zaidi ya 10,000. Ukiondoa Kariakoo na Kariakoo ni sehemu na Morocco ni jengo, Kariakoo ambayo ni sehemu huna jengo la kuweza kuingiza watu 5,000 kwa siku jijini Dar es Salaam, lakini Morocco Square uwekezaji huu utakuwa na watu takribani 10,000.

"Kuna makazi hapa na makadirio kila mmoja katika familia wapo watu watano au sita kwa hiyo hapa ni watu 500 au 600, tuna nafasi za ofisi, tunazungumzia mita za mraba 57,000.

"Tunasema una avarage square mita ambayo una area ambayo iko allocated for corridors, una area ambayo iko allocated for sitting rooms, lakini in terms of real estate distributions tunasema square mita 10 ni mtu mmoja. Kama tuna square mita 57,000. Hebu gawanya kwa 10 maana yake tuna watu 5,700. Na wale 600 kule maana yake tunazungumza watu 6300.

"Tuna watu wanaoingia na kutoka kama tunavyoenda Mlimani City. Sasa hao tukadirie kadirio la chini tuseme watu 3,000. ingawa watazidi maana yake tunazungumzia watu 9,600. Sasa hao nimekuachia watu wanaokuja kwenye movies kwa hiyo nimesema ni sehemu ambayo kuna traffic ya watu avarage 10,000 kwa siku.

"Hakuna jengo Tanzania ambalo liko limebuniwa kwa hiyo attraction ya watu 10,000. Kwa hiyo ni sehemu sahihi ya kufanya uwekezaji na ni sehemu sahihi kwenu Kinga Jada, nafikiri mafanikio ya hapa yatatusukuma kwenda kuangalia maeneo gani mengine ya kufanya uendelezaji wa majengo mchanganyiko."

"Kuna sehemu nyingi ambazo tunapanga kufanya uendelezaji huo. Mimi matamanio yangu ni kuona Morocco ikisimama na nafikiri sana Pasaka hii na Idi ijayo hii Morocco iwe imefunguliwa, hoteli iwe na activity na ninaamini tutakuwa tumewaruhusu wapangaji waweze kutumia nyumba zao na wenye ofisi wawe wanatumia ofisi zao.

"Wenye sehemu za shopping malls tumewaomba sana waanze kufanya fittings kwenye maeneo yao kilichokuwa kimechelewesha ni vioo kwa sababu ya usambazaji, nafikiri tunakwenda vizuri,"amefafanu kwa kina Mchechu.

Wakati huo huo,Mchechu amesema Watanzania wanapaswa kuendelea kulifahamu shirika lao na kazi zake kwa uwazi na ukaribu zaidi.

"Na niseme tunakwenda mbali zaidi kwa sababu Serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inatuunga mkono sana, maono yake ni kuona NHC inabadilisha uchumi wa nchi, na maelezo yake yake yapo straight kwetu tumeyaelewa na ndio maana tunasema tunakwenda kwa kasi na tuna wazimu wa kufanya kazi,"amefafanua Mchechu.

Pia Mchechu amewashukuru wadau mbalimbali wanaoshirikiana nao katika mradi huo ambao akiwemo King Jada Hotels & Apartments Ltd,mkandarasi wa mradi huu, wanunuzi wa nyumba na ofisi za mradi huo, wapangaji wa maeneo ya biashara ya mradi huo, wabia wa taasisi za fedha, na timu ya NHC kwa jitihada zao ambazo zimewezesha matokeo chanya katika mradi huo mkubwa nchini.

King Jada Hotels

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa KingJada Hotels & Apartments Ltd ambaye ni Mkurugenzi wa Swastik Trading Ltd yenye makazi yake jijini Mwanza, Congo, Dubai na India akiwa pia ni mmiliki wa Pharmacy Retail Chain, Sanjay Madanraj Shah amesema,anatarajia uwekezaji wa hoteli hiyo nchini Tanzania utaleta matokeo bora katika kufungua fursa za ajira na kuchangia pato la Taifa.

Mbali na Shah, wakurugenzi wengine wa hoteli hiyo ni Nyangeta Mwaulanga ambaye ni mbobezi na mtaalam wa usimamizi wa biashara akiwa na uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa hoteli za nyota tano ndani na nje ya nchi.

Pia yupo Mkurugenzi mwingine, Pradveen Toshniwal ambaye ni mbobezi na mwenye uzoefu mkubwa katika uhasibu na mshauri wa biashara.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa hoteli hiyo,Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano KingJada Hotels & Apartments Ltd, Morocco Square jijini Dar es Salaam,Risasi Mwaulanga amesema,dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa wawekezaji ndiyo iliyowavutia kuwekeza katika hoteli hiyo.

"Ninapenda kupongeza kazi kubwa zilizofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye yeye na wateule wake katika sekta mbalimbali imetufanya wawekezaji kujenga imani kubwa katika suala zima la uwekezaji kwa kutujengea mazingira ya kiuwekezaji na kutoa fursa ya majadiliano.

"Narudia tena, Serikali imetoa mijadala mipana na ya uwazi jinsi gani tuendeshe uchumi wetu na jinsi gani tufanye uwekezaji usio na mashaka na jinsi gani wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza na kuamini kwamba Tanzania ni sehemu salama.

"Sanjay Madanraj Shah ameonesha imani na kwa imani hiyo anatarajia kufanya uwekezaji wa Tanzania peke yake unaokadiria kufikia dola milioni 60,"amefafanua.

"Kwa niaba ya KingJada Hotels and Apartment Ltd inayoheshima na furaha kusimama mbele yenu leo Januari 27, 2023, sisi kwa pamoja na NHC kutekeleza hatua muhimu ya utiaji saini wa upangishwaji na uwekezaji wa ubia kati yetu na shirika hili kubwa kabisa la kizalendo.
"Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) chini ya uongozi mahiri wa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu ndugu Nehemia Mchechu, kiongozi mwenye dira ya kimageuzi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu kwa kuwa na dira sahihi katika kuleta maendeleo katika nchi yetu kwa uendelezaji makazi kwa watanzania.

"Lakini kuwa na fikra pana ya uendelezaji wa majengo yanayokidhi uwekezaji mkubwa na wa kati unaoendana na uwekezaji wa kisasa katika soko shindani nchini na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano KingJada Hotels & Apartments Ltd, Morocco Square jijini Dar es Salaam,Risasi Mwaulanga.

Wakati huo huo, amesema KingJada Hotels & Apartments Ltd, Morocco Square jijini Dar es Salaam ikianza kutoa huduma inatarajia kutoa fursa mbalimbali za ajira za moja kwa moja na zile zisizo za moja kwa moja kila siku huku huduma bora zikiwa ni kipaumbele chao.

"Hayo ndiyo matarajio yetu, kwani tunaamini kutanuka Tanzania nzima na Afrika Mashariki, natanguliza shukrani nyingi za dhati kwa menejimenti nzima ya Shirika la Nyumba la Taifa, kwa nyumba salama kwa Mtanzania na asiyekuwa Mtanzania, atakaye weka makazi Tanzania katika masuala ya makazi na uwekezaji. Narudia tena National Housing Corporation is a good corporation iwapo na sisi tuta-corparate kwa dhamira na dira yao njema kwa taifa letu,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mawasiliano KingJada Hotels.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news