Serikali yafanya tahmini Sherehe Miaka 59 ya Mapinduzi

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ameongoza kikao cha Tathmini ya Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil-Kikwajuni jijini Zanzibar.
Katika kikao hicho, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa kufanikiwa kwa maadhimisho hayo kunatokana na ushirikiano waliokuwa nao Wajumbe wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa katika kusimamia miongozo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyoielekeza katika kusimamia maadhimisho hayo.

Mhe. Hemed amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyosimamia maendeleo ya watanzania kadhalika viongozi Wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Viongozi Wakuu Wastaafu kwa ushiriki wao mzuri kwenye matukio mbalimbali ya maadhimisho hayo.

Sambamba na ameishukuru Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa, Sektretarieti, Viongozi wa Wizara, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wananchi kwa ujumla kwa kushiriki kikamilifu katika kufanikisha sherehe hizo.

Mhe. Hemed ameeleza kuwa katika maadhimisho hayo jumla ya miradi thalathini na tano ilizinduliwa na miradi kumi na tisa iliwekewa mawe ya msingI hatua ambayo imeakisi dhamira ya mapinduzi ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Aidha Mhe. Hemed amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa Jitihada zao kuhakikisha amani na utulivu inaimarika kipindi chote cha Maadhimisho hayo.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa kukamilika kwa sherehe hizo ni matayarisho ya kuelekea Sherehe za kutimia Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameahidi kuzinduliwa miradi mikubwa Zaidi ya maendeleo katika Sherehe zijazo.

Nae Katibu Mkuu Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dkt. Islam Seif Salum ambaye pia ni Katibu wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ameeleza kuwa Sherehe za kutimia Miaka Hamsini na Tisa ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka huu hazikutumia fedha za Serikali badala yake Taasisi na Mashirika wameweza kufanikisha Sherehe hizo.

Aidha amesema Fedha iliyotengwa katika Sherehe hizo zimeelekezwa katika Sekta ya Elimu kununulia Vifaa vya majengo yaliyozinduliwa ili kuhakikisha elimu inapatikana bila ya kikwazo chochote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news