Rais Dkt.Mwinyi atoa salamu za mwaka mpya wa jadi kwa Wachina,asisitiza jambo

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za mwaka wa jadi wa China kwa Wachina wote wakati wanakaribisha mwaka mpya wa jadi wa Sungura.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa salamu hizo kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter leo Januari 21, 2023 huku akisisitiza Zanzibar imejizatiti kuendeleza na kukuza uhusiano imara baina ya pande hizo mbili.

"Ninawatakia kila la kheri wale wote wanaosherehekea mwaka mpya wa Kichina, ninawatakia mafanikio na fanaka tele katika mwaka wa Sungura. 
 
"Zanzibar imejizatiti kuendelea kukuza uhusiano imara na ushirikiano ili kutafuta fursa zisizoweza kupimika zinazopatikana kwa mataifa yote mawili kwa ajili ya ustawi wa pamoja,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Hivi karibuni,Balozi Mdogo wa China huko Zanzibar, Mheshimiwa Zhang Zhisheng katika kumbukizi ya miaka 50 ya Sheikh Abeid Amani Karume alibainisha kuwa, uhusiano kati ya pande hizo mbili una historia ndefu na mvuto wa kipekee.

Alibainisha kuwa, Sheikh Karume alikuwa rafiki wa dhati wa Wachina. Alivutiwa na Mwenyekiti Mao Zedong na Waziri Mkuu Zhou Enlai na kuunga mkono mfumo wa kisiasa wa kijamaa wa China.

Pia,alitoa mchango mkubwa katika uhusiano wa kirafiki kati ya China na Tanzania. Alithamini sana msaada uliotolewa na serikali ya China bila malengo yoyote ya ubinafsi au hali ya kisiasa.

Kwa moyo mkunjufu, Hayati Sheikh Karume aliwaalika wahandisi, madaktari, wataalamu wa kilimo na viwanda kutoka China kwenda Zanzibar.

Alisema mara nyingi kwamba China ni rafiki wa kweli wa Zanzibar, na China daima itatoa mkono wa kusaidia pale inapohitajika zaidi.

Alifurahi kukutana na karibu kila mtaalam wa Kichina aliyefika Zanzibar au anayekaribia kuondoka. Mara nyingi aliwaongoza mawaziri wa serikali ya Zanzibar katika kazi za kujitolea na wataalamu wa China na wakazi wa eneo hilo, kama vile kukata minazi, kuondoa vigogo vya miti ili kuunda maeneo ya ujenzi kwa ajili ya miradi ya misaada ya China kama vile kiwanda cha kutengeneza ngozi na viatu.

Mara kwa mara alitembelea timu za madaktari wa China na timu za ujenzi kwa ajili ya huduma ya maji, viwanja vya michezo, mashamba na karakana ya dawa ili kuhakikisha wanasaidiwa na serikali ya Zanzibar kwa mazingira stahiki ya kazi na maisha. Mara kwa mara aliwapongeza wataalamu wa China kwa kutoa msaada wa mradi na mafunzo ya kiufundi na kuonyesha bidii na kujitolea kwa vijana wa Zanzibar.

"Tunapotazama nyuma kwenye historia yetu, tunaweza daima kujifunza mengi kutoka kwa siku zilizopita, kuelewa sheria za historia, na kusonga mbele kwa ujasiri na nguvu. Ni miaka 50 tangu Sheikh Karume atutoke. Ingawa dunia imepitia mabadiliko makubwa sana na Tanzania imeingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa, urithi wa Sheikh Karume umekuwa zaidi ya siasa za chama chochote, na ni mali ya Watanzania wote.

"Mheshimiwa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi amerithi urithi wa kiroho ulioundwa na Sheikh Karume. Tangu siku yake ya kwanza madarakani, ameweka mbele maslahi ya Wazanzibari wote. 
 
"Amekuwa akiulinda kwa uthabiti Muungano wa Tanzania, akifanya kazi kwa bidii ili kuimarisha mshikamano na maelewano miongoni mwa jamii ya Zanzibar, kuzingatia maendeleo ya uchumi, kuimarisha miundombinu, kuboresha maisha ya watu, kulinda utamaduni na urithi ambao umepata ridhaa na kuungwa mkono na Umoja wa Wananchi,"alifafanua Mheshimiwa Zhang Zhisheng.

Post a Comment

0 Comments