Nabii Dkt.David Owuor kufanya mkutano wa kihistoria Tanzania, mfahamu kwa kina nabii huyu

NA GODFREY NNKO

NABII wa Kimataifa wa Huduma ya Repentance and Holiness, Dkt.David Owuor anatarajia kufanya mkutano mkubwa wa injili ikiwemo semina kwa ajili ya watumishi wote Mungu nchini Tanzania.

Dkt.Owuor ni miongoni mwa manabii wachache wa karne hii ambao wamekuwa na maono ya kipekee katika kulieneza neno la Mungu kupitia misingi mitatu ambayo ni toba,utakatifu na kuliandaa kanisa kwa ajili ya kurudi kwa Yesu Kristo.

Hayo yamebainishwa na Mratibu Mkuu wa Mkutano huo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Makanisha ya City of Glory Church International Tanzania, Dkt.Peter Rashid Abubakar.

Amesema,Dkt.Owuor ambaye ratiba yake itaanzia nchini Ivory Coast mwezi Machi,Afrika Kusini mwezi Mei,Burundi mwezi Julai na ataingia Tanzania mwezi Septemba kabla ya kuelekea nchini India mwezi Novemba na baadaye mwezi Desemba nchini Kenya.

Dkt.Abubakar amefafanua kuwa, Nabii Dkt.David Owuor ni mtumishi mkuu wa Mungu ambaye amekuwa akifanya mikutano mikubwa ya injili katika mataifa mbalimbali duniani na pia amekuwa akifanya semina za watumishi wote wa Mungu.

"Mwaka jana tulibahatika kupata mwaliko, tuliondoka Tanzania watumishi wanne kwenda Kenya kwenye mkutano alioufanya, Nabii Dkt.David Owuoor siku mbili pale Menengai Grounds huko Nakuru.

"Na pia, semina ya watumishi alifanya siku mbili, kweli Mungu anamtumia kwa viwango vikubwa sana na kwa sababu hiyo tukapata neema Tanzania mwezi wa tisa mwaka huu wa 2023 atakuja kufanya mkutano wa injili na pia atafanya semina kwa ajili ya watumishi wote, Mungu amempa neema hiyo.

"Kwa sababu hiyo, mwezi wa tisa tunatarajia kupokea karibu mataifa 60. Kama ilivyokuwa Kenya tulikutana na mataifa mbalimbali wa kutoka Israel walikuwepo, Italy, Uingereza,Marekani, Canada, Australia, Ivory Cost, Namibia Afrika Kusini na kwingineko. Kwa ujumla,kila nchi tulikutana pale na Mungu amempa neema ya ajabu sana,"amefafanua Askofu Dkt.Abubakar.

Amesema, kamati ya maandalizi inaundwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Mwenyekiti Askofu Dkt.Peter Konki,Makamu Mwenyekiti, Dkt.David Mwasota, Katibu Mkuu Askofu Dkt.Emmanuel Mbangwile na yeye Dkt.Peter Rashid Abubakar ni mratibu mkuu.

"Mimi nikiwa na watumishi wenzangu tuliambatana na Askofu Peter Konki ambaye ni Mwenyekiti wa CPCT na Askofu Dkt.David Mwasota ambaye pia ni Katibu msataafu wa CPCT na Askofu Emmanuel Mbagwile pamoja katika mkutano huo tuliona Mungu akifanya mambo makubwa sana.

"Nabii Dkt.David Owuor huwa anaongozwa na jumbe zake tatu tu, jambo la kwanza ni toba. Mtumishi huyo wa Mungu, Mungu amempa neema ya kusimamia toba na kuliambia taifa lolote anapokwenda watubu huo ni ujumbe wake wa kwanza.

"Ujumbe wa pili anazungunza kuhusu utakatifu baada ya kutubu, Kanisa liishi na utakatifu litembee na utakatifu huo, hivyo huo ni ujumbe namba mbili.

"Na ujumbe wa tatu,Dkt.David Owuor analiandaa kanisa kurudi kwa Yesu na ni Mungu tu anamtumia kwa viwango vikubwa sana. Kwa sababu hiyo tunatarajia kupokea wageni wengi sana mwezi wa tisa. Tulivyozungumza nao kwa mfano Kenya yanaweza kuja mabasi 10 yenye watumishi mbalimbali na mataifa mbalimbali watakuja,"amefafanua Askofu Dkt.Abubakar.

Katika hatua nyingine, Askofu Dkt.Abubakar amewaomba watumishi wa Mungu hapa nchini kuendelea kuombea mwezi wa tisa na kuwajulisha wengine ili wakati huo ukifika waweze kuwapokea wageni hao kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania kupitia injili na neno la Mungu.

"Ninajaribu kuwaza Kenya alichukua hekari 110, zote walikuwa wamefurika watu. Kwa wingi huo, unaona jinsi ambavyo Mungu amempa neema, Dkt.David Owuor kuhudumia maelfu kwa maelfu ya watu.

"Katika mkutano huo maelfu waliohudhuria viwete walitembea na vipofu waliona sio wa kutengeneza yaani unaona kabisa vipofu wanaona viwete yaani miguu yake imejikunja na miembamba, lakini anatembea si zile za kutengeneza yaani original kabisa. Tunatarajia zaidi ya watu 100,000 katika kusanyiko moja, yaani Tanzania yote kwa Yesu,"amesema Askofu Dkt.Abubakar.

Nabii Dkt.David Owuor ni nani?

Yeye ni mmoja wa manabii maarufu ndani na nje ya Kenya na mwanzilishi wa Repentance and Holiness Ministry. Nabii huyo anajulikana zaidi kwa ujumbe wake wa toba.

Nabii Dkt.David Owuor alizaliwa mwaka 1966, huko Ochieng katika Kijiji cha Goma, Usenge Wilaya ya Bondo, katika familia ya wasichana sita na wavulana watatu, na alikuwa mtoto wa pili wa familia hiyo.

Alizaliwa katika nyumba ya Kikristo ambako alimjua Mungu kupitia mama yake. Jina la baba yake David ni Bw. Hezekia, huku jina la mama yake mzazi ni Bi. Margaret.

Nabii Dkt.David Owuor alisoma Shule ya Msingi ya Wambasa, Yimbo, lakini ikabidi ahamie Jusa, Luzira, na baadaye, Kitalya, kutokana na kazi ya baba yake, ambaye alikuwa mtumishi wa umma. Aliendelea na Shule ya Sekondari ya Mbale na St.Peters College huko Tororo, kwa vyeti vyake vya "O" na "A".

Alipata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere jijini Kampala kwa Shahada ya Kwanza ya Sayansi, lakini aliacha chuo hicho kutokana na machafuko nchini Uganda kipindi hicho na kuhamia Chuo Kikuu cha Nairobi, ambako alikamilisha shahada yake ya kwanza ya sayansi mwaka 1988.

Baada ya kumaliza shahada ya kwanza, alichukua Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Vinasaba Chuo Kikuu cha Nairobi. Akiwa mmoja wa wanafunzi bora chuoni hapo, alipata ufadhili maeneo mawili kwenda Ujerumani au Israel.
 
Nabii Dkt.David alichagua kwenda Israel katika Chuo Kikuu cha Ben Gurion, alibadilisha programu yake kutoka kwa vinasaba vya mimea hadi vinasaba vya biokemikali.

Alipohitimu masomo, alirejea nchini Kenya kwa muda mfupi na kufanya kazi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP) kama mfanyakazi wa kujitolea.

Nabii huyo alirudi Israel tena mwaka 1994 kwa kusomea udaktari wa jenetiki ya biokemikali katika Chuo Kikuu cha Haifa, ambapo alibobea katika mpangilio wa vinasaba.

Baada ya kukamilika, alikwenda katika Chuo Kikuu cha Chicago,Idara ya Dawa na Bioteknolojia nchini Marekani kwa majukumu ya sayansi ya vinasaba kisha akahamia Chuo Kikuu cha Tiba na Meno huko New Jersey, ambapo alifundisha na kufanya utafiti.

Nabii Dkt.David amewahi kukaririwa akisema kuwa, alijiunga na Taasisi ya Saratani kama mtaalamu na alijikita zaidi katika kutafiti chanzo cha uvimbe na jinsi unavyokua. Alifanya kazi katika kituo hicho hadi mwaka 2003 alipoondoka na kuanza kuhubiri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news