RC Mtaka:Tena wazazi wafanye usafi hapa huku watoto wakiwa wanaona

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Njombe,Mheshimiwa Anthony Mtaka amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa kuwakamata wazazi wote ambao hawajapeleka watoto kuanza muhula mpya wa masomo na kuwafanyisha usafi kwenye shule hizo.

Sambamba na vituo vya afya badala ya kuwaweka rumande. “Tena wazazi wafanye usafi hapa huku watoto wakiwa wanaona.”

Mheshimiwa Mtaka ametoa agizo hilo akiwa katika Shule ya Sekondari Mbeyela Mjini Njombe wakati akikagua zoezi la kuripoti wanafunzi shuleni ambapo katika shule hiyo wameripoti wanafunzi 62 pekee kati ya 300 wa kidato cha kwanza wanaopaswa kuanza masomo.

"Hatuwezi kuruhusu ujinga kwenye suala la elimu nikuagize DC wa Njombe kamata wazazi wote ambao hawajawaleta wanafunzi shuleni, beba magari ya polisi yote wapakiwe humo ili waje mashuleni kufanya usafi wa vyoo na madarasa."

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema hakuna sababu ya kuwapeleka rumande wazazi hao wakamalize chakula cha Serikali, hivyo wanapaswa kufanya usafi, kwani haiwezekani Serikali ikajenga madarasa na kufuta ada halafu wazazi washindwe kuwapeleka watoto shuleni.

Aidha, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mbeyela, Mwalimu Jimmy Ngumbuke amesema kasi ya wanafunzi kuripoti shuleni ni ndogo na hivyo jitihada zaidi zinahitajika kwa wazazi ili wote waweze kuripoti.
Hatua hiyo inakuja ikiwa pia awali, RC Mtaka aliwataka wazazi na walezi wenye watoto waliofikia umri wa kuanza darasa la kwanza kuwapeleka shule Januari 9, 2023.

Akizungumza na wafanyabiashara wa Mkoa wa Njombe kwenye Baraza la Saba la Wafanyabiashara lililofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe tarehe 5 Januari 2023, RC Mtaka alisema lazima mzazi atambue umuhimu na haki ya mtoto kupata elimu katika mazingira rafiki na kupewa vifaa vyote muhimu kwa mahitaji ya elimu.

RC Mtaka aliongeza kuwa, Serikali imejenga madarasa katika shule mbalimbali zilizokuwa na upungufu hivyo hakuna haja ya mzazi au Mlezi kumkosesha haki ya elimu mtoto.

Pia aliwataka wazazi na walezi kuwanunulia vifaa vya shule watoto wao na hata ambao watashindwa wahakikishe watoto wanapelekwa shule kuanza masomo.Hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde alisema wanafunzi 1,073,941 waliochaguliwa kidato cha kwanza 2023 wataanza shule kwa wakati mmoja nchini kote.

Hatua hiyo inafanya kusiwepo na utaratibu wa chaguo la pili (second selection) kama ilivyozoelekea kutokana na kukamilika kwa madarasa 8,000.

Dkt. Msonde aliyasema hayo wilayani Kongwa mkoani Dodoma wakati wa zaiara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa.

Alisema, hakutakuwa na changuo la pili kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza Januari hii na kuwasihi wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti shuleni kwa wakati.

"Kwa mwaka huu hakutakuwa na second selection (chaguo la pili la wanafunzi) kwa sababu fedha zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya elimu zimetosha kuboresha miundombinu ya kuwachukua watoto wetu wote kwa intake (mkupuo) mmoja."

Alisema, tangu Rais aingie madarakani ameshatoa fedha zilizowezesha kujenga zaidi ya vyumba vya madarasa 20,000 ndani ya miaka miwili hatua ambayo imewaondolea adha watoto kwa kuanza masono kwa pamoja huku wazazi wakiwa hawajachangishwa kitu.

Katika kukabiliana na ongezeko la wanafunzi kwa mwaka huu ametoa shilingi bilioni 160 zilizotumika kujenga madarasa 8,000.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news