ADA:Mjadala mkubwa Januari, huu hapa mtazamo chanya

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

MAZUNGUMZO na mijadala mbalimbali kuhusiana na suala la ada hupamba moto kila ifikapo mwezi Januari kila mwaka. Kimsingi, mjadala huanza tangu mwezi Disemba na shule zinapofunguliwa mwezi Januari mjadala hupamba moto.
Kwa fasili ya haraka haraka, ada ni malipo yanayolipwa kwa ajili ya kupatiwa huduma na katika muktadha wa shule, ada hulipwa ili mwanafunzi aweze kupatiwa huduma za masomo, malazi na chakula.

Ada hulipwa kwa awamu kulingana na mihula na makubaliano baina ya shule na mzazi, mlezi au mfadhili wa mwanafunzi.

Kiini cha Mada

Baada ya usuli huo mfupi, ni vema pia kufahamu katika nchi ya Tanzania ada hulipwa katika shule za binafsi na shule umma elimu hutolewa bila ada.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa Elimu bila ada kuanzia ngazi ya awali, msingi, sekondari na sekondari za juu.

Hivyo kwa wazazi ambao huwapeleka watoto wao kwenye shule za umma wao hawazungumzii ada bali huzungumzia maandalizi ya msingi kwa mwanafunzi kama vile sare, daftari, kalamu, viatu na begi la kuweka daftari.

Kwa mnasaba huo nimeona ni vema kutoa maoni yangu juu ya suala la mjadala wa ada katika kipindi cha mwezi Januari kwa mtazamo chanya kama ifuatavyo:

Mosi: Mwamko mkubwa wa Watanzania katika Elimu. Mjadala mkubwa wa ada katika kipindi cha mwezi Januari ni ishara kwamba Watanzania wana mwamko mkubwa kuhusiana na Elimu kwa watoto wao na ndio maana mjadala unapamba moto katika kipindi hiki cha mwezi Januari.

Hii ni naiona ni mwamko kwa sababu hata pale inapotokea mzazi ama mlezi au mfadhili amekwama au amepungukiwa fedha za ada hufika shuleni na kuomba apewe muda kisha atalipa kiasi hicho.

Nimepitia katika mitandao ya kijamii, nimeona baadhi ya watu wakiweka picha za watu ambao wamelowa jasho, nguo zikitiririsha maji kwa madai kwamba wametoka ofisini kwa Mkuu wa shule kuomba watoto wao wapokelewe na kuanza masomo na wazazi hao waendelee kutafuta fedha za ada wakalipe baadae.

Huu unaweza kuwa ni mzaha lakini mimi ninaona ni hatua nzuri ya wanajamii kutambua umuhimu wa elimu na kuhakikisha watoto wanapokelewa shuleni hata kama bado hawajalipiwa ada na pindi wanapoendelea na masomo wazazi na walezi wanatafuta fedha za ada.

Pili: Elimu ni Uwekezaji, mjadala mkubwa kuhusu ada za shule katika kipindi cha mwezi Januari ni ishara kwamba Watanzania walio wengi wametambua kwamba elimu kwa watoto ni uwekezaji muhimu katika kujiletea maendeleo ya kweli. Mjadala wa ada ni uthibitisho kwamba wapo tayari kulipa ada na michango mingine ili watoto wao wapate elimu kwa maendeleo yao binafsi, familia na taifa kwa jumla.

Tatu: Msisitizo kwamba watoto lazima wapate elimu. Kuna picha moja huwa inasambaa mtandaoni ikimuonesha mtu ambaye anatajwa kuwa ni mzazi au mlezi ameweka kiganja cha mkono wake mezani vidole vikiwa vimenyanyuka juu akipiga meza kwa vidole hivyo.

Hii ni ishara ya msisitizo kwamba mwanafunzi apokelewe bila ada au ada pungufu na mzazi aendelee kutafuta fedha.

Natumai wasomaji wa mitandaoni watakuwa wanaufahamu mfano huu vizuri sana na watakaposoma pointi hii wataushare huo mfano wa mkono kuwekwa mezani kwa msisitizo kwamba mtoto apokelewe aendelee na masomo.

Nne: Uwajibikaji katika elimu ya watoto, kwa maoni yangu naona kwamba, mjadala wa ada kupamba moto katika kipindi cha mwezi Januari ni ishara ya uwajibikaji wa Watanzania katika Elimu ya watoto wao.

Kama si uwajibikaji basi kusingalikuwa na mjadala wa ada bali mwezi wa Januari ungepita kimyakimya.

Tunawaona hata wazazi ambao wanapeleka watoto wao kwenye shule za umma nao pia wakiwajibika katika kutafuta mahitaji wa shule ya watoto wao. Mjadala wa ada ni ishara ya uwajibikaji wa Watanzania katika Elimu ya watoto wao.

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinapata faraja kubwa kuona mwamko kuhusu elimu kwa wanajamii ukishamiri kila siku.

Lengo la kuanzishwa chuo hiki ni ili kutoa fursa pana kwa Watanzania kupata elimu ya juu popote pale walipo bila kipingamizi chochote.

Mwamko wa elimu kwa wazazi na bila shaka wanafunzi wa ngazi za msingi na sekondari ni chachu ya kufikia elimu ya juu.

Hivyo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kipo tayari kabisa kuwapokea wanafunzi wote ambao wanahitimu katika ngazi za sekondari wakiwa tayari wamejiajiri, wameajiriwa au bado katika mawili haya. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinatambua kwamba, kadri nchi inavyokuwa na wasomi wengi ndivyo ubunifu na ugunduzi nao hukuwa na kuleta maendeleo nchini.

Hitimisho

Dodoo hizi nne ni miongoni mwa faida nyingi za mjadala wa ada katika kipindi cha mwezi Januari. 

Hata hivyo, wapo baadhi ya wazazi wachache ambao hawajauona umuhimu wa elimu kwa watoto, tunawasihi sana kuhakikisha wanawapeleka watoto shule.

Serikali inatoa elimu bila malipo na hivyo hakuna sababu ya mtoto kukosa elimu kwa kisingizio cha kukosa ada.

Wale ambao hatuna fedha za ada tuwapeleke watoto wetu kwenye shule za serikali elimu bila ada kwa Watanzania wote.

Kikubwa zaidi, tuendelee kulipa kodi na kuhamasishana kulipa kodi ili serikali iendelee kutoa elimu bila ada na watoto wote wa Tanzania waendelee kupata elimu kwa maendeleo ya taifa letu.

Insha za Maendeleo nchini Tanzania

MWANDISHI

Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news