Serikali, CCM yapewa kongole Rufiji kwa usimamizi bora wa miradi

NA JOHN MAPEPELE

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu CCM Taifa ndugu Fadhili Rajabu Maganya amepongeza jitihada za Serikali na Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa za kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo huku akiwataka wataalam kusimamia na kutekeleza miradi kwa wakati ili kupata matokeo tarajiwa.
Mwenyekiti, Maganya ametoa pongezi hizo leo wakati wa ziara yake ya kwanza anayoifanya kwenye Mkoa wa Pwani kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwa pia ni maadhimisho ya kutimiza miaka 46 ya Chama Cha Mapinduzi.

Pamoja na wadau wengine, ndugu Maganya amemtunikia Mhe. Mchengerwa hati ya shukrani kwa kutambua mchango wake mkubwa anaoutoa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo la Rufiji.

Aidha, ameupongeza Mkoa wa Pwani kwa kuonyesha mshikamano na ushirikiano kwenye jumuiya zote za chama katika kuwatumikia wananchi huku akiitaka mikoa yote kuiga mfano huo.

Amewataka watendaji wa Chama Cha Mapinduzi katika ngazi zote nchini kuwa na nidhamu katika kusimamia fedha zote za miradi zinazotolewa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi huku akisisitiza kuwa wao ndiyo jicho la chama katika ngazi husika.
Pia amewaelekeza kupokea kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi wa changamoto hizo ili wananchi waendelee kuwa na Imani na chama chao

“Ninawapa makali ya kusimamia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, lakini jambo la kwanza ni kusimamia kero,” amesisitiza Mwenyekiti Maganya.

Mbali na hayo, amewahimiza wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kukisemea chama hicho mambo makubwa ya kimaendeleo ambayo yamefanyika katika kipindi hiki kifupi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC) wa Mkoa wa Pwani, na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameishukuru Serikali chini ya Rais Samia kwa kutekeleza miradi mbalimbali kwa wananchi wa Rufiji.
Ametaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kwa mafanikio makubwa katika jimbo hilo kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, vituo vya afya ikiwa ni pamoja na jengo jipya la kutolea huduma ya mionzi la hospitali, shule na upatikanaji wa umeme takribani katika vijiji vyote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news