Mwinjilisti Temba:Rais Dkt.Samia katuheshimisha kupitia Royal Tour, tena amepandisha intaneti Kilimanjaro matunda yatakuwa mengi

NA DIRAMAKINI

MWINJILISTI wa Kimataifa na Kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, ndugu Alphonce Temba amesema jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuitangaza Tanzania kupitia filamu ya Royal Tour zina matokeo chanya katika sekta mbalimbali ikiwemo uwekezaji na utalii nchini.

"Nataka niwaambie Watanzania hasa sisi tunaotoka Mkoa wa Kilimanjaro. Kwa Mara ya kwanza tumepata Mkongo wa Taifa umefika mpaka juu Mlima Kilimanjaro.
"Kinachoendelea sasa hivi watalii wengi wanaokuja nchini wanapiga picha tu. Wa Marekani, Italy, Australia, Uingereza yaani Wazungu wanatumia gharama kupiga picha kuonesha mlima Kilimanjaro kwa ndugu zao huko Ulaya haya yote ni matokeo ya Royal Tour ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hasaan.

"Haikuwa hasara kwa Rais kuitangaza nchi yetu kupitia filamu hiyo imekuwa ni faida kubwa sana. Wazungu wanatumia gharama zao kumsapoti Mama (Rais Samia), Mama yuko vizuri sana.Ninaamini kabisa utalii utakuwa kwa kasi mkubwa sana nchini, yaani utaongezeka,"amefafanua Mwinjilisti Temba.

Mwishoni mwa mwaka jana Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) lilifanikiwa kufikisha huduma za mawasiliano ya intaneti kwenye Kilele cha Mlima Kilimanjaro, ikiwa ni juhudi za kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kutangaza vivutio vya utalii nchini.

Akizungumza katika hafla ya awali kuelekea uzinduzi wa mawasiliano ya Data Katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro uliofanyika Makao Makuu ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye aliipongeza TTCL kufanikisha mradi huo wa kuweka mawasiliano katika Mlima Kilimanjaro.

Alisema, kukamilika kwa mradi huo kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kusimika huduma za mawasiliano katika kilele cha Mlima kilimanjaro, jambo ambalo litaongeza kasi ya kuutangaza mlima huo duniani na kuvutia idadi kubwa ya watalii kuutembelea.

Jumla ya kilometa 44.7 za njia ya Mkongo wa Mawasiliano zimejengwa kuanzia Kituo cha Marangu hadi kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, uwekezaji ambao umefanikisha vituo vyote vilivyopo katika Mlima Kilimanjaro kupata mawasiliano ya intaneti na simu za mezani.

"Tangu kuzinduliwa kwa huduma za mawasiliano katika vituo vya awali, watalii wanaopanda mlimani wameanza kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki wakiwa mlimani na kuelezea uzuri wa vivutio vyetu jambo ambalo linaendelea kuutangaza utalii nchini, licha ya kurahisisha shughuli za huduma kwa watalii zinazofanywa na taasisi mbalimbali katika Mlima Kilimanjaro," alisisitiza Waziri Nnauye.

Wakati huo huo, Mwinjilisti Temba ameiomba Serikali, iangalie vizuri mapato ya ndani ili yaweze kufanya shughuli za maendeleo kwa ustawi bora wa Taifa na jamii ya Watanzania.

"Usifanyike mchezo wa kuchezea mapato hayo. Mama kafanya kazi yake nzuri sana na sisi tumuunge mkono kwa hakika Mama anaupiga mwingi sana.

"Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amefanya kazi kubwa sana, tangu Uhuru haijawahi kutokea juu ya mlima Kilimanjaro kukawa na intaneti. Hakuna mtu aliyekuwa na maono hayo isipokuwa Awamu ya Sita chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan na imewezekana.

"Sasa hivi Wazungu wanafanya kazi kubwa sana ya kutangaza vivutio vya utalii nchini. Kwa hiyo Royal Tour inafanya kazi vilivyo, tuendelee kuwakirimu vilivyo ili waendelee kuitangaza nchi yetu.

"Na, tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, mama yuko vizuri. Hongera sana Rais wetu, kazi yako ni njema sana, tuko nyuma yako na tunaendelea kukuunga mkono na kukuombea kwa Mungu aendelee kukupa uzima tele uweze kuwatumikia Watanzania kwa bidii,"amefafanua Mwinjilisti Temba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news