TAKUKURU yawafikisha mahakamani aliyekuwa DED na Mtunza Hazina wa Halmashauri ya Ruangwa

NA DIRAMAKINI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi imewafikisha mahakamani aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Reuben Mfune (58) na aliyekuwa mtunza hazina wa halmashauri hiyo, Juma Masatu (56) kwa tuhuma ya kuisababishia hasara mamlaka.

Akiwasomea mashitaka Januari 11, 2023, mwendesha mashitaka wa Serikali, Peter Camilius amesema wawili hao wameisababishia hasara Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa jumla ya shilingi 51,792,615.

Ni kutokana na kuvunja mkataba na mzabuni ambaye aliteuliwa kufanya kazi ya kuchimba visima 11 vya maji katika baadhi ya vijiji vilivyopo katika halmashauri hiyo ya wilaya ya Ruangwa.

Mwendesha mashitaka huyo katika shauri hilo la uhujumu uchumi namba 1 la mwaka 2023 linalosikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa, mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Mariam Mchomba amesema Januari 2,2014 Halmashauri ya Ruangwa ilipokea shilingi milioni 200 kutoka kwa Katibu Mmkuu wa Hazina. Ambapo fedha hizo zilipokelewa na kuwekwa kwenye akaunti ya maendeleo katika benki ya NMB namba 71101200032.

Amesema kiasi hicho cha fedha ambacho ilibidi kitumike kwa ajili ya kuchimba visima 11 vya maji katika vijiji vya Nandenje, Mtakuja, Matambarale, Ng'alile, Nandanga, Namahema, Namakuku, Likunja, Mbangala, Namilema na Mkaranga hazikutumika kwa kusudio lililokuwa limekusudiwa.

Badala yake takribani shilingi milioni 192 zilifanyiwa matumizi mengine. Alibainisha kwamba kitendo hicho kilisababisha mkandarasi ambaye ni kampuni ya Maswi isilipwe shilingi milioni 182.7. Kitendo ambacho ni kinyume cha mkataba baina ya kampuni hiyo na halmashauri ya wilaya ya Ruangwa ulioingiwa Novemba 26,2014.

Hali ambayo ilisababisha mkandarasi huyo kuishitaki halmashauri ya wilaya ya Ruangwa. Alisema halmashauri hiyo iliomba shauri hilo lizungumzwe na kumalizwa nje ya mahakama. Jambo ambalo lilifanyika na kusababisha halmashauri iilipe kampuni ya Maswi shilingi milioni 247.4 badala ya shilingi milioni 182.7.

Kwa hiyo ikalazimika kuongeza na kupata hasara ya shilingi milioni 51.7. "Na walitenda kitendo hicho cha kutumia fedha kinyume cha matumizi yaliyokusudiwa kati ya Oktoba 2,2014 na Desemba 31,2014," alisema Camilius.

Mwendesha mashitaka huyo aliieleza mahakama kwamba kitendo kilichofanywa na watumishi hao wa umma ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 10(1) jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, sura ya 200 mapitio ya mwaka 2002.

Kwa upande wao, washitakiwa hao wanaotetewa na wakili Sia Ngowi wa Mafuru Company&Advocate Ltd walikana mashitaka hayo.

Ambapo mahakama imepanga kuanza kusikikiza shauri hilo Februari 7,2023. Huku wakiwa nje kwa dhamana baada ya kutekeleza kikamilifu masharti ya dhamana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news