NHC kuvunja mikataba na wapangaji waliokaidi kulipa madeni, kukamata mali

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limesema linakusudia kuvunja mikataba ya upangaji kwa wapangaji waliokaidi kulipa madeni yao na kuwaondoa kwenye nyumba ikiwemo kukamata mali zao kwa ajili ya kuuza ili kufidia madeni yao.
Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Muungano Saguya (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko, Bi.Joyce Luhanga,Afisa Uhusiano Mkuu wa NHC, Yahya Charahani na Meneja Mauzo na Masoko, Bw.Ernest Dilli baada ya kumaliza mazungumzo wakati wa ziara katika vyombo vya habari vya IPP Mikocheni jijini Dar es Salaam leo Januari 9, 2023.

Hayo yamesemwa leo Januari 9, 2023 kwa nyakati tofauti na Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Muungano Saguya katika ziara ya vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kuvishukuru kwa namna ambavyo vimekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi mbalimbali za shirika hilo.

Ziara hiyo ambayo ilianzia katika Kampuni ya IPP Media inayomiliki magazeti ya Nipashe, The Gurdian, runinga za Independent Television (ITV), Capital TV, Capital Redio,East Africa TV, Radio One na East Africa Redio huko Mikocheni jijini Dar es Salaam iliwakutanisa maafisa wa NHC na Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko, Bi.Joyce W.Luhanga na Meneja Mauzo na Masoko, Bw.Ernest H.Dilli.
Pia, maafisa hao wa NHC walifanya ziara Clouds Media Group ambao wanamiliki runinga ya Clouds na Redio Clouds karibu na Barabara ya CocaCola huko Mikocheni jijini Dar es Salaam ambapo waliteta na Meneja Rasilimali Watu na Utawala, Bw.Elikimbilio Kitoi.

Katika hatua nyingine, ziara hiyo iliendelea katika E-FM Company Limited ambao ni wamiliki wa TV E na E FM Redio iliyopo Mtaa wa Nachingwea huko Mbezi Beach jijini Dar es Salaam na kutetea na Mkurugenzi wa Maendeleo na Uzalishaji, Geoffrey Ndawula Kisekka.

Wakati huo huo, maafisa wa NHC walifanya ziara Wasafi Media Group ambao ni wamiliki wa Wasafi Fm na Wasafi Tv huko Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ambapo waliteta na Meneja Vipindi, Bw.Innocent Sanga.

"Tunaendelea kukusanya madeni ya kodi ya nyumba yanayofikia shilingi bilioni 21 na madeni mbalimbali yatokanayo na uuzaji wa nyumba na viwanja yanayofikia shilingi bilioni 11.1.

"Msisitizo utakuwa kuhakikisha kuwa kila anayedaiwa analipa deni lake ili kuliwezesha shirika kuendelea kuwahudumia Watanzania wote kwa kutumia rasilimali hizi za umma.
Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Muungano Saguya (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Meneja Rasilimali Watu na Utawala Clouds Media Group, Bw.Elikimbilio Kitoi na kushoto ni Afisa Uhusiano Mkuu wa NHC, Yahya Charahani baada ya kumaliza mazungumzo wakati wa ziara katika makamo makuu ya Cloud Media jijini Dar es Salaam leo Januari 9, 2023.

"Aidha, kwa wapangaji ambao walishapewa notisi mbalimbali utekelezaji unaendelea kama notisi hizo zinavyoelekeza. Na shirika linaendelea na hatua mbalimbali ikiwemo kuingia mikataba na wapangaji ya kuwaruhusu kulipa madeni yao kwa awamu,"amefafanua Saguya.

Pia amesema, katika kampeni ya miezi miwili iliyofanywa na shirika ya kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa sugu wanaodaiwa malimbikizo ya kodi hadi sasa shirika limeweza kukusanya kiasi cha shilingi bilioni tano.

Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko, Bi.Joyce Luhanga na Meneja Mauzo na Masoko, Bw.Ernest Dilli wameelezea kuguswa na heshima ya kipekee waliyopewa na shirika hilo kwa kufika kuwasalimu huku wakiwaelezea mikakati waliyonayo kwa ajili ya kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili kufikisha taarifa kwa umma.

"Hii ni heshima ya kipekee kwetu sisi IPP, tutaendelea kushirikiana nanyi ili kuhakikisha mnafanikisha malengo yenu ya kutoa huduma za makazi bora kwa umma,"amefafanua Bi.Luhanga.

Naye Bw.Dilli amesema, vyombo hivyo vya habari vina uwanda mpana na vinawafikia watu wengi kwa wakati mmoja, hivyo ushirikiano baina ya NHC utawezesha kuongeza thamani katika huduma na miradi wanayotekeleza.

Bw. Saguya aliwaeleza kuwa, dhumuni la ziara hiyo ni kuwashukuru kwa namna ambavyo vyombo vyao vya habari vimeendelea kuwa na mchango chanya kwa shirika.

Amesisitiza kuwa, NHC inathamini vyombo vyote vya habari kuanzia magazeti, redio, runinga na mitandao ya kijamii, hivyo wataendelea kushirikiana navyo popote pale nchini ili kuhakikisha vinawapa taarifa wananchi waweze kufahamu yale ambayo yanatekelezwa na shirika lao ikiwemo miradi mbalimbali.

Aidha, amesema kutokana na ushirikiano ambao uongozi wa shirika uliupata kutoka vyombo vya habari nchini kwa mwaka uliopita 2022, shirika lilipata mafanikio makubwa.
Meneja huyo amefafanua kuwa, katika kipindi cha mwaka 2022 Shirika la Nyumba la Taifa liliendelea na ajenda ya kuwapatia Watanzania makazi bora na yenye staha kama lilivyoelekezwa na Serikali na chama tawala.

Miradi ya Ukandarasi 2022

Amefafanua kuwa,shirika mwaka jana liliendelea na utekelezaji wa miradi ya ukandarasi ikiwemo ujenzi wa majengo ya ofisi za wizara nane jijini Dodoma (awamu ya pili).

"Miradi hii itakapokamilika itagharimu jumla ya shilingi bilioni 186.83, Miradi hiyo ya ujenzi ni pamoja na ile ya makao makuu ya Wizara ya Madini, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Nishati na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

"Ukamilishaji wa miradi hii unaendelea na inatarajiwa kukamilika Juni, mwaka huu. Aidha, Shirika liliendelea na ujenzi wa jengo la Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,ujenzi wa majengo matano ya Wakala wa Ununuzi wa Serikali (GPSA), ujenzi wa jengo la TANZANITE Mirerani, ujenzi wa jengo la Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete (JKCI),"amefafanua Meneja huyo.

Kwa upande wa ujenzi wa nyumba za makazi, amefafanua kuwa, shirika liliendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa nyumba 5,000 za gharama ya kati chini za mradi wa Samia Housing Scheme (SHS).

"Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Mheshimiwa Rais na tunatamani Watanzania waje wamkumbuke kwa miaka mingi ijayo. Asilimia 50 ya nyumba hizi zitajengwa Dar es Salaam, Dodoma asilimia 20 na mikoa mingine asilimia 30.

"Nyumba hizi zimeanza kujengwa mwezi Septemba eneo la Kawe Dar es Salaam (nyumba 400). Mradi huu utakaotekelezwa kwa awamu utagharimu takribani shilingi bilioni 466 sawa na dola za Kimarekani milioni 200.

"Kadhalika, shirika lilikamilisha ujenzi wa nyumba 300 eneo la Iyumbu jijini Dodoma na nyumba 100 eneo la Chamwino. Nyumba hizi ni kwa ajili ya kuuzwa na zinaendelea kuuzwa.

"Aidha, kazi ya kukamilisha mradi wa Morocco Square uliokuwa umesimama ilifanyika kwa ukubwa wake na kazi hiyo ipo katika hatua za mwisho za kuukamilisha,"amefafanua Saguya.

Sera ya Ubia

Wakati huo huo, Saguya amesema kuwa, shirika limeweza kuhuisha, kuitayarisha na kuizindua sera ya ubia ili kushirikisha wadau mbalimbali kuendeleza sekta ya makazi na kuongeza makazi bora kwa ajili ya Watanzania.
Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Muungano Saguya (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo na Uzalishaji E-FM Company Limited, Geoffrey Ndawula Kisekka kushoto ni Afisa Uhusiano Mkuu wa NHC, Yahya Charahani baada ya kumaliza mazungumzo wakati wa ziara katika makamo makuu ya E FM Mtaa wa Nachingwea huko Mbezi Beach jijini Dar es Salaam leo Januari 9, 2023.

"Sera hiyo ilizinduliwa rasmi Novemba 16 mwaka 2022 na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb). Uzinduzi wa Sera ya Ubia unaenda kufungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba na kwa hakika tunaunga mkono maono na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuvutia uwekezaji nchini kwa kuruhusu sekta binafsi ambayo ni injini ya kujenga uchumi imara wa Taifa letu."

Mwaka 2023

Saguya amefafanua kuwa, kwa mwaka huu shirika limejipanga kuendelea kutekeleza mipango mbalimbali ikiwemo kuendelea kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Morocco square ambao ujenzi upo kwenye hatua ya uboreshaji wa mandhari (landscaping na ufungaji wa lifti na viyoyozi) ili kuweza kupangisha na kuuza nyumba za mradi huo.

Pia shirika hilo, linaendelea na utekelezaji wa mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) katika eneo la Medeli jijini Dodoma ambapo nyumba 100 zitajengwa kwa ajili ya kuuza.

"Na tutaendelea na ujenzi wa Shopping Mall kubwa jijini Dodoma ili kuweza kuwapa wakazi wa Jiji hilo eneo zuri na kubwa la kujipatia huduma mbalimbali za kijamii,"amefafanua Saguya.

Amesema,wataendelea kutekeleza miradi ya ubia kwa kushirikiana na sekta binafsi kadri itakavyokuwa imepitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa.

"Kuendelea kusimamia miliki ya nyumba za shirika zipatazo 18,622, kwa kuzifanyia matengenezo ipasavyo kupitia Mpango wa Matengenezo ya nyumba wa miaka mitano (2021/22-25/26). Ukarabati mkubwa utakaohusisha kubadilisha paa, vyoo na madirisha chakavu,"amefafanua Bw.Saguya.

Wakati huo huo amesisitiza kuwa, wataendelea kujenga mahusiano yenye tija na wabia na taasisi mbalimbali yakiwemo mashirika, Bunge, Serikali na vyombo mbalimbali vya sheria ili kuweza kupata manufaa kwa shirika.

"Pia kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali ili kurahisisha utekelezaji wa miradi yetu hususan ushiriki wao wa kuweka miundombinu muhimu ya barabara, maji na umeme katika maeneo ya ujenzi. Na kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari kama mhimili muhimu wa upashanaji habari kwa wananchi, uelimishaji na kujenga taswira ya shirika,"amefafanua Bw.Saguya.

Kwa upande wao Meneja Rasilimali Watu na Utawala Clouds Media, Bw.Elikimbilio Kitoi,Mkurugenzi wa Maendeleo na Uzalishaji E-FM Company Limited, Geoffrey Ndawula Kisekka,Meneja Vipindi Wasafi Media, Bw.Innocent Sanga wamefafanua kuwa, wataendelea kushirikiana na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati wowote ili kuhakikisha malengo yake hususani ya kujenga makazi bora na miradi mbalimbali nchini inafanikiwa na jamii inafahamu ilipo.

Shirika la Nyumba la Taifa lilianzishwa mwaka 1962 kwa Sheria Na.45 likiwa na jukumu la kuwezesha ujenzi wa nyumba na majengo mengine kwa matumizi mbalimbali hususani makazi,ofisi na biashara.
Mwaka 1990 shirika liliunganishwa na iliyokuwa Msajili wa Majumba (Rob) iliyoanzishwa mwaka 1971 kwa Sheria Na. 13 ili kusimamia majumba yaliyotwaliwa na Serikali.

Aidha,ili kulifanya shirika kujiendesha kibiashara mapitio ya Sheria ya NHC ya mwaka 1990 na Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999 yalifanyika mwaka 2005 kupitia Sheria Na. 2.

Majukumu ya shirika yanatekelezwa kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Shirika wa Miaka 10 (2015/16-2024/25) ambao unalenga kusukuma mbele ujenzi wa nyumba zipatazo 10,000 na kuwezesha ukuaji wa sekta ya nyumba kupitia ushirikishwaji wa sekta binafsi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news