RC Meja Jenerali Mzee:Wote wakamatwe, haya mambo ni marufuku ndani na nje ya Mara

NA FRESHA KINASA

MKUU wa Mkoa wa Mara,Meja Jenerali Suleiman Mzee ameliagiza Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime-Rorya kuwakamata wazazi wa wasichana (watoto wa kike) 70 katika Wilaya ya Tarime ambao wamewakeketa watoto wao ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Pia, amelitaka jeshi hilo kuwakamata viongozi wa vijiji na vitongoji wa maeneo ambako watoto hao wamekeketwa kwa kushindwa kuwajibika kama viongozi kudhibiti vitendo hivyo katika maeneo yao.

Meja Jenerali Mzee ametoa agizo hilo Januari 10, 2022 akiwa katika Kituo cha ATFGM Masanga kinachotoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji kilichopo Kata ya Gorong'a wilayani Tarime mkoani humo.

Amesema kuwa kitendo cha wazazi kuwakeketa watoto hao ni kinyume cha sheria na kwamba Serikali haiwezi kuwafumbia macho hata kidogo wahusika wote waliofanya ukatili huo kinyume cha sheria za haki na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

"Msimu wa ukeketaji ulikuwa unaisha lakini wazee wa kimila wameongeza muda wa kukeketa, tulifika kituo cha Masanga decemba 24, 2022 kuleta salamu za Mheshimwa Rais tulikuta watoto walikuwepo zaidi ya 400. Na katika Mkoa mzima kulikuwa na wasichana 750 ambao walikuwa katika vituo vyote," amesema Meja Jenerali Mzee na kuongeza kuwa.

"Cha ajabu wasichana 70 waliokuwa hapa Masanga wamerudi nyumbani wazazi wao wamewakeketa, naomba polisi muwakamate wazazi hawa na wafikishwe mahakamani. Haiwezekani hawa watoto wamekeketwa na hakuna mzazi aliyekamatwa yuko polisi ama mahakamani na viongozi wa wilaya mpo, katibu tawala yupo na viongozi wa mitaa wapo. Ukeketaji ni kinyume na sheria za nchi na Ilani ya CCM sura ya tatu imekemea udhalikishaji huu. lazima wadau na viongozi wote tushirikiane kuumaliza,"amesema Meja Jenerali Mzee.

Amesema, majina ya wazazi waliowakeketa watoto hao yapo na tayari yamekabidhiwa kwa kamanda wa Polisi Tarime -Rorya na kwamba kitakachofuata ni kuwakamata viongozi wa maeneo husika ambako ukeketaji unafanyika.

"Bila kuchukuliana hatua ukeketaji hauwezi kuisha, lazima tukamate kama ni baba ama mama ngariba wanaofanya hivi kwa nini hawakamatwi? na ukeketaji unafanyika kwa sherehe kabisa Viongozi wapo hawachukui hatua kudhibiti jambo hili. Serikali haiwezi kuwafumbia macho watu ambao wanafanya mila hii mbaya kutokana na madhara yake." amesema Meja Jenerali Mzee.

Aidha, Meja Jenerali Mzee, ameyataka mashiriki yasiyo ya kiserikali (NGOs) mkoani Mara yanayojishughulisha na mapambano ya ukatili wa kijinsia kufanya kazi kikamifu kumaliza tatizo la ukeketaji kwani licha ya uwepo wa mashirika hayo vitendo hivyo bado vina zidi kufanyika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Patrick Chandi akizungumza katika Kituo cha Nyumba Salama cha Anglican wilayani Serengeti amesema, Chama Cha mapinduzi kinaendelea kupinga mila hiyo na kwamba, ukeketaji ni ukatili ambao haufai kuendelea kufanywa. Hivyo wanaofanya ukeketaji waache waache.

"Jambo hili liwe shirikishi chama, Serikali na wadau wote kwa pamoja unajua binti anapokeketwa anakuwa sokoni kwa mila za kikurya hivyo jambo hili sote tuungane pamoja kuweza kulimaliza,"amesema Chandi.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee ametembelea Kituo cha Masanga wilayani Tarime, Kituo cha Kanisa la Anglican Wilayani Serengeti na Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama. Ambapo amesema kwa sasa wanofanya ukeketaji wakibainika ni kufikishwa mahakamani na si vinginevyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news